Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuanzia tarehe 24-25 Oktoba 2019 limeadhimisha Warsha: Kauli mbiu "Uchumi jamii na wa soko wa kuwajengea vijana uwezo" Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuanzia tarehe 24-25 Oktoba 2019 limeadhimisha Warsha: Kauli mbiu "Uchumi jamii na wa soko wa kuwajengea vijana uwezo" 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Warsha ya uchumi kwa vijana 2019

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuanzia tarehe 24-25 Oktoba 2019 limeendesha Warsha iliyokuwa inaongozwa na kauli mbi "Uchumi jamii na wa soko wa kuwajengea vijana uwezo". Wawezeshaji wamegusia: TEHAMA; Misingi ya uchumi imara; Vijana, imani na ushiriki wao katika uchumi; Nafasi ya ujasiriamali; Mitandao ya kijamii na umuhimu wa kanuni maadili na utu wema.

Na Padre Adolf Bernard Minga, - Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, DSM.

Utangulizi na utambulisho: Padre Daniel Dulle, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kwa niaba ya Katibu Mkuu aliwakaribisha wajumbe na kuwashukuru pia waandaaji kwa kuwapatia vijana fursa ya kujifunza. Alianza kwa sala na kisha kusomo neno la Mungu kutoka kwa 1Wafalme 3:8-15. Kwa niaba ya TEC nawakaribisha sana kwenye warsha ya kuwajengea uwezo.  Mafunzo haya yawasaidie katika kutelekeza wajibu kama mtu mmoja na kama taifa kwa ujumla. Tunawashukuru wafadhili wa warsha hii Konrad Adenauer Stiftg (KAS), kama tunavyoambiwa vijana ndio nguvu kazi basi ni imani yangu kwamba mtanufaika na warsha hii nzuri nawaomba sana yale mtakayo jifunza yafanyieni kazi ili kujiletea maendeleo. Kanisa pia linajua hilo hivyo vijana ni nguvu ya kanisa mafunzo mtakayojifunza mkayaweke katika utekelezaji mzuri ili kanisa liwe hai kiroho na kimwili ili likue pande zote mbili kwa maana ya kiuchumi na kiroho kwa maana uchumi wa kanisa unawategemea pia.

Padre Dulle anasema "kama mnavyojua mtazamo wa Kanisa ni tofauti na mitazamo mingine yote mtakayojifunza yawekeni ndani yenu, hizi ndizo tunu za uadilifu wa kanisa ambao unatuongoza ili tuondokane na ubadhirifu, ufisadi na tuwe waaminifu hata tunapokabidhiwa kutekeleza majukumu fulani tuongozwe na roho ya Injili.  Kwa maneno machache hayo napenda niwakaribishe sana mahali hapa muwe tayari kujifunza na mtakayojifunza myatekeleze ili muwe chumvi kwa wale ambao hawajafika ili kile mtakachojifunza kiwafae na wengine pia. Karibuni sana Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Baada ya kusema hayo aliendelea na utambulisho kama ifuatavyo: Upande wa Serikali alitegemewa Mh. Jokate Mwegelo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe lakini kwa bahati mbaya sana amepata udhuru. Kutoka TEC tunaye Mhashamu Askofu Augustino Shao, Cssp.,  kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Tunaye Bw. Daniel El-Noshokaty, mwakilishi mkaazi kutoka Konrad Adenauer-Stiftung ambao ni wafadhili wetu amefuatana na watendaji kazi wengine."

Kutoka ofisi ya Vijana Taifa tunaye Pd. Adolf Bernard Minga, Mkurugenzi wa Vijana Taifa. Pia tunaye Bw. Erick Mwelulila Mkurugenzi wa Fedha na Utawala pamoja naye wapo watendaji wengine wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Tunaye mwezeshaji Bw. Ponsian Ntui kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino-SAUT. Pd. Daniel Dulle alimkaribisha Bw. Daniel El-Noshokaty kutoa neno lake kwa vijana. Alianza kwa kuwashukuru vijana wote waliofika na kusema KAS ilifika Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1964 kwa mwaliko wa Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kujiletea maendeo. KAS inaamini kwamba maendeleo ni maendeleo ya watu na ndicho tunafanya hapa Tanzania “development is the development of people” alisisitiza kwamba, Tanzania inahitaji uchumi mpya maana kila siku kila mtu anahitaji maendeleo nchini kote “Social Market Economy “why is important? ambao ni uchumi muhimu lakini haimanishi kwamba tunawalazimisha kufuata mfumo huo sisi tunawaelimisha ili nyinyi wenyewe mchague”, Alikazia zaidi.

Katika msemo wa maendeleo ni maendeleo ya watu, tunajifunza mifumo miwili (ubepari na ujamaa) na kufanya mfumo mmoja ili kila mmoja aweze kufaidika na matunda ya nchi yake. Hatupo hapa kuwalazimisha kufuata huo mfumo tupo kuwaelimisha, kwa hiyo msikilize na muelewe ili mchague njia nzuri/ mfumo mzuri kwa Tanzania.  Nawaomba wote mliofika tuungane na wakufunzi wetu kutoka SAUT, tumefanya hivyo ili iwe rahisi kuelewana kwa vile wote ni kutoka taasisi moja.  Kwa hiyo nawasihi muwe tayari kusikiliza na kujifunza mfumo unaotoka katika hiyo mifumo miwili, mfumo huo ulianzia Ujerumani.  Alimalizia kwa kumkabidhi Askofu kitabu cha “muhtasari wa mfumo wa uchumi wa soko jamii kwa Tanzania” lakini pia washiriki wote waligawiwa kitabu hicho. Mtoa Mada ambaye ni Mkufunzi kutoka SAUT Bw. Ponsian Ntui alianza kwa kutaja mada ya warsha kuwa ni “Uchumi jamii na wa soko wa kuwajengea vijana uwezo”, kwa maslahi ya taifa na mtu mmoja mmoja na kwa utangulizi alizitaja sehemu zitakazojadiliwa katika mada hii: Nia ya warsha ni kumjengea kijana uwezo ili ashiriki ujenzi wa nchi na uchumi wake binafsi.

Lakini pia ni kuwahamasisha vijana kushiriki katika kazi za uchumi kwa kuifahamu mifumo mbali mbali ya kiuchumi duniani kwa kuzingatia uchumi unaojari utu, mazingira na wenye uendelevu ndani yake. Alitoa mfano kwamba, ukishiriki uchumi bila kujali mazingira na utu utaharibu lasilimali zote kana kwamba unakufa kesho, tukumbuke ni sisi tunaopaswa kuandaa mazingira mazuri ya vizazi vijavyo. Tutajifunza pia uhusiano uliopo kati ya ujasiria mali na uchumi jamii wa soko. Umuhimu wa TEHAMA kama fursa ya ajira iwapo vijana wataichukua kama fursa na kipimo cha ukomavu na mkumbuke kuwa teknolojia hii usipoingalia vizuri ni janga kwenu na kwa taifa zima. Ni lazima kujua kuwa vitu unavyofanya kwenye mitandao havifutiki, wewe utaondoka lakini vyenyewe vitabaki watakuja kuviona wajukuu wako. Tuone umuhimu wa mfumo imara kwenye nchi yetu.  Nchi isipokuwa na mfumo mzuri wa uchumi unaoeleweka inakosa mwelekeo, mfumo unatafsiri marafiki wanchi, mitaala ya elimu na afya na hivi vyote haviwezi kusimama imara bila mfumo. Kama vijana nawaomba muondoke na uelewa huo.

UFUNGUZI: Warsha ilifunguliwa asubuhi na Askofu Agustino Shao wa Jimbo Katoliki la Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Fedha na Mipango kutoka TEC. Alianza kusema, kwa mara ya kwanza alipohudhuria hii warsha alitamani sana Kitabu hicho kiwekwe vyuo vikuu vyote kama moja ya vitabu muhimu vya kujifunzia. Kama somo kutoka Kitabu cha kwanza cha Wafalme 3:8-15 na sisi kama Solomon tuombe hekima ya Mungu. Tujue hekima inatusaidia nini? Kila mmoja ana chembe ya hekina maana tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.  Ila ile ya ziada tunaipata vyuoni, kwa kusoma vitu mbali mbali na kuhudhuria warsha kama hizi, kukutana na watu tofauti  wa mila na tamaduni tofauti kama tulivyofanya leo. Tunapoongelea uchumi shirikishi ni kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu.  Aliwashauri vijana kujiwezesha wenyewe maana ukijiwezesha utalipa kodi, ni wewe na vipaji vyako na kusema kijana utambue msemo huu “wewe upo kwa sababu mimi nipo na mimi nipo kwa sababu wewe upo“ kijana usijidharau wewe ni mmoja na ni tofauti na mwingine hata uwe dhaifu kiasi gani bado una mchango katika kumkamilisha mwingine.

Tuachane na ile dhana ya elimu ya mwafrika ambayo inalenga utajiri wa haraka haraka unaolenga mhusika na familia yake tu. Aliwasisitiza vijana kuwa waadilifu, wabunifu na kutunza utambulisho wao “ fanyeni vitu vya ubunifu ili muwape ajira wengine” vijana kuweni wakarimu, waaminifu wenye upendo wa kweli bila kutegemea chochote na bila masharti “add value to your value” Kumbukeni huwezi kuwa tajiri peke yako ukizungukwa na maskini wengi, huo siyo uchumi shirikishi. Ulizaliwa tupu na utaondoka tupu lakini mazuri unayoyafanya yatakumbukwa daima na siyo mali utakazoziacha. Alimaliza kwa kusema “Mungu ndiye anayetenda yote, tafuteni kwanza kuwahudumia watu na mengine Mungu atawapatia”.

MADA YA KWANZA: Mwezeshaji alianza kwa kuhitaja misingi ya chumi imara kwa familia ambazo zinaundwa na upendo, furaha, uvumilivu, amani na utu wema.  Nchi imara watu wake wana furaha, upendo, uvumilivu, amani na utu wema na haya yote ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa maana hiyo familia au nchi ikifuata misingi hii itakuwa imara. Tukianza na historia kidogo, tunaona uchumi wa soko ulikuwepo tangu mwanzoi wakati wa azimio la Arusha pole pole ulibadilika kadri ya viongozi wanaokuwa madarakani na sasa dira ya Taifa la Tanzania ni viwanda, uchumi wa kati na wenye nguvu.  Kwa nini sasa tunataka mfumo mzuri zaidi, kabla ya uchumi nchi iliongozwa na mfumo wa Magharibi na Mashariki mfumo wa kibepari na unyonyaji ambao uliwaacha wazawa katika umaskini mkubwa.

Mwaka 1967 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere aliona anahitaji mfumo tofauti yaani wa Ujamaa na Kujitegemea (Socialism) mfumo huu ulipelekea kutaifisha mali binafsi.  Hata hivyo Serikali ilikuwa na uwezo wa kutoa ajira, viwanda vilianzishwa kwa wingi na mashirika ya umma.  Lakini mfumo ulishindwa kuleta maendeleo yaliyokusudiwa ndipo Rais Ali Hassan Mwinyi alikuja na uchumi huru “ruksa” hata hivyo ni katika kipindi hiki uchumi ulianza kupata shida na fikra za ujamaa zilipotea, serikali ikashindwa kuendesha mashirika yake, watu pia wakashindwa kushiriki kikamilifu kwenye uchumi.  Baadae kwenye utawala wa Rais Benjamin William Mkapa akaendelea na uchumi wa masoko huru, uchumi ambao uliimarisha ushindani na kuamsha ushiriki wa wananchi.  Tukumbuke ubinafsishaji haukuwa tatizo ila tatizo lilikuwa usimamizi wa mali ya umma. Ubinafsi na uchoyo ukajitokeza. Tunashuhudia sasa kwenye utawala wa Rais John Pombe Magufuli, sekta binafsi ina nguvu na serikali inaweza kukusanya kodi kwa wingi, ingawaje bado haitoshi. 

Na sasa tunatekeleza dira ya taifa ya uchumi wa kati, vijana tushiriki kwenye uzalishaji ili tuweze kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi. Pamoja na jitihada hizo nchi kama nchi bado inashindwa kufika mahali pazuri zaidi kwa sababu mipango ni mingi lakini hakuna mwongozo, hatuna mfumo unaotuongoza na ndio maana kila Rais akiingia madarakani anakuja na dira yake, bado kama nchi hatujafaulu kuweka mfumo endelevu utakao mfanya Rais ajaye madarakani aendeleze aliyoanzisha mtangulizi wake. Mfumo wa Ubepari ni mfumo wa unyonyaji usiojali watu, faida ndio kitu cha msingi na soko ndio hupanga bei, ni mfumo ambao hauangalii utu na uendelevu wa jamii mfumo huo unatazama faida tu. Ni wakati sasa wa kuangalia mifumo yote miwili wa ujamaa na ubepari ii tuone tuchukue mazuri yapi kutoka kila mfumo na tutengeneze mfumo mzuri ambao utahakikisha kila mtu anashiriki kwenye “uchumi fungamani” au uchumi jumuishi,  na kuhakikisha haumwachi mtu. Na nipende kuwahakikishia vijana nchi zilizotumia mfumo huu ndio nchi imara kiuchumi duniani  mfano ni: Ujerumani, Scandinavia, Norway, Dernmark, Sweden na Ireland. Alisisitiza kuwa nchi ikiwa na mfumo mzuri inakuwa pia na mfumo mzuri wa maamuzi.

Ili maendeleo yawe na maana sana lazima yawe na mahusiano na watu, yamguse mtu mmoja mmoja na kumweka huru. Alitoa ushauri kwa vijana kujipanga ili kuweza kuyamudu maisha yao na bila kumwacha mtu awaye nyuma; waanze leo kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na huduma za kijamii Majadiliano/Ushauri/mapendekezo kutoka kwa vijana: Nchi iweke sera zinazotabirika ili kijana awekeze na kufanya biashara. Ushindani huu unaleta ubora na fikra mpya kwa mfanyabiashara. Ukipoteza unawajibika-kijana anza wewe usiseme sina mtaji, mtaji msingi ni mawazo yako, ukishindwa utashikwa mkono anza na kidogo ulicho nacho leo. Serikali itoea huduma muhimu kwa wote mfano BIMA za afya na elimu. Serikali iwape motisha vijana kwa kuwatoza kodi kidogo vijana wanaoanzisha biashara ili vijana waweze kushiriki kwenye uchumi wa nchi na sio kuwaachia wageni peke yao. Vijana sisi wenyewe tuwe waajiri tusisubiri ajira maana tukiweza kujiajiri hata nchi ikipata shida basi uchumi uendelee. Kanisa litengeneze miradi ya kuwapa vijana fursa ya kujitegemea kiuchumi. Vijana wamependekeza kwamba, watunga sera wa nchi waone na kupanga namna ya kufanya ili vijana waondokane na mawazo ya ajira baada ya kuhitimu vyuo vikuu kwa kuwaandalia mfumo wa ajira binafsi tangu huko mashuleni. Vijana tuanze na talanta tulizopewa na Mungu na hizo hizo ndizo viwanda vyetu. Vijana tuwe “Leader marker” yaani vitalu vya kuunda viongozi, anza na kidogo ulichonacho usisubiri kikubwa. Tujiandae wakati ufahao na wakati usiofaa.

Changamoto katika maisha ya ujana, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa uchumi fungamani: Katika mfumo huu wa uchumi tunaona watu wenye BIMA ya afya ni wachache sana kwa sababu ya umaskini mkubwa. Ni mwaka wa nne sasa Serikali haiajiri. Makusanyo ya kodi hayatoshi. Kilimo bado hakijachangia sana katika Pato Ghafi la Nchi. Tumeharibu mazingira hasa kwenye migodi mfanpo ni Geita na Mara. Elimu kuhusu mfumo wa uchumi haijaenea sana. Serikali inabadilisha sana mifumo, kila Rais anaingia na mfumo wake hakuna anayeingia akaendeleza mfumo ulioachwa na mwenzake, tunahitaji mabadiliko ya kiutawala na kiungozi, ili kusimamia sera, mikakati na na utekelezaji wake. Vijana tumechoka, tunahitaji fursa mf. Mikopo, tumehudhuria semina na mafunzo mengi lakini bado hatujajikomboa. Tunataka semina zinazokuja na majibu yote. Kutokuwepo kwa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi ya kuuza mazao kunawakatisha tamaa vijana. Mifumo ya elimu ya taifa bado ipo kwenye kuajiri na siyo kumuandaa muhitimu kujiajiri. Tunaomba ibadilike. Vijana wakati mwingine wapo tayari kuanzisha ajira zao ndogo ndogo lakini mfumo wa Serikali wa kupata vibari na leseni ni sumbufu sana mf. Unaweza kulipia frame lakini mpaka upate vibari tayari kodi yako inakaribia kuisha.

Fursa mbali mbali zilizopo miongoni mwa vijana: Uhusiano na mataifa mbalimbali. Mfumo wa sasa ni mzuri kibiashara. Vijana watumie mfumo wa kimtandao  “networking” kama fursa, achaneni na mawasiliano yasiyo na tija kwenu na kwa taifa, kila leo jifunze kupata mawazo mapya kwa njia ya kujisomea vitabu, majadilida na kuhudhuria semina na warsha kama hizi. Vijana tusiogope kushiriki katika nafasi mbali mbali za uongozi. Majadiliano/maswali: Nini kifanyike kama nchi ili kufikia uchumi wa kati? Ni namna gani fundi ujenzi,ushonaji au muuza maandazi anaweza kuchangia uchumi wa taifa? Uchumi wa soko jamii unawezaje kutufaidisha wote kwa pamoja? Kila Rais akiingia madarakani na mfumo wake ni vipi tunaweza kutumia mfumo shirikishi? Tunaambiwa taifa linaendelea kiuchumi lakini mbona wachache wanalipa kodi, nini shida ni elimu au uzembe? Je, mitandao ya utandawazi “Globalization” inasaidia au kutokomeza uchumi? Serikali inajaribu kuwainua vijana kwa asilimia 4 na je taasisi binafsi zinasaidiaje? Kanisa limejipanga vipi kuishauri serikali kutumia huu mfumo mpya? Mkufunzi umetwambia tuanze biashara tukianguka tutashikwa mkono, naomba kumjua hasa ni nani atanishika mkono maana hata mimi nimeanguka. Ni mipango ipi tutumie kama vijana ili kutekeleza uchumi shirikishi? Kanisa, Je? Lina mkakati gani wa kukusanya mawazo ya vijana? Vijana tusikate tama kujaribu fursa mbali mbali maana mafanikio ni jaribio la kushindwa mara nyingi.

Ufafanuzi wa mkufunzi: Ukiwa na wazo lako zuri tengeneza hoja, shawishi wakubwa, onesha tofauti, fanya hivyo hata parokiani kwako na pia tumia majukwaa yenu mfano Easter Conference, Mikutano ya kitaifa ya TYCS, TMCS na VIWAWA. Nawashauri vijana kutosubiri kufanya kazi kwa kile ulichosomea siku hizi hilo hakuna panga tofauti na fanya tofauti mfano Kilimo kinaondoa umaskini katika muda mfupi sana. Wewe mwenyewe anza kubadilika na uwe balozi kwa wengine. Elimu yako ikufanye uishi popote na kufanya kazi yoyote na ujue elimu yako haipitiwi na muda inabaki pale pale. Serikali ina fursa nyingi tengenezeni vikundi nendeni kwenye halmashauri zenu mkiwa mmejipanga, mnataka nini na mtakelezaje hicho mlichopanga, msiogope, jaribu leo.

MADA YA PILI- Pd. Adolf Minga, Mratibu wa Vijana-TEC: Vijana, imani na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya kiuchumi. Duniani kote vijana ndio nguzo kuu ya maendeleo.  Vijana mna uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika utendaji na hivyo kuwa kichocheo kikubwa katika maendeleo ya nchi.  Lakini pamoja na uwezo huo mkubwa bado mnakabiliwa na matatizo mengi katika jamii ya Tanzania na ulimwenguni kote hapa nitagusia moja la ukosefu wa ajira. Ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo ambalo linajumuisha ama linatokana na sababu nyingi. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na vijana kukosa elimu na ujuzi hitaji.   Mbaya zaidi waajiri wengi wanatangaza nafasi za ajira huku wanataka sifa ya uzoefu kazini kama hitaji la muhimu.   Mimi najiuliza huo uzoefu kijana aliyemaliza shule ataupata wapi?  Ukubwa wa tatizo la ukosefu wa ajira Tanzania unaonekana wazi kwa kuangalia takwimu tulizo nazo, ambazo zinaonyesha kuwa, kila mwaka takribani vijana kati ya 600,000 na 800000 huingia kwenye soko la ajira kutafuta kazi,  wakati sekta rasmi huzalisha nafasi za ajira 40,000 tu.  Hali hii huacha wengi bila ajira kwenye sekta rasmi. 

Aidha, sasa hivi ajira zote za serikali na mashirika yake hazizidi asilimia tatu.  Kwa hiyo vijana msitegemee kupata ajira serikalini, huko nafasi ni chache sana.  Sehemu ya kukimbilia ni kwenye sekta binafsi na hasa ile isiyo rasmi, ikiwa na pamoja na biashara na kilimo.   Kinachotakiwa ni kuongeza tija kwenye uzalishaji ili ajira hizo ziwe na manufaa na kuvutia wengi. Tujuavyo Vijana wakitumika vizuri na wakiamua kufanya kazi kwa bidii, akili, juhudi na maarifa wataleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini Tanzania. Ninyi ni Jeshi kubwa sana kwa maendeleo kiuchumi na ya kidini na hata ya nchi kwa ujumla.  Vijana mnaweza kufanikisha jambo lolote mkitaka.  Tumieni ujana wenu vizuri mkiwa bado na nguvu maana nguvu ndio mtaji. Ninawahasa vijana msipotumia vizuri ujana wenu mnaweza kuwa Jeshi la yule mwovu shetani na mkafanya mambo mengi ya uovu, kama ujambazi, wizi, kampeni ya kupinga mambo mema ikiwa ni pamoja na ya kidini.  

Leo hii tunapozungumzia vijana, wengi wamejitumbukiza katika lindi la uvivu, ukosefu wa nidhamu na hata ufanyaji wa biashara haramu kama vile uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, utumwa mamboleo; mambo ambayo wote tunafahamu wazi kuwa ni kinyume na maadili na utu wema. Kuporomoka kwa maadili ya kijadi na pia ya kiimani yanapelekea vijana kukosa adabu na nidhamu. Popote pale kijana yeyote anayekosa nidhamu, adabu na heshima kwa wakubwa wake hukosa pia hofu kwa Mungu. Na kijana anapokosa hofu kwa Mungu anapungukiwa kwa namna fulani hali yake sahihi ya ubinadamu. Tabia mbaya kama hizo hufanya kijana kushindwa kuwa kiongozi bora kwa kujawa ubinafsi, kukosa amani, kushindwa kutenda haki na hivyo kupelekea ukosefu wa amani katika jamii yetu. Ili kukwepa hayo yote imani inajengwa na mambo mengi baadhi ya hayo ni : Kijana na makusudi ya Mungu. Kila kijana ameletwa duniani kwa makusudi maalum, na makusudi hayo kuyajua mapema na kuanza kuenenda sawasawa na mapenzi ya Mungu. Hauko humu duniani kwa bahati mbaya hivyo jitahidi sana kutafuta fursa za kujikwamua.

Kijana na Uongozi wa Roho Mtakatifu: Wote wanaongozwa na Roho wa Mungu hao ndio wana wa Mungu. Tunaishi katika Dunia inayochanganyikiwa, imejaa mitazamo ya kila aina na mingi inavunja watu moyo wasimkilize na kuongozwa na Mungu. Hili hata makanisani limeanza kuwa la kawaida. Lakini ukiwa kijana uliyeitwa kwa makusudi maalum na Mungu katika mipangilio yako jitahidi kuongozwa na Roho wa Mungu katika maisha yako yote. Kijana na Kazi/Biashara: Vijana mna nguvu na fahari ya Vijana ni nguvu zao lakini kwa Vijana wengi nguvu hizi hazitumiwi ipasavyo kuboresha maisha yao. Vijana wengi wanakaa tu bila kufanya kazi au biashara zitakazowaletea maendeleo katika maisha yao huku wakitoa sababu nyingi kwanini hawafanyi chochote cha maana.  Utasikia “mimi sijasoma, mimi sina mtaji, mimi sina wazazi, mimi nilikataliwa, mimi sina hiki la kile”. Badala ya kutoa sababu kwa nini hafanyi yakupasanyo, hebu tafuta ni namna gani unaweza kufanya yakupasayo.  Uwezo mnao, nguvu mnazo, msaada wa Mungu upo, mnaweza yote kupitia nguvu akutiayo Kristo. Yusufu hakuwa na chochote lakini alifanikiwa, Daniel, Shadrack, Meshack na Abedgego walikuwa utumwani lakini walifanikiwa. Unaweza kufanikiwa bila kujari hali yako na ya ukoo wako ikoje, cha kujua ni ujue ufanye nini.

Kijana na Kazi ya Mungu: Wote wafanyao kazi ya Mungu kwa uaminifu huheshimiwa na Mungu na kufanikiwa. Imani yangu wengi kwa kufanya kazi ya Mungu mmepewa majina mbalimbali mpaka labda mkaitwa walokole. Vijana jitahidini kufanya kazi ya Mungu ili kuweza kufanikiwa kwa asilimia zote. Kijana na usafi wa mwili, nafsi na roho: Hakuna jambo la msingi kwa kijana kama kuwa safi mwili, nafsi na roho. Usafi wa kiroho na nafsi utakupa kibali kwa Mungu.  Usafi wa mwili utakupa kibali kwa watu na kwa Mungu pia.  Yusufu wakati anapelekwa kwa Farao ilibidi anyoe ndevu ili aonekane safi kwa sababu wanadamu huangalia nje na kwao si dhambi kufanya hivyo ila Mungu huangalia ndani. Utakatifu ndio msingi wa kutembea na Nguvu za Mungu, shetani anatafuta kwa bidii kuchafua vijana kwa dhambi kama tamaa za macho na mwili na matendo yanayoambatana nazo na kutuletea hatia na mashaka ili tukose ujasiri wa kumtumikia Mungu.

Kijana na Urafiki: Kuwa na rafiki ni jambo la kibiblia kabisa na kuna faida nyingi za kuwa na marafiki wazuri lakini pia kuna hasara nyingi kuwa na marafiki wabaya (Mithali 13:20). Rafiki wa kweli ni yule anayemtii Mungu, anayekutia moyo kwenye maono uliyo nayo, aliye tayari kukuonya na kukukosoa unapokosea, anakuombea, ni mwaminifu kwako, hana wivu na mafanikio yako, anakuheshimu na kukuthamini. Urafiki wa jinsia moja hauna majaribu sana kama urafiki kati ya watu wenye jinsia mbili tofauti.  Vijana kuweni na misimamo na mipaka. Ni muhimu na nashauri ni vizuri kumwomba Mungu sana wakati wa kuchagua marafiki au watu wa kushirikiana nao katika jambo lolote. Yesu alimwomba Mungu Usiku kucha kabla hajachagua wanafunzi wake 12 ( Lk.6:12-13). Kijana na Maamuzi yake: Maamuzi huamua ubora wa maisha na hatima ya Mtu. Maamuzi mabaya huzaa maisha mabaya na maamuzi mazuri huzaa maisha mazuri.  Vijana wengi hufanya maamuzi kwa haraka, kwa hasira, kwa msisimko, kwa kushawishiwa na marafiki au watu wengine kuona wanafanya naye anafanya, bila kuangalia athari zake na kufikiria kwa undani na umakini mkubwa tena katika hali ya maombi.  Ubora wa Maamuzi yako kuhusu maisha yako, elimu yako, wazazi wako, kazi yako, biashara zako, Kijana yeyote makini lazima kujifunza stadi za kufanya maamuzi bora mapema katika maisha yako.

Kijana na Muda: Kama vijana mnatakiwa muwe mstari wa mbele katika kuukomboa wakati (Waefeso 5:15-17), siku zetu za kuishi hapa duniani zimehesabiwa (zaburi 90:12)  na tunatakiwa kufanya mambo ambayo Mungu ameyakusudia katika kila hatua ya makuzi kwa kutumia muda ambao Mungu ametupa.  Kuna mambo ambayo lazime tuyafanye kwa ajili ya Mungu na maisha yetu tukiwa kama vijana na tukiwa kama watu wazima hali kadhalika. Hatupaswi kupoteza muda kwa ajili ya mambo yasiyo na manufaa kwenye maisha yetu ya ufalme wa Mungu. Mungu ametupa rasilimali muda ni lazima tuwe mawakili waaminifu. Mungu anajali sana muda, aliwaambia wana wa Israel katika kitabu cha kutoka 21:18-19. Kijana na Malengo: Kwa bahati mbaya vijana wengi wanaishi bila malengo katika maisha yao kwa sababu ya kukosa maono au mwelekeo wa maisha, hawajui umuhimu wa kuwa na malengo na hivyo hawajui jinsi ya kuweka malengo, wana mtazamo potofu kwamba kuwa na malengo ni kujitumaini nafsi zao na kutomwamini Mungu aliyekuumba, wengine wanakaa na watu au marafiki wasio na tabia ya kuweka malengo katika maisha yao na hivyo kukosa changamoto ya kujifunza.  Usipojiwekea malengo katika maisha yako wewe mwenyewe, matukio, hali na watu wanaokuzunguka vitaamua mwelekeo wa maisha yako. Usipojua uendako waweza kufuata barabara yoyote na kuishi kokote kusikofaa.

Kijana na Vipaumbele katika Maisha: Katika maisha kuna mambo mengi sana yanayotukabili kama vijana, kuna masomo, kuna marafiki, kuna wazazi, kuna kanisa, kuna kazi ya Mungu, kuna biashara, kuna ndugu na watu wengi wanatuwekea matarajio tofauti tofauti.  Na changamoto tuliyo nayo ni kwamba, hatuwezi kufanya yote kwa wakati mmoja au ndani ya muda mfupi.  Kama vijana kuna umuhimu mkubwa kujua yapi ni ya msingi ili kuyapa kipaumbele. Kijana na Uongozi: Vijana ndio viongozi katika sekta mbalimbali, ndio maana popote ulipo ni vizuri kutafuta kushika walau wadhifa fulani ili kupata uzoefu maana hatuibuki tu na kuwa viongozi. Vijana wengi niwajuao wamejaa aibu na kutojiamini, hawajengi uwezo wao wa kuzungumza lugha zinazotakiwa katika mawasiliano na hawana moyo wa kujituma wanasubiri kutumwa.  Japokuwa si wote tutakuwa na nyadhifa za uongozi lakini naamini wote tunahitaji maarifa na stadi za uongozi ili tuweze kufanikiwa katika Nyanja mbalimbaliza maisha yetu. Ndoa au familia inahitaji ujuzi wa uongozi, biashara zetu na kazi zetu zinahitaji uongozi, huduma makanisani zinahitaji watu wanaofahamu vizuri uongozi.  Vijana mnatakiwa kuwa na moyo wa kujituma zaidi kwenye vikundi vya kikristo mashuleni na vyuoni, makanisani, kazini, kwenye biashara n.k.

Kijana na Maisha yaliyopita: Huwezi kuwa na maisha mazuri kesho kama wakati wote unafikiri yale yaliyopita jana. Kuna watu katika maisha haya hawasongi mbele, hawaendelei wako pale pale kwa sababu wameruhusu maisha yaliyopita kuwashikilia kiasi cha kuamua kubaki pale walipo na kuwalaumu watu wengine. Jifunze kwa yaliyopita lakini usiyaruhusu yakuvunje moyo. Ni vizuri kuchuchumia yaliyo mbele. Kuchuchumilia ni neno linalodokeza umuhimu wa kutumia nguvu fulani kuhakikisha kwamba unasonga mbele bila kujali nini kinatokea, nini kinakupinga na kinakuzuia, unajikwamua kutoka kwenye vile vinavyokushikiria. Ni uamuzi unaotoka ndani ya moyo wa mtu kwamba nitafanya kile kinachotakiwa kufanyakwa wakati ninaotakiwa kufanya bila kujali ninajisikia kufanya au la kwani hii ndiyo nidhamu pekee inayotakiwa ili niweze kutoka pale nilipo na kwenda ambapo Mungu amekusudia niwe.

Kijana na Tofauti: Vijana wengi wamejaa kuigana na kufanya mambo ambayo kila mtu anafanya. Lakini wakati umewaadia vijana amkeni na muwe tayari kufanya mambo tofauti na wengine. Wakati wengi hawawezi kuamka mapema kufanya maombi na kusoma neno la Mungu, wewe unaweza ukiamua, wakati wengi hawawezi kusaidia rafiki zao kubadilika, wewe unaweza ukiamua, Wengi wetu hatuwezi kusaidia yatima na wahitaji tukiamua tunaweza. Vijana mkiamua mnaweza kufanya mambo ya tofauti yatakayowafanya muwe vijana wa tofauti.  Kwa sasa njia pekee ya kujipatia maendeleo ni kuwa na ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi. Mwito wangu kwenu vijana, tumieni muda mwingi kufuatilia mafunzo popote yalipo ili kupata mwanga mpya wa soko la ajira. Ulimwengu mzima unakuhitaji wewe ni vizuri kuitangaza, kuifahamu na kuiishi imani yako.

Maswali/maoni/ushauri: Vijana tunaamini Kanisa linayo nafasi kubwa ya kuwasaidia vijana hasa kuwapa elimu na pia linazo fursa nyingi, swali langu je kanisa linafanya nini kuwasaidia vijana? Tunaomba semina kama hizi zinazokutanisha vijana wa lika na taaluma mbali mbali ziwepo mara kwa mara na ikiwezekana zishuke hadi ngazi ya jimbo. Nalipongeza Kanisa maana linaweza kueleza ukweli hata serikali ikipata kigugumizi. Vijana tusikurupuke tuingie ndani kutafuta fursa.  Kijana muda wako mzuri wa kutafuta mafanikio ni leo usingoje wakati mwingine haupo anza leo Maisha yanaanza katika umri wa miaka 40, ulitumiaje ujana? Tutumie maarifa katika kutafuta fursa, tuwe na vipaumbele.  Tumtangulize Mungu, tuangalie mfano wa Mama Bikira Maria hata katika chagamoto zote hakukata tamaa.

Vijana wa leo hatuna “focus”, hatujiulizi tunagusa gusa vitu hatuna uzoefu, tunapokea kila kitu kilivyo bila kuchambua, fanya jambo ili upate matokeo siyo lipite. Vijana tuache kulalamika kama wengine hawataki simama mwenyewe ukabili changamoto ili usonge mbele “zifanye changamoto zako ziwe fursa”.  Kijana fanya unachofanya katika kweli na uwazi na si kwa ndoto. Ombi kwa Mkurugenzi wa Vijana, tukalishe vijana kwa ajili ya kujadili mustakabali wa Kanisa letu. Vijana tunashindwa kwa sababu ya kutaka mishahara mikubwa kwa muda mfupi na pia kushindwa kujitolea. Majibu/ufafanuzi mtoa mada: Ukitaka kumjua mtu sikiliza asichosema.  Kijana ukitaka kufanikiwa katika maisha fuata maamuzi yako ili usipate shida au ukizipata uweze kuzivumilia, ushauri unatolewa ili ukusaidie kufanya maamuzi. Kanisa linajitahidi kuwapa fursa vijana wake kadri inavyowezekana mfano Kuna baadhi ya majimbo limeanzisha VICOBA. Vijana muwe na mtazamo mpya muoneshe vipaumbele katika maisha ili msaidiwe.Vijana mjijue na kujitambua wenyewe alisema Mwanafalsafa Socrates. Vijana jipangieni  muda wa kujitathmini ili mjue mko wapi.

SIKU YA PILI: Warsha ilianza na “RECAP”: MADA YA TATU: Bw. Richard Jackson Ndila kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Social Market Economy as a gateway to Entrepreneurship” ni nini: Ni hatua katika kuanzisha shughuhuli au biashara za uzalishaji mali.Kuwa na soko peke yake hatoshi tuwe na ziada? tuone nafasi ya ujasiria mali ukiunganisha na soko jumuishi. Hakuna aliyewahi kushindwa ujasiria mali kama ukiweza kutumia fursa kwa kuyaishi mazingira yanayokuzunguka “Vijana mjue humu duniani tunavyoishi hakuna aliye tofauti na mwingine, tofauti yetu ni tabia, tunavyoishi na tunavyotenda” amka sasa na tenda tofauti na mwingine. Changamoto za vijana wa leo: Katika soko la ajira kila siku waajiri wanakuja na matakwa mapya, vijana mjipyaishe katika maisha na vipaumbele. Ajira siku hizi hazipo na zilizopo hazitoshi, mbuni ajira binafsi. Kijana ujitambue na malengo yako na wakati wako, jithamini ili uwe wa thamani.Matarajio ya wazazi yalikuwa makubwa juu yako baada ya kumaliza elimu ya juu. Jipange onesha hayajapotea kwa kutumia vipaji vyako hasa kuwa mbunifu.

Mahusiano-jamii yamebadilika sana, uhusiano umepoteza matumaini ya baadae, tuishi maisha chanya “positive”. Tuwe na mahusiano yanayojenga mtandao wa mafanikio, mtandao ukulipe. Jiulize bando unaloweka kwenye simu yako linafanya kazi gani? Vijana mnapaswa kubadilika, waajiri leo hawajiri degree yako, wanajili kile ulicho nacho, unafanyaje kazi uliyopewa “tupo maskini kwa sababu hatufanyi wala kutenda kwa weledi. Nawashauri sana vijana baada ya warsha hii mbadilike, namna ya kufikiri na kutenda ili mfanye vitu tofauti ili muweze kusimama. Kuweni na mpango na tulieni katika mpango huo, usifanye vitu nusu nusu bila kukamilika.  Changamoto kubwa ya Vijana wa leo ni kwamba, hatuanzi mambo mapema, anza mwenyewe leo watu wataona wakutafute, watapenda kazi zako.  Usifanye vitu kwa msukumo sikiliza sauti ndani yako “passion”. Ukitaka kufanikiwa anza kitu chako mwenyewe na ufikirie utafanya na nani?

Waguse wengine uwe chumvi na mwanga ndani ya jamii na si mzigo kwa jamii. Fanya kazi kwa kuzingatia muda na kwa bidii usingoje miujiza. Mjadala/maoni/maswali: Vijana wengi hawafanikiwa kwa sababu hawana nia ya ndani, ubunifu na kujituma. Je? biashara inaweza kuanza na pesa za mkopo? Kwanini vijana wengi wanahudhuria semina nyingi lakini bado hawafanikiwi?Ufafanuzi mkufunzi: Ulimwengu mamboleo ni wa ushindani kila mtu ana haraka anatumia kila mbinu avuke vikwazo, sasa usipoanza leo utakufa na ndoto zako. Unavyoamini ndivyo inavyokuwa, ukitaka kufanikiwa bila tathimini hufiki mbali.

MADA YA NNE- Dr. Camillus Kassala, Kutoka Idara ya Haki, Amani na Uumbaji- Baraza la Maaskofu TEC: Nawashauri vijana kukumbuka kuwa katika mfumo wa soko huria kila kitu ni bidhaa ili mradi kinauzika, kuweni makini msiyumbishwe na nguvu ya soko alitoa mfano kuwa dunia ya leo hata binadamu amekuwa bidhaa. Kijana jiulize wewe na vipaji/ujuzi wako unaweza kuanzisha shughuli gani za uchumi? Na Je, vitu gani vinakukwamisha? Basi ukipata majibu hayo biashara hizo zitakuwa na manufa kwa jamii. Uongozi wa uchumi- shughuli zote za uchumi haziwezi kuongozwa kisiasa au kitaasisi tu bali kwa njia ya amani, kusimamia na kuongoza utekelezaji wa haki za binadamu. Kila mtu atumie talanta zake kuchangia kukuza uchumi kwa manufaa ya wote. Kama tunaambiwa uchumi wa Tanzania unakua lakini bado maisha ya watu wake yapo pale pale ni wazi haushirikishi na pia unachangiwa na mgawanyo usio wa haki. Vijana ni wakati sasa wa kufikiri kwa vigezo, viwango na mantiki la sivyo itakuwa vigumu kufikia uchumi wa soko, mkumbuke kuwa mitara yote ya elimu haifundishi namna ya kufikiri.

MADA YA TANO-Bw. Paschal Mwanache, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Nini Mchango wa “Social Media” yaani “mitandao ya kijamii” katika maendeleo ya uchumi na namna vijana wanavyo shiriki. Tangu mwanzo, Kanisa linathamini matumizi sahihi ya vyombo vya habari kama njia rahisi ya kuwafikia watu katika uinjilishaji mfano Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alisema “kama tunataka kuinjilisha hatuwezi kukwepa matumizi ya vyombo vya mawasiliano” Kanisa linaviona vyombo vya mawasiliano kama zawadi ya Mungu vikiunganisha watu kama kaka na dada.Vyombo vya habari na maendeleo: Maendeleo ni suala shirikishi na vyombo vya mawasiliano ndio kazi yake. Dunia ya leo tunashirikishana kila kitu mfano elimu. Tumieni vyombo vya habari kujikwamua kiuchumi. “Social Media Economy” ina faida zake nyingi mfano kutengeneza kazi na kuziuza “Job creation”, Marketing/business collaboration, Skills Acquisition (unaweza kupata ajira kupitia network na small capital, social media yenyewe ni mtaji. 

Kijana ujuzi ulio nao ni ajira weka bidhaa zako mtandaoni zionekane, uuze upate pesa. Shida kubwa tuliyo nayo vijana ni matumizi yasiyo sahihi ya vyombo vya mawasiliano, ukimuuliza kijana bando aliloweka leo amewasiliana na fursa ngapi za masoko au ajira ni hakuna. Zipo pia changamoto nyingi za mitando iwapo kijana hukuwa makini mfano, matumizi ya picha chafu, utekaji, mafunzo ya kigaidi na mengine mengi. Tufanye nini”: Tumieni ile karama uliyopewa na Mungu ya kukutofautisha na viumbe wengine. Jiepushe na kuangalia vitu vibaya na “posts” mbaya kumbukeni maneno yanaua na uzingatie usipotumia mitandao vizuri utaishia kubaya. Tumieni pia “channel” za Kanisa mfano TEC kila siku tunaweka tafakari ya masomo kwenye mtandao, sikilizeni Radio na TV mbali za kanisa na kusoma mafundisho yanayolenga kukuza imani yako na ustawi wa utu wako. Maswali/mchango: Waendeshaji wa mitandao ya Kanisa wapo nyuma sana si wabunifu mfano wanachelewa sana kuboresha taarifa zao. Vijana wameshauriwa kujifunza matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii: Majibu toka kwa mtoa mada. Mapendekezo yenu tumeyapokea tutajitahidi kuyafanyia kazi. Lakini na ninyi vijana badilikeni tafuteni fursa na kuzitumia.

KUFUNGA; Askofu Mkuu Renatus Nkwande, wa Jimbo kuu la Mwanza alifunga warsha hiyo kwa kusema “nawashukuru vijana mlioweza kuketi hapa kwa siku mbili na kuwa tayari kujifunza”. Akionesha masikitiko yake kwa mahangaiko waliyonayo vijana alisema, ‘mimi daima nashangaa kusikia wanaowaambia mjiajiri wao wameajiriwa” lakini msisahau kuwa yanayotokea leo hapa yanatokea hata Ulaya. Lakini nataka niwatie moyo kuwa, changamoto za leo zitajibiwa na nyie vijana kwa kujishughulisha, mkumbuke pia kuwa Kanisa halijawaacha linawasaidia lakini haliwezi kutosheleza mahitaji ya vijana wote wa Tanzania. Alisisitizia “Vijana wangu tumieni hekima na busara kushinda vishawishi ambavyo dunia ya leo  ndiyo changamoto kubwa, nawasihi sana mwaminini Mungu na Kristo na toeni ushuhuda wa imani yenu hata katika mahangaiko; teteeni imani yenu msikubali kuharibikiwa. Daima kanisa likiona kitu huweka taadhari na wale wanaokataa maongozi ya Mungu wakitaka uhuru ndio waathirika wakubwa hasa vijana. Niwaombe basi vijana wangu kuweni wasikivu, wanyenyekevu kwa wazazi na walezi wenu msipotumia hekima mtaingia katika magenge ya kiarifu mfano: mauaji, utoaji mimba, ushonga na suala zima la kubadili jinsia.

Alisisitiza kuwa, ili kufanikiwa lazima kuungana, kuacha ubinafsi na kushirikishana kwa kufanya kazi kimtandao yaani kwa lugha ya Kiingereza “networking” ili muweze kuelezana fursa zilipo.  Kijana tulia na sali maana huwezi kufanikiwa ukiwa umechanganyikiwa, acheni kuiga mambo maovu mfano uvutaji bangi na matumizi haramu ya kulevya.  Kijana ujue uliumbwa na Mungu ili uchangie kuleta maendeleo ya ulimwengu, na sasa Je? Umefanya nini mpaka sasa kuchangia maendeleo fungamani nchini Tanzania? Vijana wametoka katika makundi na mikoa ifuatayo: Vijana: Kagera, Morogoro, Songea, Mtwara, Iringa na Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa upande wa Vyuo kikuu ni : TIA, UDSM, Muhimbili, DUCE , IFM, Iringa,  Excellent na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi Wadau wengine ni pamoja na: Radio Maria, Maritain Institute, Fahari Sekondari na Kalamu ndogo. Sarah ambaye alikuwa mwongozaji alianza kwa kuwashukuru TEC na KAS kwa kuandaa hii warsha na kusema “Vijana ni kundi kubwa katika nchi yetu, tuhakikishe tunalipeleka taifa mbele toka tulipo tuujue mfumo wetu wa uchumi ili tufike mahali bora zaidi.  Aliwaomba vijana kuwa makini kusikiliza na kuchangia Neno la Mungu “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.

Warsha ya Vijana Tanzania

 

30 October 2019, 13:28