Tafuta

IMBISA: Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, linasema, chuki dhidi ya wageni Afrika ya Kusini ni vitendo vya kigaidi na kamwe haviwezi kuvumiliwa! IMBISA: Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, linasema, chuki dhidi ya wageni Afrika ya Kusini ni vitendo vya kigaidi na kamwe haviwezi kuvumiliwa! 

Tamko la IMBISA: Xenophobia: Chuki dhidi ya Wageni ni Ugaidi!

Vitendo vya chuki dhidi ya wageni vilivyojitokeza hivi karibuni Afrika ya Kusini na kutikisa hata baadhi ya nchi za Kiafrika ni vitendo vya kigaidi, ambavyo kamwe haviwezi kuvumiliwa na wapenda haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. IMBISA inapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na kutikiswa na vitendo hivi vya kigaidi. XENOPHOBIA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni “akichonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika alisema, chuki dhidi ya wageni Afrika ya Kusini “Xenofobia” ni ugonjwa hatari sana katika maisha mwanadamu na umeenea sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kielelezo cha uchoyo na ubinafsi; kiburi cha baadhi ya watu kujisikia kuwa ni watu wa maana zaidi kuliko wengine na mara nyingi chuki hizi zinachochewa na wanasiasa wanaotaka umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Haya ndiyo yaliyosababishwa na viongozi kama Adolf Hitler. Ukabila, udini na upendeleo ni magonjwa ambayo yamesababisha mauaji ya kimbari huko Rwanda na hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu mauaji haya yalipotokea na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anasema, alipokuwa nchini Kenya aliwataka vijana kuachana na tabia ya kukumbatia ukabila usiokuwa na mashiko. Hizi pia ni chuki za ndani dhidi ya ndugu wamoja. Ukabila katika baadhi ya nchi za Kiafrika anasema Baba Mtakatifu umekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kama ilivyotokea nchini Rwanda!

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kusini mwa Afrika, IMBISA, katika tamko lake kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii linasikitika kusema kwamba, vitendo vya chuki dhidi ya wageni vilivyojitokeza hivi karibuni Afrika ya Kusini na kutikisa hata baadhi ya nchi za Kiafrika ni vitendo vya kigaidi, ambavyo kamwe haviwezi kuvumiliwa na wapenda haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. IMBISA inapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na kutikiswa na vitendo hivi vya kigaidi. Wanawaombea wote faraja kutoka kwa Roho Mtakatifu. IMBISA inazialika nchi za Kiafrika kuwa na utulivu na wala wasitake kulipiza kisasi kwani watawasha moto wa chuki na uhasama, utakaokuwa ni vigumu kuweza kuzimishwa. Changamoto zilizojitokeza iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ili kujenga udugu wa kibinadamu unaozingatia na kuheshimu tofauti msingi kama utajiri na amana ya Bara la Afrika.

Askofu Lucio Muandala, Mwenyekiti wa IMBISA anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunga mkono mapambano dhidi ya wale wote wanaopandikiza “ndago za chuki” dhidi ya wageni nchini Afrika ya Kusini, kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho! IMBISA inayaalika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika kutenga siku maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa chuki dhidi ya wageni. Nabii Yeremia anawakumbusha Waisraeli kutowaonea wageni, yatima wala wa wajane; kamwe wasimwage damu ya watu wasiokuwa na hatia, wala kuifuata miungu mingine, kwani wakitenda yote haya itakuwa ni kwa hasara yao wenyewe. Rej. Yer. 7:6-7. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kusini mwa Afrika, IMBISA kunako mwaka 2009 lilisikika likisema, chuki dhidi ya wageni pamoja na machafuko ya kijamii na kisiasa kwa nchi zilizoko Kusini mwa Afrika, katika kipindi cha Mwaka 2009, yalishuhudia idadi kubwa ya wahamiaji na wageni wakifukuzwa na kutotendewa haki na baadhi ya wananchi wa Afrika ya Kusini.

Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika, yalijitahidi kuhakikisha kuwa, wahamiaji na wageni hao, walau wanapata mahitaji yao msingi. Wahamiaji na wakimbizi hao, walikumbana na nyanyaso na ubaguzi kutoka kwa baadhi ya wananchi wa Afrika ya Kusini, jambo ambalo lilikuwa ni kikwazo kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, kwa kuwakumbusha wananchi hao, kwamba, wakati fulani katika historia ya maisha yao, walikuwa pia ni wahamiaji na wakimbizi, watu waliopata hifadhi na ukarimu kutoka katika nchi kadhaa za Kiafrika. Ustawi na maendeleo ya kiuchumi, kisiwe ni kikwazo cha kuwafanya wasahau taabu na mahangaiko ya ndugu zao kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

IMBISA: Xenophobia
17 September 2019, 14:50