Tafuta

Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania katika kupambana na: Ujinga, Umaskini na Magonjwa. Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania katika kupambana na: Ujinga, Umaskini na Magonjwa. 

Jubilei ya Miaka 50 ya ASC: Injili ya huruma na matumaini & mapendo

Damu ya Kristo, mto wa rehema ni chemchemi ya umoja na mshikamano wa watu kutoka katika kabila, lugha na jamaa waliokombolewa, tayari kuwashirikisha wengine ile furaha ya Injili. Ni katika muktadha huu, Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 2019. Dodoma kumekucha!

Na Padre Richard A.  Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, wanatambua dhamana na wajibu wao wa kuendelea kujitakatifuza, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Damu ya Agano Jipya na la milele, Fumbo la upendo, huruma na msamaha wa Mungu. Damu Azizi ya Kristo inawabidiisha kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuinua “Kalisi ya Matumaini” na hivyo kuweza kushiriki katika Injili ya furaha na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Damu ya Kristo, mto wa rehema ni chemchemi ya umoja na mshikamano wa watu kutoka katika kabila, lugha na jamaa waliokombolewa, tayari kuwashirikisha wengine ile furaha ya Injili inayowakutanisha na Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu. Ni katika muktadha huu, Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wao nchini Tanzania kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 2019.

Katika kipindi chote hiki, Waabuduo, au watoto wa “De Ma” wameshiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu ukimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watanzania na hususan, Jimbo Katoliki la Singida. Ni wanawake wa shoka waliosimama kidete kutetea utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi kwa kuwekeza katika elimu kwa wanawake na wasichana ili kuwajengea uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Wakaanzisha chuo cha ufundi na maarifa ya nyumbani, sekondari na chekechea, ili kupambana na adui ujinga na hatimaye, kumletea mwanamke wa kitanzania ukombozi wa kweli, unaomshirikisha hata yeye katika ujenzi wa Kanisa na taifa katika ujumla wake. Wamepambana na mila na desturi zilizopitwa na wakati bila kusahau mfumo dume! Leo hii kutoka Wilayani Manyoni kuna wasichana waliosoma na kufaulu kwenda vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Masista wa ASC., ni watawa ambao wameguswa na mahangaiko ya wagonjwa, wazee na watoto yatima; kiasi cha kusukumwa kuanzisha mchakato wa huduma ya tiba kwa kuwatembelea wagonjwa vijijini; hatimaye, wakaanzisha zahanati na kituo cha afya. Kijiji cha Matumaini ni kito cha thamani, amana na utajiri wa Injili ya huruma inayomwilishwa katika matendo, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha watoto yatima, waathirika wa Virusi vya ugonjwa wa Ukimwili pamoja na kuwajengea wanawake matumaini ya kuweza kujifungua watoto wakiwa salama hata baada ya kuambukizwa Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi. Kijiji cha Matumaini ni mahali ambapo, watoto waliokuwa wameegeshwa wakisubiri, waitwe na Baba wa milele, wameendelea kuwashangaza walimwengu, tangu umri wa miezi michache ya kuzaliwa, leo hii, wamemaliza masomo ya Sekondari na Vyuo, na baadhi yao wamerejea tena Kijiji cha Matumaini kutoa huduma kwa watoto walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi.

Watoto yatima, wameweza kupata mazingira ya kifamilia, wakaonja huruma na upendo kwa waamini walei wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watoto hawa kama familia zao kwenye Kijiji cha Matumaini. Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa Masista Waabuduo ni wimbo wa shukrani, sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huruma na upendo wake kwa maskini, wagonjwa na wale waliokata tamaa! Kijiji cha Matumaini ni kielelezo cha Injili ya matumaini kwa watoto yatima na wale walioathirika kwa virusi vya Ukimwi. Watoto wa “De Ma” wanaendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Penye nia panya njia! Kwa jicho la kibinadamu, unaweza kusema. Kijiji cha Matumaini ni mwanga angavu wa maisha na utume wa ASC nchini Tanzania. Huu ndio uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika majadiliano ya kiekumene na kidini kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanao sukumizwa pembezoni mwa jamii. Waabuduo wameshiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa awali Jimbo Katoliki la Singida, hususan katika Wilaya ya Manyoni.

Masista wa ASC wamekuwa bega kwa bega na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania. Wakasaidia katika katekesi na mafundisho ya dini: vigangoni na shuleni, ili kupandikiza na hatimaye, kustawisha mbegu ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala. Kuanzishwa na kuimarishwa kwa nyumba za malezi ni hatua muhimu sana ya kuendeleza maisha, utume na karama ya Shirika la ASC ndani na nje ya Tanzania. Hiki ni kipindi muafaka cha “kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.” Changamoto kubwa kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, ni kusimama kidete kuendeleza maisha na utume ulioanzishwa na waasisi wa Mashirika haya hususan katika nchi za Kimisionari kama ilivyo Tanzania. Kujitegemea na kulitegemeza Shirika, sadaka na majitoleo ya wanashirika wote ni chachu muhimu sana itakayowawezesha watawa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha ya changamoto, matatizo na magumu wanayoweza kukabiliana nayo katika maisha.

Umefika wakati wa kuwekeza katika elimu kama huduma na kitega uchumi; kwa kuwa na rasilimali watu walioandaliwa na kunolewa katika nyanja mbali mbali kadiri ya karama ya Shirika pamoja na kusoma alama za nyakati. Kwa njia hii wataweza kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wao wa Kiinjili, lakini pia watasaidia kulitegemeza Shirika kwa ajili ya mahitaji ya mchakato wa uinjilishaji. Sr. Bridget Pulickakunnel, ASC anapoyatafakari Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu anasema, “Tumeitwa kuishi kwa kuwajali wengine siyo kwa sababu wanatuhitaji sisi, lakini kwa sababu tumeumbwa na tunatamani sana kuendeleza utume wa Yesu katika mazingira ya sasa ambamo tunaishi. Mungu ambaye tunamwamini haishi peke yake, bali anaishi katika umoja na Mwana na Roho, siyo katika nadharia tu bali katika uhalisia. Kuishi na wanadamu wengine wasio wakamilifu mara nyingi husababisha usumbufu. Mara nyingi, katika hali kama hizo, mjaribu hujitokeza na suluhisho rahisi na zinzoonekana kufaa na kupitia njia nyepesi.

Tuna mifano kadhaa kutoka katika maisha ya Yesu mwenyewe, kama majaribu matatu jangwani (Lk 4, 1-13); Petro akijaribu kumshawishi Yesu akimbie Msalaba (Mk, 8, 32); umati ambao unamtafuta Yesu unamsubiri baada ya muujiza wa mikate ili kumfanya Mfalme wao (Yoh 6, 14-15). Katika nyakati hizo zote, kulikuwa na uhusiano wa moja kwa moja kati ya Nafsi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ambao ulimfanya Yesu aweze kuchagua njia sahihi, na, mara nyingi, njia sahihi ni ile ya mateso. Kwa hiyo ni vizuri kujiuliza: ninashughulika vipi na watu na hali ambazo zinanifanya kukosa raha? Je! Mimi ninasikiliza kwa makini sauti ya ndani wakati wa kutafuta majibu au suluhisho? Tumruhusu Roho Mtakatifu, aliyemwongoza Kristo yesu jangwani, pia awe kiongozi wetu katika kuishi "asaufi ya Damu ya Kristo”. Kwa Waabuduo, moyo wa shukrani ni tunu ambayo inawasukuma kusikiliza na kujibu kwa mtindo binafsi upendo mkuu wa Yesu Msulubiwa, ikiwapeleka kwenye kipimo cha uwepo wao katika Injili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Katika mchakato wa mabadiliko yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, wanasukumwa kurejesha tabia ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu na kwa jirani. Kwa hiyo, kukuza moyo wa shukrani kunamaanisha kuendelea kuupyaisha ubinadamu wao na hivyo kukua katika tunu msingi za Injili ya upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa. Kimsingi upendo na huruma ni fadhila kubwa zinazopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Mama Kanisa!

ASC. Jubilei 50
20 September 2019, 15:12