Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 26 ya Mwaka C wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ana upendeleo wa pekee sana kwa maskini. Jengeni utamaduni wa kuwapenda na kuwathamini maskini. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 26 ya Mwaka C wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ana upendeleo wa pekee sana kwa maskini. Jengeni utamaduni wa kuwapenda na kuwathamini maskini.  (AFP or licensors)

Tafakari Jumapili 26 Mwaka C: Upendeleo wa Mungu kwa maskini!

Tajiri na mwenye mali alionwa kama mtu aliyepewa upendeleo fulani na Mungu. Kinyume cha mtazamo huu, Yesu anaonesha kuwa utajiri na mali si lazima viwe ni alama ya upendeleo wa Mungu kwa mtu, tena vinaweza kuwa ni sababu ya kumtenga mtu na Mungu. Yesu anaonesha kwamba, utajiri si kosa hata kidogo. Kosa lake lilikuwa ni kutokumjali masikini Lazaro aliyekuwa jirani naye.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 26 ya mwaka C wa Kanisa. Lazaro maskini na tajiri ambaye hakuguswa na mahangaiko ya Lazaro. Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 inaadhimishwa Jumapili,  tarehe 29 Septemba, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Si Wahamiaji peke yao”. Baba Mtakatifu  Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Hili si suala la wahamiaji na wakimbizi peke yake, bali linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kutowatenga watu kwa sababu ya maamuzi mbele, kwani kwa kufanya hivi, ni kuendeleza ukatili dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawataka wahamiaji na watu wenye mashaka wawe na imani, matumaini na mapendo katika kukabiliana na changamoto za vurugu na migogoro ya kiuchumi na kijamii inayoendelea kusambalatisha hali ya utu na heshima ya binadamu ulimwenguni.

Somo la kwanza (Amo 6:1°, 4-7 ) ni kutoka katika kitabu cha Nabii Amos. Amos alifanya utume wake wa unabii katika kipindi ambacho Israeli ilikuwa imeshamiri sana kiuchumi. Ushamiri huu lakini haukuendana na ushamiri wa kimaadili, ushamiri wa haki wala ule wa kiimani. Katika somo la leo Nabii anakemea juu ya utofauti mkubwa wa maisha kati ya wenye nacho na wasio nacho. Waliokuwa matajiri walizidi kuishi maisha ya starehe na ya anasa ilhali masikini walizidi kuteseka kwa kukosa mahitaji yao. Maisha ya starehe ya matajiri yalijionesha kwa kupenda kwao kuimba nyimbo za upuzi, kujifanyia vinanda vya namna nyingi na kunywa divai katika mabakuli badala ya kutumia vikombe au glasi.  Nabii Amos anawaalika wawafikirie masikini na tena watambue kuwa wanao wajibu wa kuwasaidia.

Somo la pili (1 Tim 6, 11-16) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timoteo. Huu ni Waraka wa kichungaji ambao Paolo anauandika ili kutoa maelekezo ya kichungaji katika Makanisa na jumuiya ambazo Paulo mwenyewe alizianzisha. Hapa anamwandikia Timoteo aliyemweka kuwa Askofu wa Kanisa la Efeso ambalo yeye mwenyewe Paulo alilianzisha. Katika somo la leo Paulo anamwasa Timoteo kuishika imani sawasawa na kuiungama katika maisha yake ya utumishi. Anamwandikia kusisitiza kuwa kuiungama imani ni kuyakimbia matendo maovu, kujiepusha na uovu na kuchuchumalia fadhila njema: haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

Injili (Lk 16:19-31) Katika Injili ya dominika ya leo Yesu anatoa mfano wa mtu mmoja tajiri na maskini aliyeitwa Lazaro. Yesu anautoa mfano huu kugeuza mawazo ya watu kuhusu utajiri na mali. Kwa mtazamo wa kiyahudi, utajiri na mali vilionekana kama alama ya baraka kwa Mungu. Tajiri na mwenye mali alionwa kama mtu aliyepewa upendeleo fulani na Mungu na alionekana kama mtakatifu. Kinyume cha mtazamo huu, Yesu anaonesha kuwa utajiri na mali si lazima viwe ni alama ya upendeleo wa Mungu kwa mtu, tena vinaweza kuwa ni sababu ya kumtenga mtu na Mungu. Katika mfano huo Yesu anaonesha kuwa kosa la tajiri halikuwa kuwa tajiri. Kosa lake lilikuwa ni kutokumjali masikini Lazaro aliyekuwa jirani naye. Tajiri hakumuona Lazaro kama mtu aliye na hadhi kama yake na ambaye ni mtu mwenye mahitaji. Alimuona tu kama kitu au kama uoto wa kawaida wa asili. Hakumtendea wema. Mwisho wa mfano Yesu anaonesha kuwa wakati wa kubadilisha mitazamo ya maisha ndiyo sasa. Wajumbe wote wa Mungu na misaada yote ya kimungu ya kutusaidia tunayo sasa. Tuitumie. Tusisubiri hadi mtu afufuke kutoka wafu au ashuke toka mbinguni ndipo tujirekebishe. “ wanao Musa na manabii, na wawasikilize wao”.

Liturujia J26
30 September 2019, 08:55