Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 23 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Masharti ya ufuasi wa kweli kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 23 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Masharti ya ufuasi wa kweli kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka: Mfuasi wa kweli wa Yesu!

Hekima inayomwongoza mtu katika njia ya wokovu ni zawadi ya Mungu, ni tunda la Roho Mtakatifu. Mtu peke yake hana ufahamu huo. Mungu hawanyimi watu wake hekima hiyo. Katika somo la injili twaona kuwa siyo jambo rahisi kuwa mfuasi wa Kristo. Yatakiwa tafakari, ufahamu na ung’ang’anizi. Ni ufuasi unaotuweka huru na malimwengu, ikiwa na maana kuwa Kristo ndiye yote.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma

Neno la Mungu latuongoza kutafakari juu ya ufuasi unaoongozwa na upendo kwa Mungu aliye sababu ya maisha yetu. Tunaalikwa kujipanga vizuri na kupiga mahesabu vizuri ili tuweze kukamilisha na kuufikia ule mwaliko mtakatifu aliotushirikisha Bwana. Lengo ni kurithi mbingu. Katika somo la kwanza twaona kuwa hekima inayomwongoza mtu katika njia ya wokovu ni zawadi ya Mungu, ni tunda la Roho Mtakatifu na hutoka juu. Mtu peke yake hana ufahamu huo. Mungu hawanyimi watu wake hekima hiyo. Katika somo la injili twaona kuwa siyo jambo rahisi kuwa mfuasi wa Kristo. Yatakiwa tafakari, ufahamu, bidii na ung’ang’anizi. Ni ufuasi unaotuweka huru na ulimwengu, ikiwa na maana kuwa Kristo ndiye yote. Katika mifano miwili inayotololewa katika injili, twaambiwa kuwa Yesu hakutoa maelezo ya kina kwa kile alichosema lakini baadaye wataalamu wanasema Yesu alitaka kusema kuwa tuwe makini na kukamilisha vizuri kile tunachofanya.

Mtakatifu Gaspari del Bufalo, muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu anasema, kwa Mungu ni lazima kufanya mengi, vizuri na haraka. Mengi kwa sababu ndivyo inavyotakiwa, vizuri kwa vile ndivyo impendezavyo Mungu na haraka kwa vile maisha yetu ni mafupi. Hakika ufuasi unatudai mambo mengi na makubwa. Tukumbuke kuwa ipo tofauti kubwa kati ya wafuasi wa Mafarisayo na wafuasi wa Yesu. Wafuasi wa mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakienda huku na huko na walichagua walimu na pia kitu walichotaka kusikia na mafundisho waliyoyapenda halafu kuchagua mwalimu waliyempenda zaidi. Mwanafunzi huyu aliitwa talmid hakam au mwanafunzi wa hekima. Mfuasi huyu alimchagua mwalimu na hata kitu alichotaka kusikiliza. Ufuasi wa Yesu ni tofauti. Yesu alikuwa na ujumbe maalumu aliotangaza, wengi walisikiliza huo ujumbe na kuufanya sehemu ya maisha yao. Lakini zaidi ufuasi wa Kristo katika Agano Jipya ni kule kujitoa kabisa kwa Bwana.

Siyo kusikiliza ujumbe fulani tu, bali utambulisho wa mfuasi wa Kristo ni kujitoa kabisa kwa Bwana. Hili halihitaji akili ya juu sana au uwezo wa pekee wa kuelewa mambo n.k Ili kuelewa hili tazama mifano miwili atoayo Yesu katika Injili. Matumizi ya maneno katika mifano yaweza kutuchanganya. Neno kuchukia katika lugha ya Kiebrania lieleweke kupenda kidogo (angalia Mt. 10,37 – anayempenda baba au mama zaidi yangu hafai kwa ufuasi). Hivyo wito hapa ni kumtanguliza Kristo na kutoka hapa mahusiano mengine yote yanapata maana katika maisha yetu, hata yale ya familia. Kuachana huku na mali kunakosemwa na Yesu ni kule kuwa huru na kufungamanishwa nayo. Nguvu ya kweli na mweza ya yote ni Yesu pekee. Katika mwendelezo wa fundisho lake leo, Kristo anatualika kuchukua msalaba – kwa nini? Kuacha yote kwa nini? Bila shaka hana maana kuwa tutafute mateso au matatizo.

Tunaambiwa kuwa Yesu hakutafuta Msalaba ila alichukua kwa utii Msalaba. Alimtii Baba yake kama alama ya upendo na utii kwake. Pengine hii ndiyo hekima ya kweli kama tusomavyo katika somo la 1 na wito mpya kama Paulo anavyoshuhudia kwa Onesmo. Hakika Yesu hakuja kufanya migumu misalaba yetu au maisha yetu. Ila kutoa maana mpya kwa maisha yetu. Husemwa kuwa yeye amfuataye Kristo bila msalaba, atapata msalaba bila Kristo. Kwamba ataupata msalaba lakini bila nguvu ya kimungu ndani yake ya kuubeba. Tukumbuke kuwa upendo kwa Kristo huimarisha mapendo mengine, maana katika yeye upendo wa kweli hupata maana na msingi wa kudumu na neema ya Mungu yaweza kuonekana. Upendo wa kweli wa mume na mke katika sakramenti ya ndoa huonekana katika upendo wa Kristo kwa kanisa lake. Katika Efeso 5:2 tunasoma maneno haya – mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi, tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.

Maisha halisi ya ufuasi huonekana katika mapendo kamili kama alivyotupenda Bwana. Katika somo la pili twasikia habari juu uzima mpya wa Kristo. Sisi siyo watumwa tena, bali watufanya ndugu katika Bwana. Katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika’, uk. 55 ikitoka katika kitabu cha ‘Our Ancestors in Faith’ tunapata habari ya maisha ya ujasiri ya kina Karoli Lwanga na wenzake wafia dini mashahidi wa Uganda. Yosefu Mukasa alikuwa wa kwanza kuuawa na baadaye usukani wa kundi ukachukuliwa na Karoli Lwanga. Alihakikisha na kuhamasisha kundi libaki aminifu. Walikaidi amri ya ufalme na wakaweka matumaini yao yote kwa Mungu. Walipoamrishwa kumkana Kristo, Bruno mmoja wa mashujaa chipukizi alisema kwa utulivu, ‘unaweza kuichoma moto miili yetu, lakini hutaweza kuziunguza roho zetu. Roho zetu zitakwenda Paradiso’.  Huu ndio ufuasi wa kweli na maisha mapya katika Kristo. Katika msalaba wa Kristo wanapata utukufu. Hakika hatuna budi kujipanga upya na kujipanga vizuri. Hatuna budi kumjua vizuri adui wa ufuasi wetu na kutafuta mbinu nzuri za kumkabili na pia kuzifahamu vizuri zana nzuri za ujenzi na kuzitumia ili tuweze kufika mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

11 September 2019, 17:40