Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIV ya Mwaka C wa Kanisa: Dhambi ni chanzo kikuu cha mateso na mahangaiko ya mwabnadamu! Toba na wongofu wa ndani ni muhimu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIV ya Mwaka C wa Kanisa: Dhambi ni chanzo kikuu cha mateso na mahangaiko ya mwabnadamu! Toba na wongofu wa ndani ni muhimu!  (AFP or licensors)

Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka: Dhambi ni chanzo cha mateso!

Liturujia ya Neno la Mungu inatuongoza kumtazama Mungu ambaye ni Baba mwenye furaha, huruma na mapendo. Amejifunua kama Mungu mwenye furaha na anaishirikisha furaha yake pale mapenzi yake yanapotimia. Dhambi inabaki kuwa tatizo linaloleta mahangaiko makubwa katika maisha ya mwanadamu. Jibu la mwanadamu katika dhambi ni: Unyenyekevu, Toba na Wongofu.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji, karibu katika tafakari ya Dominika ya 24 ya Mwaka C. Maandiko Matakatifu yanatuongoza kumtazama Mungu ambaye ni Baba mwenye furaha, huruma na mapendo. Mwenyezi Mungu anajifunua kwa taifa lake kama Mungu mwenye furaha na anaishirikisha furaha yake pale mapenzi yake yanapotimia. Aidha dhambi inabaki kuwa tatizo linaloleta mahangaiko makubwa katika maisha ya mwanadamu.  Jibu la mwanadamu katika dhambi ni kunyenyekea na kumrudia mwenyezi Mungu ili kupata furaha ya milele katika upendo wa kibaba. Katika somo la kwanza, linalotoka kitabu cha Kutoka (kut 32 7-11, 13-14):Furaha ya Mungu, huruma ya Mungu na upendo wa Mungu unapimwa kwa kukengeuka kwa mwanadamu. Taifa la Israeli ambalo Mungu alipenda kulichagua kuwa mfano wa mataifa mengine linamwasi kwa kujitengenezea “mungu wa kuchonga” yaani sanamu na kumtega Mungu mgongo wakianza kuiabudu sanamu waliyoichonga kwa mikono yao. Furaha ya Mungu haitenganishwi na ukweli kuwa Mungu ni Baba mwenye kufundisha ukweli, hasira yake si ya kuangamiza bali ya kufundisha, anamsikiliza mtumishi wake Musa na kuwasamehe waisraeli kosa lao la kutokuwa waminifu katika ibada zao.

Katika somo la Pili linalotoka waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timotheo(1Tim 1,12-17): Mtume Paulo kama mlezi wa Timotheo anamshirikisha kijana wake uzoefu wake wa kimisionari. Anmwambia “mwanangu namshukuru Mungu anayenitia nguvu” Paulo anakiri udhaifu wake wa hapo mwanzo kabla ya kuipokea Injili, na nmna alivyoonja huruma ya Mungu isiyo na mipaka, ikamugeuza na kumfanya kiumbe kipya. Furaha hiyo aliyo nayo Paulo siyo ya kwake tu bali inapaswa kushirikishwa kwa watu wote. Mtume Paulo anakiri wazi kabisa kuwa furaha kuu kuliko zote ni pale mkosefu anapomrudia Mungu wake na kuendelea na furaha, kumtukuza Milele yote. Katika somo la Injili linalotoka katika Injili ya Mtakatifu Luka (Lk 15 1-32): Furaha, huruma na mapendo ya Mungu yanajifunua katika mifano mitatu tofauti lakini yenye fundisho moja. Ni kutokana na mfano swali mfano wa mkuki unaochoma moyo na kuifungua hazina ya furaha, huruma na mapendo ya Mungu. Swali la mfarisayo lenye kumshangaa Mungu kuhusika na wadhambi lemeleta mambo matamu na yenye hekima. Kutoka swali hilo Yesu asimulia asili ya Mungu ya kiuchungaji na mahangaiko ya kupotea kwa kondoo.

Yesu anafananisha na hisia ya kawaida kabisa ya mwenye kondoo wake malishoni kupotelewa na badhi ya kondoo wanaotoroka kundini wakifikiri watapata malisho mazuri wakiwa peke yao. Mchungaji anahuzunika kumpoteza kondoo wake na kumnyima ukamilifu wa furaha yake, mchungaji anafanya bidii ya kumtafuta kondoo wake akiwaacha wengine mahali salama, arudipo baada ya kumpata anakuwa na furaha kuu, Yesu anatufundisha kuwa ndivyo Mwenyezi Mungu anavyohangaika kumrudisha kondoo wake alipotea na kusababisha furaha kuu mbinguni. Aidha, Yesu anatoa mfano mwingine wenye kufanana. Mwanamke katika himaya yake anapoteza pesa yake na kumsababishia msongo wa mawazo maana bila kuipata hiyo sehemu iliyopotea fedha yake haijakamilika kama ilivyokuwa. Mfano huu unadokeza furaha ya Mungu katika ukamilifu wake, mwanamke anaonekana daima mwenye furaha baada ya kuiona sehemu ya pesa yake iliyokuwa imepotea na anawashirikisha majirani zake furaha yake. Mfano wa mwanamke daima hutukumbusha fumbo la Kanisa ambamo furaha za Mungu hushirikishwa katika ukamilifu wake. Mfano wa tatu ni wa mahusiano ya kifamilia, Yesu anagusa familia zetu akijifunua Yeye mwenyewe kama chanzo cha maisha ya jumuiya.

Mwinjili Luka anatukumbusha kuwa mtindo wa dhambi ni uleule wa kutaka kujifurahisha katika ubinafsi, kuchukua riziki na kwenda kulia mbali , ili usiombwe na wahitaji. Ndivyo yule kijana mdogo anavyotawaliwa na ubinafsi na kuomba haki zake, anapewa na Baba yake na kuondoka kwenda kufurahia maisha, afikapo huko anatapanya ovyo mali zake, mali zinaisha na kugeuka kuwa ombaomba, anajaribu kutafuta kibarua lakini nacho kinakuwa na manyanyaso ya kutosha, hii ndiyo malipo ya dhambi. Anazingatia moyoni katika tafakari za kina, anapata jawabu la kujinyenyekesha na kuanza safari ya kurudi katika moyo wa toba na kutokustahili, amejiwekea mikakati mizito ya kutorudia tena ujinga alioufanya, anapofika nyumbani anashangazwa na mapokezi ya Baba yake anayembusu sana na kumvika nguo mpya, na kuadhimisha furaha pamoja. Hakika uzoefu alioupata kijana mdogo haungeweza kufutika kirahisi moyoni mwake.

Mwinjili Luka hakuishia hapo, bali anasonga mbele kueleza hali ya kijana mkubwa ambaye alibaki na Baba yake na kuwa mwaminifu katika kumtumikia, lakini hakuwa mbunifu wa kushirikisha upendo wake kwa wengine. Hii inajipambanua hata wakati wa kurudi kwa mdogo wake, hapakuwa na sababu ya kuhoji baada tu ya kusikia mdogo wake amesharudi, alipaswa kukimbia kwa furaha na kuungana naye katika kuadhimisha furaha yake. Lakini kijana huyo kwa kukosa mapendo ya kweli kwa mdogo wake anamung’ang’ania Baba yake kwa maswali mengi. Na jibu lake linakuwa ni moja tu, tunapaswa kufurahi kwa maana ndugu yetu amepatikana akiwa hai. Kumbe, Yesu alitaka kuwaambia mafarisayo na watu wote wanaojidai kuwa wanashika sheria za Mungu bila kuwa na upendo wa dhati ndani yake.  Maana Mungu ni Upendo. Na furaha ya milele aliyowaandalia watu wake hufumbatwa katika maisha ya huruma kwa wakosefu. Mungu hamchukii mdhambi lakini huchukia dhambi yake, ndiyo maana anamwita kila wakati kuacha kufanya kitu kinachomchukiza na badala yake atimize mapenzi yake.  Hii ndiyo maana ya kuwa Mungu mwenye furaha, huruma na mapendo.  TUMSIFU YESU KRISTO.

Neno J24 Mwaka
15 September 2019, 08:59