Tafuta

Vatican News
Wakatoliki nchini Malawi wanahimizwa kusoma kufungua Neno la Mungu kutoka katika Biblia kila siku Wakatoliki nchini Malawi wanahimizwa kusoma kufungua Neno la Mungu kutoka katika Biblia kila siku 

MALAWI:wakatoliki wahimizwa kusoma Biblia kila siku!

Katika harakati za kujiandaa na maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari,Oktoba 2019,Kanisa Katoliki nchini Malawi,wamezindua mwezi wa kusoma Biblia Takatifu kila siku.Kuanzia Mosi Septemba,kila mbatizwa anahimizwa kuwa na Biblia ili kusoma Neno la Mungu,kulielewa na kutalingaza kwa kila kiumbe.Wapo wakatoliki wengi wanao changamotishwa sana kutokana na kutojua Neno la Mungu.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Wakatoliki nchini Malawi wanashauriwa kusoma Biblia kila siku. Haya yamesemwa wakati wa Maadhimisho ya Misa Takatifu tarehe Mosi Septemba 2019 wakati wakizindua Mwezi wa Biblia katika Parokia moja ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Kuu Katoliki la Lilongwe. Akizungumza wakati wa maadhimisho Padre Henry Zulu amesema wote waliobatizwa wanatumwa kutangaza Injili. Kazi ya wamisionari kwa namna hiyo wanahitaji kukuza uelewa wao wa kina kuhusu Neno la Mungu ambalo linaweza kupokelewa tu na kuendelea kukuza njaa ya na kiu ya kuhisi kusoma Neno la Mungu.

Mwendelezo wa Mwezi wa Biblia unakuja kabla ya Mwezi Maalum wa kimisionari

Padre Zulu akifafanua kuhusu mwezi huo amesema, mwezi wa Biblia kwa mwaka huu unakuja mapema kabla ya mwezi Maalum wa Kimisionari 2019 unaotarajiwa Oktoba na ambao unakumbusha kila mkatoliki mbatizwa na kazi yake ya kutangaza Neno la Mungu katika ulimwengu mzima. Kusoma biblia kila siku, ni muhimu kwa maana wakristo hawawezi kushirikisha kile wasichokuwa nacho mioyoni mwao! Padre Zulu ambaye ni Mratibu wa Biblia Jimbo Kuu katoliki la Lilongwe, aidha amewasihi waamini wote katoliki nchini Malawi kuendeleza utamaduni wa kusoma Biblia kila siku ili waweze kuwa na uelewa mzuri wa Neno la Mungu na kuweza kulishirikisha Neno hili kwa wengine wakati wa sherehe za Kanisa, ibada na shughuli nyingine na zaidi kuimarisha kwa kina imani yao.

Umuhimu wa kusoma toleo jipya la Majibu ya Biblia Katoliki

Na kwa mujibu wa maelezo yake, balozi wa Biblia kwa ajili ya kutoa Jibu jipya Katoliki la Biblia  Dk. Saulos Chilima na ambaye ni Makamu Rais mstaafu wa Jamhuri ya nchi ya Malawi, amesema Wakatoliki wengi hawajuhi ni kwa nini baadhi ya Ibada za Kanisa na maadhimisho yake yanafanyika. Aidha amesema wakatoliki wengi pia wanapata changanoto nyingi kutoka kwa baadhi ya Makanisa ya kikristo na dini nyingine zilizomo nchini humo na wanapata shida hasa ya kuweza kutetea imani yao katoliki. Utangulizi wa toleo jipya la majibu ya Biblia Katoliki ambalo lina maswali 88 ya pamoja yanayo ulizwa mara kwa mara na majibu yake Kikatoliki ni muhimu sana ili Wakatoliki waweze kuwa na  uelewa wa kujizatiti kwa kina imani yao. Amehimiza kwamba familia zote katoliki wanunue Biblia na  zaidi kila mtu ndani ya  familia. Ni kwa njia ya kusoma Biblia tu amesisitiza, inawezekana kuelezea kwa nini wakatoliki wanasali Rosari; kwa nini wanaomba kupitia maombi ya watakatifu,na kwa nini kutoa Sakramenti ya mpako wa wagonjwa. Mwezi wa Septemba ambao umetolewa kusali unataka kuwakumbusha wakatoliki wote umuhimu wa kusoma Biblia katika maisha ya kila mmoja  na kila mbatizwa yeyote yule!

Ufahamu wa kujua Biblia ni muhimu, asili, historia, waandishi na mipaka yake

Wanadamu bila ya Mungu wanajipeleka kwenye uangamizi wa sayari hii kwa vile wamejitenga na Muumba wao Mungu,Na kama siku hizo zisingalifupizwa, hakuna mtu yoyote angeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitapunguzwa siku hizo. Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. (Mathayo 24:22-26) . Ni watu wachache tu wanalielewa hili kwa usahihi, na kile ambacho Mtume Petro alisema, kwamba Yesu ndiye “aliye na maneno ya uzima wa milele” (Yohana 6:68).

Ni lazima kujua Biblia imeundwa namna gani

Lazima kujua kwamba Biblia ni mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vinavyohusu kazi ya Mungu ya kuwakomboa mwanadamu kuanzia enzi za Mababu na manabii wa Waisraeli, enzi za Yesu na za Mitume wa Yesu. Biblia iliundwa kwa kukusanya vitabu vya dini vya wakristo hapo zamani na kuunda kitabu kimoja. Kwa maana hii, Biblia ni vitabu teule vya dini vilivyoonekana vinafaa kutumika kwa waamini,Wakristo ili kusaidia imani yao iwe imara zaidi. Na kama Biblia ni vitabu teule tuu, lakini pia ni  lazima kutambua ya kwamba vipo hata vitabu vingine vya dini ambavyo havikuwekwa kwenye Biblia. Biblia kwa hakika ni mwongozo wa maisha, ni historia hai inayozungumza kila wakati,  enzi za kale, za kati na sasa! Ni Mungu mwenyewe anayezungumza na watu wake, na anayeendelea kuzungumza kila wakati, yaani jana, leo na kesho. Biblia inasaidia kufundishia, ibada na kukuza imani. Na vitabu vingine Katoliki vinasaidia katika mchakato mzima wa historia ya ukombozi wa mwanadamu kamili.

Kanisa katoliki pia linatumia  mapokeo na Maandiko ya Watakatifu

Kuhusiana na vitabu vingine, Kanisa katoliki linatumia  vitabu vingi kuliko madhehebu mengine mengi ambavyo pia vinaitwa mapokeo na Makala au maandishi ya watakatifu kwa imani kwamba Mungu yule yule aliyezugummza, aliyefanya kazi tangu zamani, anazungumza na anafanya kazi na watu wake mpaka sasa, hivyo Maandiko ya watu wa Mungu yanafaa kutumika kama yalivyotumika ya watu wa kale. Kadhalika  Kanisa Katoliki linatumia pia Hati mbalimbali za Mababa wa Mtaguso, Mababa watakatifu wa nyakati zote hadi sasa. Na Maandiko ya Watakatifu, ni kwa ajili ya kuwaimarisha imani yao waamini wote katika kumfuasa Kristo Mungu pia katika safari yao ya kiroho kwa kila mwaamini.

Jambo muhimu la kukumbuka kutoka katika Injili ya Yohane

Yesu alituambia hivi katika: "Ninayo mengi ya kuwaambieni ila kwa sasa hamuwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa Ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote. Maana hatasema kwa Mamlaka yake mwenyewe bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. Yeye atanitukuza Mimi kwa kuwa atawajulisheni Yale atakayo yapata kutoka kwangu"(Yohane 16:12-15). Vile vile  habari ni nyingi za mambo ya Kanisa, mitume na wakristo, walipoanza kuhubiri Injili na matendo ya Yesu ambapo wanasema hayakuweza kuandikwa: “Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yangeandikwa yote moja baada ya nyingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka  vitabu ambavyo vingeandikwa". ( Yh 21, 25). Huu ni uthibitisho hai ambao kwa wakatoliki tunaamini na kupitia katika maandiko ya mapokeo na hati mbalimbali, ni ushuhuda hasa kwamba Mungu bado anaendelea kuwapo katika historia ya mwanadamu.

09 September 2019, 16:05