Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar linasema, familia ya Mungu nchini humo ni watu wenye imani thabiti; wanathamini maisha ya binadamu kwani ni matakatifu! Lakini....!	Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar linasema, familia ya Mungu nchini humo ni watu wenye imani thabiti; wanathamini maisha ya binadamu kwani ni matakatifu! Lakini....!  

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Changamoto & Utume wa Kanisa

Ukosefu wa ulinzi na usalama ni changamoto inayotishia maisha ya watu wengi, lakini kila mmoja akitekeleza dhamana na wajibu wake, Madagascar inaweza kubadilika na kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Madagscar inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Dèsirè Tsarahazana, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Toamasina, na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Madagascar anasema, ni furaha isiyokuwa na kifani watu wa Mungu kumpokea na kumkarimu Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea nchini mwao; moja ya nchi maskini sana duniani, lakini imesheheni utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu. Madagascar imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa madini, misitu asilia na imezungukwa na Bahari ya Hindi. Lakini, utajiri mkubwa kuliko vyote ni rasilimali watu! Kanisa Katoliki nchini Madagascar liko mstari wa mbele katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Kardinali Dèsirè Tsarahazana, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Madagascar, Jumamosi, tarehe 7 Septemba 2019 katika risala ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar amependa kumhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, mbele ya macho yake kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu wenye imani thabiti kwa Mungu muumbaji wa vyote vinavyoonekana na vile visivyonekana; Baba na asili ya maisha na kwamba, Madagascar ni mahali ambapo maisha ya binadamu yanathaminiwa sana kwani ni matakatifu. Ni kutokana na muktadha huu, familia ya Mungu nchini Madagascar inajikuta ikiwa na udongo mzuri wa kuweza kupokea Injili ya Kristo Yesu.

Kanisa nchini Madagascar limekuwa daima mstari wa mbele kupambana na umaskini, rushwa na ufisadi; ukosefu wa usawa na haki msingi za binadamu. Ukosefu wa ulinzi na usalama ni changamoto inayotishia maisha ya watu wengi, lakini kila mmoja akitekeleza dhamana na wajibu wake, Madagascar inaweza kubadilika na kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Familia ya Mungu nchini Madagscar inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutembelea nchi yao. Ujumbe wake wa matumaini na amani unagusa na kukita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo zao. Huu umekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato mzima wa kuendelea kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Kardinali

 

07 September 2019, 17:32