Wakleri na watawa nchini Madagascar wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko matumaini, changamoto na fursa walizo nazo katika mchakato wa uinjilishaji wa kina. Wakleri na watawa nchini Madagascar wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko matumaini, changamoto na fursa walizo nazo katika mchakato wa uinjilishaji wa kina. 

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Mashuhuda wa uinjilishaji wa kina!

Nguvu ya Kristo inayojidhihirisha katika udhaifu wao ndiyo inayowaimarisha ikiungana na mwitikio chanya unaowafanya wawe na bidii za kutekeleza majukumu yao kwa nguvu zao zote katika utume wa shamba la Bwana na wakisaidiwa na mastahili ya Mama Kanisa. Katika muungano huo wa dhati, wameweza kujitoa kikamilifu kwa ukarimu wa maisha yao yote kwa Mungu na Kanisa.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Makundi mabilimbali ya wakleri, watawa, waseminari na wanovisi yakutana na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Septemba 2019 katika Chuo cha Mtakatifu Mikaeli wa Antananarivo wakimpokea kwa furaha kuu na ndelemo za kukata na shoka. Katika hali hiyo ya furaha walimshirikisha mafanikio na changamoto kubwa wanazokumbana nazo katika utume wa uinjilishaji ambazo nimepyaishwa kwa ujio wa Baba Mtakatifu nchini Madagascar na kwa mafundisho yake yaliyojengwa katika kauli mbiu ya “Mpanzi wa amani na matumaini” ambayo inakonga nyoyo za watu. Aidha furaha yao imezidi kukua kwa sababu ya unyenyekevu na moyo wa dhati wa Baba Mtakatifu wa kuwajali maskini na kutetea wanyonge ulimwenguni kote.  Kiongozi mwakilishi na msemaji mkuu wa makundi hayo Sr. Suzanna Maria Raharisoa ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume nchini Madagascar, alimkaribisha Baba Mtakatifu kwa furaha kubwa akiyatambulisha makundi mbalimbali yaliyokuja kumlaki kwa nyimbo na nderemo. Mchana huo uliopambwa vifijo na cherekochereko za kihistoria kutoka kwa watumishi wa Kanisa, wamemweleza Baba Mtakatifu hisia zao, upendo wao kwa Kanisa na matumaini yao kwa wakati ujao.

Sr. Suzanna Maria Raharisoa aligusa nyanja zote muhimu zinazoeleza utumishi fungamani katika sekta mbalimbali za Kanisa. Akiambatanisha mafanikio hayo na shukrani za dhati kutoka kina cha mioyo ya wahudumu wa Kanisa, amesema wakleri na watawa kwa ujumla wao wanampongeza sana Baba Mtakatifu kwa moyo wake wa kibaba na majitoleo yake hasa ya kuwajali watu maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Bidii hizo za Baba Mtakatifu zimezaa mbegu njema nchini madagascar inayodhihirishwa na ziara yake ambayo inagusa maisha ya watu wengi wakatoliki na watuwa imani mbalimbali.  Sr. Suzanna Maria Raharisoa amemdhihirishia nia ya dhati na ari ya kiutume waliyo nayo katika kupambana na changamoto za kiutume. Nguvu ya Kristo inayojidhihirisha katika udhaifu wao ndiyo inayowaimarisha ikiungana na mwitikio chanya unaowafanya wawe na bidii za kutekeleza majukumu yao kwa nguvu zao zote katika utume wa shamba la Bwana na wakisaidiwa na mastahili ya Mama Kanisa. Katika muungano huo wa dhati, Sr. Suzana Maria Raharisoa amesema, wameweza kujitoa kikamilifu kwa ukarimu wa maisha yao yote wakijikabidhi mikononi mwa Mungu na Kanisa lake kwa furha kubwa. 

Injili imekuwa chanzo cha furaha ya mioyo yao inayowatuma kujisadaka bila kujibakiza katika utumishi wao. Sr. Suzanna Maria Raharisoa amekazia kusema Injili kama furaha ya mwanadamu imepyaisha maisha yao na kuwafanya wawe marafiki wa Mungu na kuimarisha ujirani kati yao. Aidha wanajisikia kuwajibika bila kuchoka katika kutoa huduma zao kwa wahitaji wanaowatumikia.  Jitihada hizi za uenezaji Injili zimejidhihirisha katika sekta ya elimu na afya ambapo wanaendelea na malezi ya Miito mitakatifu ya upadre na utawa wakiwasaidia vijana kupambanua na kuitikia wito wao wa kumtumikia Mungu katika maisha yao. Sanjari na hilo wameweza kujenga Hospitali Vituo mbalimbali vya afya kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwa huruma na utulivu mkubwa.  Jitihada hizi fungamani zinaeleza lengo la kumkomboa mwanadamu kimwili na kiroho na kumsaidia kujitambua ili ashiriki vyema katika utunzaji wa mazingira iliyo nyumba ya Pamoja.

Pamoja na taarifa hiyo ya mafanikio makubwa katika utume wa Kanisa nchini Madagascar wakleri, watawa na wenye maisha ya wakfu wamemshukuru sana Baba Mtakatifu kwa kufanya ziara yake na kutambua uwepo wake. Wamejifunza kutoka kwake moyo wa kibaba na kumwomba azibariki fikra, hisia, na kazi zao ziweze kuwa takatifu zenye kumpendeza Mwenyezi Mungu. Wakiendelea kujiweka mikononi mwa Mungu na Kanisa lake wamemwomba apokee sadaka ya maisha yao ya kiroho yanayojipambanua katika uaminifu, utii na ufukara wa maisha yao ya kijumuiya. Aidha waliendelea kumfahamisha changamoto iliyoko mbele yao inayowahitaji kwenda zaidi kwenye vijiji na sehemu silizosetwa na jamii kwa ajili ya kupanda mbegu ya neno la Mungu. Kazi hii daima huwa na ugumu wake lakini hata hivyo wanajikabidhi mikononi mwa Mungu aneyewawezesha kujisahau kwa ajili ya wengine na kwa ajili ya injili. Wakitambua ugumu wa changamoto hii walimwomba Baba Mtakatifu aendelee kuwaombea katika sala zake za kila siku. Akionesha furaha kubwa waliyokuwa nayo wakleri, watawa,waseminaristi na wanovisi walimkaribisha tena nchini Madagascar.

 

09 September 2019, 17:58