Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha na vijana amesikiliza shuhuda na changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kizazi kipya nchini Madagascar. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha na vijana amesikiliza shuhuda na changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kizazi kipya nchini Madagascar.  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Shuhuda, matatizo na changamoto za vijana

Vijana wamemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko changamoto za ukabila wanazokabiliana nazo nchini Madagascar kutokana na tofauti za kitamaduni, mila na desturi; lakini kwa njia ya uvumilivu na upendo wa kifamilia, wamebahatika kuzivuka na sasa ni sehemu ya amana na utajiri wa wananchi wa Madagascar katika ujumla wao. Vijana wanataka kuandika ukurasa wa matumaini! VIJANA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 7 Septemba 2019 ameongoza mkesha wa umati mkubwa wa vijana kutoka ndani na nje ya Madagascar. Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar linasema, uwepo mubashara wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kutoka Madagascar ni ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo kutoka kwa watoto wa Kanisa nchini Madagascar. Wanamtambua Baba Mtakatifu kama Mchungaji mwema anayejitaabisha kuwatafuta kondoo walioko pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Vijana nchini Madagascar wanaunda asilimia 60% ya idadi ya wananchi wote wa Madagascar. Hawa ni vijana waliosheheni furaha, imani na matumaini, wanataka kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi. Lakini pia ni vijana wanaokabiliana na changamoto changamani pamoja na matatizo yanayofumbatwa katika maisha ya: kijamii, kitamaduni, kiakili na kidini.

Lakini pamoja na changamoto zote hizi, vijana wa Madagascar wanataka kusimama kidete kuwasha tena moto wa matumaini unaokita mizizi yake katika imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, akashinda nguvu za giza na mauti. Maaskofu wanasema, daima, waamini walei wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa, hasa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Victoria Ramoamanarivo, mwanamke wa shoka, aliyethubutu kuliongoza Kanisa changa la Madagascar, kipindi cha madhulumu wakati wamisionari walipolazimika kuikimbia Madagascar. Vijana mbali mbali wametoa ushuhuda wao jinsi walivyoguswa matatizo ya wafungwa gerezani, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia kwa upendo, hali ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao.

Vijana walikumbana na changamoto za maisha, lakini hawakukata tamaa, leo hii hata ndugu zao, wanathamini sana huduma wanayoitoa kwa wafunga gerezani. Wanawataka kuwasaidia ili wanapomaliza adhabu yao waweze kuwa ni watu wema zaidi katika jamii. Vijana wamemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko changamoto za ukabila wanazokabiliana nazo nchini Madagascar kutokana na tofauti za kitamaduni, mila na desturi; lakini kwa njia ya uvumilivu na upendo wa kifamilia, wamebahatika kuzivuka na sasa ni sehemu ya amana na utajiri wa wananchi wa Madagascar katika ujumla wao. Vijana wamesema, changamoto nyingine ni majadiliano ya kiekumene yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Tofauti za kiimani zisiwe ni makwazo kwa maisha mafungamano ya kifamilia kama ilivyotokea kwa baadhi yao. Kwa sasa vijana wanataka kujikita katika masomo zaidi ili waweze kuwahudumia ndugu zao katika Kristo kielelezo cha majadiliano ya kiekumene katika huduma ya upendo.

Askofu: Mkesha

 

08 September 2019, 16:01