Tafuta

Vatican News
Kardinali Dèsirè Tsarahazana asema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar ni kielelezo cha uwepo wa unabii, ili kukabiliana na changamoto za maisha katika mwanga wa imani. Kardinali Dèsirè Tsarahazana asema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar ni kielelezo cha uwepo wa unabii, ili kukabiliana na changamoto za maisha katika mwanga wa imani.  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Ushuhuda wa kinabii!

Kardinali Dèsirè Tsarahazana asema mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, unapata mwelekeo wa pekee kwa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar. Familia ya Mungu inasubiri kwa hamu kubwa kusikia ujumbe wa kinabii kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko; ili kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anawakumbusha wananchi wa Madagascar kwamba, nchi yao ni maarufu sana kwa uzuri wa mazingira asilia, kiasi hata cha kuwahamasisha watu wengi kuimba utenzi wa sifa na shukrani kwa kusema, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako”. Ni wajibu wa binadamu kuhakikisha kwamba, analinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Pamoja na uzuri wa mazingira asilia, lakini kuna uzuri wa pekee ambao umegota katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ambao ni uzuri wa utakatifu wa maisha yao.

Kardinali Dèsirè Tsarahazana, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Toamasina, nchini Madagascar anasema, ni furaha isiyokuwa na kifani watu wa Mungu kumpokea na kumkarimu Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea nchini mwao; moja ya nchi maskini sana duniani, lakini umesheheni utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu. Madagascar imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa madini, misitu asilia na imezungukwa na Bahari ya Hindi. Lakini, utajiri mkubwa kuliko vyote ni rasilimali watu! Kanisa Katoliki nchini Madagascar liko mstari wa mbele katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Kanisa linaendelea kuhamasisha utakatifu wa watoto wake kwa njia ya ushuhuda makini wa waamini walei pamoja na umati mkubwa wa Makatekista wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kurithisha imani pamoja na kuwaandaa vijana wa kizazi kipya katika maisha kwa njia ya elimu makini na utume kwa vijana! Kanisa nchini Madagascar linaheshimiwa na kuthaminiwa na wengi kutokana na mchango wake katika maisha ya watu: kiroho na kimwili; kwa kuendelea kusimama kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Pamoja na utajiri wote huu, bado familia ya Mungu nchini Madagascar inakabiliwa na changamoto ya umaskini mkubwa wa watu wake; ulinzi na usalama wa watu na mali zao; rushwa na ufisadi pamoja na ukosefu wa haki jamii.

Kanisa nchini Madagascar linawahamasisha waamini walei kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu na nuru ya maisha yao ya kiimani, kimaadili na kiutu. Kwa maneno mengine, waamini wanatakiwa kutangaza na kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika matendo. Mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, unapata mwelekeo wa pekee kwa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar. Familia ya Mungu inasubiri kwa hamu kubwa kusikia ujumbe wa kinabii kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko; ili kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa litaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa.

Viongozi wa Serikali na jamii katika ujumla wake, anasema Kardinali Dèsirè Tsarahazana, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Toamasina kwamba, wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Uongozi ni huduma kwa watu wa Mungu na wala si kichaka cha kuchumia mali na utajiri wa haraka haraka.

Papa: Madagascar: Utakatifu

 

04 September 2019, 15:53