Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwahudumia ndugu zao kwa imani na upendo ili kuondokana kishawishi cha Eutanasia! Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwahudumia ndugu zao kwa imani na upendo ili kuondokana kishawishi cha Eutanasia!  

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Kuhusu kifo laini! Eutanasia!

Kishawishi kinachomnyemelea mwanadamu ni kufikiri kwamba anayo haki na uhuru wa kukatisha maisha yake. Kardinali Gualtiero Bassetti amekazia kuwa hiyo siyo maana ya uhuru inayokusudiwa. Kuangamisha maisha ya mtu kwa njia yeyote ile aidha kwa lengo la kumsaidia mgonjwa asiendelee kuteseka ni fikra zinazojikita katika ubinafsi na mtazamo wa kuona maisha ni mzigo. Injili ya uhai!

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Jopo la vyama vya wataalam wa afya na tiba ya akili nchini Italia, hivi karibuni, walikutana kujadili suala la “eutanasia” yaani kifo laini. Mjadala huo mzito uliongozwa na kauli mbiu ya “familia na maisha” ambayo imejadiliwa na wajumbe kutoka vyama mbalimbali vya watalam wa afya na tiba, vyama vya kijamii na wanaharakati wanaoshughulika na sayansi na maisha. Mwendelezo wa mada hiyo iliyoanzishwa na mahakama ya Milano mnamo tarehe 14 Februari 2018 juu ya uhalali wa kifungu cha Katiba ya Italia namba 580 inayotoa adhabu juu ya mtu anayesaidia au kusababisha mtu mwingine kujiua. Mkutano huo umelenga kutoa mwafaka wa hoja zitakazotolewa katika mkutano wa tarehe 24 Septemba 2019 utakaohusisha pia wabunge kutoka nchini Italia.  Katika upembuzi wa mada hiyo, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, amesema, mwanadamu analazimika kuishi kama alama ya shukrani ya hali ya juu ya zawadi ya maisha anayoipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa maana hiyo, anapaswa kuipokea zawadi hii na kuitunza kwa mapendo makubwa.

Kishawishi kinachomnyemelea mwanadamu ni kufikiri kwamba, anayo haki na uhuru wa kukatisha maisha yake kwa kutafuta njia laini ya kujiua. Kardinali amekazia kuwa hiyo siyo maana ya uhuru inayokusudiwa. Kuangamiza maisha ya mtu kwa njia yeyote ile aidha kwa lengo la kumsaidia mgonjwa asiendelee kuteseka ni fikra zinazojikita katika ubinafsi na mtazamo wa kuona maisha ni mzigo. Hali hii hujitokeza mara kwa mara pale wanaomhudumia mgonjwa wanapochoka na kuhisi kuwa mgonjwa anakuwa mzigo katika familia yao hapo ndipo mawazo ya kutaka kumuua hutokeza kwa kisingizio cha kutaka kukatisha mateso yake. Akifafanua mada hiyo Kardinali Bassetti amekazia kuwa, watu wanapaswa kukishinda kishawishi hicho na badala yake watoe huduma stahiki ya kirafiki na yenye alama ya kujaliana.  Fumbo la mateso ni tendo la huruma ambapo mgonjwa anapaswa kulipokea kwa imani, matumaini na mapendo. Na kwa wanaomuhudumia wanapata fursa ya kuonesha upendo wao wa dhati kwa mgonjwa.

Akiendelea kuelezea, Kardinali Bassetti amesema ni jambo la ubinafsi kwa mgonjwa kukata tamaa na kujiua au kwa wanaomhudumia kumtakia kifo kwa sababu kila mmoja wetu ana kitu cha kuchangia katika jamii. Hivyo haki ya kujiua inapaswa kupingwa kwa nguvu zote, na kuhamasisha ulazima wa kuishi hata kwa wagonjwa kwa sababu katika kuishi kwa kuhudumiana, tunapata faraja na kujenga urafiki, tunashirikishana na kutiana moyo katika magumu, na wakati wote tunadaiwa kuonesha upendo zaidi kwa wahitaji. Mantiki ya kufikiri kuwa wengine hawana umuhimu tena katika jamii ni kumkosea haki Mwenyezi Mungu ambaye anahusika na uamuzi wa mwisho wa maisha ya mtu una pia kumkosea haki mhusika mwenyewe. Kipeo hiki cha kisheria kiliibuka katika historia ya taasisi za afya na kinaendelea hadi sasa kama swali linalodai haki ya mtu. Katika ngazi ya Bunge, mswada huu ulishajadiliwa na kuwekwa katika katiba ya nchi ya Italia ambayo inapaswa kujadiliwa upya na kufanyiwa marekebisho.

Aidha mabadiliko ya sheria hiyo yanapaswa kuwafikia walengwa katika ngazi ya familia inayopambana na uhalisia wa suala hilo. Katika kushirikisha uzoefu wake Kardinali Bassetti amesema, sehemu nyingi zenye malalamiko ya kutaka kudai haki ya kujiua yanatoka katika nchi ambazo zimesharuhusu utamaduni huo wa kifo. Haki ya kujiua inasigana na haki msingi za binadamu na inajificha katika madai ya haki ya kuwa huru lakini huo siyo uhuru wa kweli! kifo laini kinaweza kujitokeza katika mifumo mbalimbali ya maisha, iwe katika uchaguzi wa mazingira, nyenzo na vigezo vya kujiua. Kanisa kwa upande wake linaendelea kutoa ushuhuda wa kiinjili juu ya heshima yaki ya kila mtu na hasa anapokuwa katika mateso na mahangaiko. Hivyo Kanisa daima litaendelea kusimamia kidete haki za waliodhaifu na wanyonge zinazosiginwa katika dai la uhuru binafsi unaokumbatia utamaduni wa kifo. Kanisa daima litabaki aminifu katika kutetea thamani ya utu na ulazima wa kuishi.

CEI: Eutanasia

 

15 September 2019, 11:29