Tafuta

Vatican News
Wosia wa Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko  “Laudato si” unatuasa kuvisikiliza vilio pacha vya Maskini na ulimwengu.Ni lazima kuheshimu mazingira nyumba yetu ya pamoja Wosia wa Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” unatuasa kuvisikiliza vilio pacha vya Maskini na ulimwengu.Ni lazima kuheshimu mazingira nyumba yetu ya pamoja 

AMECEA-Upangaji wa mikakati ya pamoja Uganda na Kenya!

Tarehe 28 hadi 29 Agosti 2019,umefanyika mkutano wa upangaji mikakati pamoja na wadau wake kutoka nchi za Kenya na Uganda uliondaliwa na Shirika Katoliki linalojihusisha na maendeleo ya nchi za nje(CAFOD)katika nchi za Afrika Mashariki.Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Kituo cha JJ McCarthy,Nairobi,Kenya.Mpango mkakati ni dira katika mipango ya wakati ujao katika kuenzi matakwa ya Wosia wa Laudato Si.

Na Padre Angelo Shikombe- Vatican News

Shirika Katoliki linalojihusisha na maendeleo ya nchi za nje (CAFOD) katika nchi za  Afrika Mashariki, kuanzia tarehe 28 had 29 Agosti 2019, limefanya mkutano wa upangaji mikakati pamoja na wadau wake kutoka nchi za Kenya na Uganda. Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi  wa Kituo cha JJ McCarthy, Nairobi, Kenya ukihudhuriwa na wajumbe wa CAFOD, washiriki kutoka majimbo sita na vyuo vikuu vitano vilivyoko nchini Kenya na washiriki wengine kutoka majimbo Makuu matatu katoliki ya (Gulu, Moroto na Kotido) na wengine kutoka katika ofisi za kitaifa za Haki na Amani Nchini Uganda.

Bi Ogolla:Wosia wa Laudato si unashauri kusikiliza vilio vya maskini

Naye Bi Catherine Ogolla,Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki (CAFOD), katika mkutano huo ametoa taarifa juu ya lengo la mkutano huo wa kupanga kwa pamoja kwa ajili ya wakati ujao kama hamasa ya upangaji mkakati kwa nchi ya Kenya na Uganda. Mipango-Mkakati huo (CAFOD) ambao umelenga kiulimwengu kutekeleza lengo la “Nyumba yetu ya  Pamoja” kama inavyohuishwa na Wosia wa Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko  wa “Laudato si” ambao  unatuasa kuvisikiliza vilio pacha vya Maskini na ulimwengu! Aidha, Bi Ogolla anaendelea kusema, “Tunajikita zaidi katika mahitaji msingi yanayoelezwa na Wosia wa Papa, wa  “Laudato Si” ambao inajihusisha zaidi na majanga mawili yaani, la kijamii na la kimazingira linafafanuliwa kwa ukamilifu”. Vile vile anakazia kuwa, CAFOD imekuwa ikifanya kazi katika ushirikiano na wadau wake katika mazingira ambapo ofisi ya Kanda jijini Nairobi hazifiki. Na hivyo, imekuwa ikijenga na kuwaimarishia uwezo wadau wake wanaofanya kazi kwa ngazi za chini.

Kazi nyingine ni pamoja na uhifadhi wa chakula cha kutosha

Bi.Catherine Ogolla katika hoja yake anaendelea kusisitiza kuwa, kazi wanazolenga kuzitekeleza ni pamoka na kuwa na hifadhi ya chakula cha kutosha, uongozi na ushauri ikijumuisha kuimarisha amani na kutafuta suluhu ya migogoro. Kadhalika amesema,“Tunatekeleza miradi inayohusiana na majanga ya watu, na tahadhari katika nchi za Kenya na Uganda. Kwa mfano hali za wakimbizi katika nchi ya Uganda na ukame katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya”. Akiwahakikishia, Bi Catherine Ogolla, amesema CAFOD inashikamana na wadau wake wa muda mrefu ili kupambana pamoja wakisaidiana katika kazi zao. Hata hivyo, amekiri kuwa mazingira yamekuwa yakibadilika kwa kasi kubwa kwa upande wa kifedha. Mfano Kenya kwa sasa inahesabika katika Uchumi wa kati katika Standard za kimataifa ikiongeza  changamoto kubwa katika utunishaji wa mfuko.

Sr. Thabitha Nyawira Mpango wa nyumba ya pamoja ni chanzo kikuu

Kwa upande mwingine hata Sr, Tabitha Nyawira, ASN, Afisa Mipango wa AMECEA, katika kitengo cha Maendeleo ya Utumishi, anasema, “Mpango wetu wa Nyumba yetu ya pamoja ni chanzo kingine kikuu cha uhuisho kinachoendeshwa na AMECEA katika kitengo cha Maendeleo ya Utumishi, kinachopambana na changamoto zinazohusiana na mazingira na zinazowalenga wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.Kutokana na hilo, Sr. Tabitha amesisitiza kuwa,“Mpango mkakati ni dira katika Idara kwa mipango ya wakati ujao katika kuenzi matakwa ya Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko wa  Laudato Si”.

Katibu wa Kamati ya Haki na Amani, Baraza la maaskofu Katoliki Uganda

Katika kuchangia hoja, naye Dk. Emmanuel Kiiza Aliba, Katibu Mkuu wa Kitaifa wa Kamati ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda ambaye kwa muda mrefu amekuwa mdau wa CAFOD ameeleza kuwa “jambo la pekee ni kuwa, CAFOD inatoa mpango mkakati unaoufungua mahusiano na ushiriki katika hadhi yake. Akikazia zaidi amesema “Tunapanga kwa ajili ya miaka mitano ijayo tukitoka katika malengo ya wakati uliopita na kujidhatiti katika Nyumba ya Pamoja, Mpango Mkakati unaolenga kulinda shughuli zetu za miaka mingine mitano. Hivyo tuko hapa kupanga ili tuweze kwenda pamoja katika mpango wa Nyumba yetu ya pamoja”.

03 September 2019, 12:51