Tafuta

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika maadhimisho ya Siku ya Utunzaji Bora wa Mazingira, tarehe 1 Septemba: Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya vinasaba vya imani ya Kanisa. Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika maadhimisho ya Siku ya Utunzaji Bora wa Mazingira, tarehe 1 Septemba: Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya vinasaba vya imani ya Kanisa. 

Ujumbe Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira 1 Septemba 2019: Taalimungu ya Kiekolojia

Mazingira ni kazi ya uumbaji ambayo ina umuhimu wa pekee katika Liturujia Takatifu, hususan katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha muhtasari wa utimilifu wa nyakati. Hii ndiyo karamu kuu inayodhihirisha utimilifu wa utukufu wa Ufalme wa Mungu anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira. Ekolojia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya imani kwa Wakristo inayofumbatwa katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu. Maisha na utume wa Kanisa unamwilishwa katika matukio mbali mbali yanayogusa na kumwambata mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Taalimungu ya kiekolojia inagusa pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kujizatiti katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kutokana na uchafuzi wa mazingira ambao unaendelea kusababisha athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mambo msingi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo imepewa nafasi ya pekee katika Liturujia Takatifu, hususan katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha muhtasari wa utimilifu wa nyakati. Hii ndiyo karamu kuu inayodhihirisha utimilifu wa utukufu wa Ufalme wa Mungu.

Hiki ndicho kiini cha ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote, inayoadhimishwa na Kanisa la Kiorthodox, likiungana na Kanisa Katoliki kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 1 Septemba 2019. Imegota miaka 30 tangu maadhimisho haya yalipoanzishwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kunako mwaka 1989. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira, maadhimisho haya yakaendelezwa hadi kufikia kilele chake tarehe 4 Oktoba, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Matukio yote kuhusu utunzaji bora wa mazingira katika kipindi hiki chote, yanapania kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiekolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu na heshima ya binadamu pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kwa njia ya kazi tendaji ya Roho Mtakatifu, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanaweza kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuelewa matatizo, changamoto na umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Machapisho mbali mbali yaliyowahi kutolewa na Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika kipindi hiki cha miaka thelathini ni utajiri na amana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo kwa sasa ni kati ya majanga makubwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Hii inatokana na dhambi ambayo imempelekea mwanadamu kubeza tunu msingi za maisha ya mwanadamu, hali ambayo kwa sasa inahitaji toba na wongofu wa kiekolojia. Umefika wakati wa kujifunga kibwebwe kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kusimama kidete ili kudumisha haki jamii; mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana.  

Mchakato wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza tangu mwaka 1989 wa kusimama kidete katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ulipania pamoja na mambo mengine kuweka msingi thabiti ili kuweza kutangaza na kushuhudia: sheria, kanuni na taratibu za Kanisa katika kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji inayofumbatwa katika taalimungu ya ekolojia, sehemu muhimu sana ya imani kwa Wakristo. Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, ekolojia hii inamwilishwa katika maisha na vipaumbele vya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Kimsingi, utunzaji bora wa mazingira ni mwendelezo wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na uhusiano wake na ulimwengu. Kumbe, Liturujia ya Kanisa, Sheria, Kanuni na Taratibu zake sanjari na huduma za shughuli za kichungaji ni sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, Fumbo la ukombozi linalogusa maisha ya viumbe hai.

Ni katika muktadha huu, waamini wanakuwa kweli wadau wakuu wa utunzaji wa kazi ya uumbaji; wanashiriki ile dhamana ya kulinda na kuombea mazingira nyumba ya wote. Uelewa makini na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, yawasaidie waamini  kujenga uhusiano mwema na mazingira nyumba ya wote. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakiri kwamba, ulimwengu mamboleo umegeuka kuwa kama kijiji. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utandawazi wa umoja na mshikamano wa dhati, ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazojitokeza kwa ajili ya kulinda, kudumisha na kuendeleza ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Watu wanapaswa kutambua athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ambazo kamwe hazipaswi kufanyiwa mzaha. Tabia ya baadhi ya watu kutaka kufumbia macho changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi ni hatari sana kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni faida kubwa hata kama ni kwa hasara kwa utu na heshima ya binadamu. Uchumi unapaswa kuongozwa na kanuni maadili, utu, mahitaji msingi ya binadamu; mshikamano unaosimikwa katika kanuni auni pamoja na haki. Haya ni mambo msingi na ni sehemu muhimu sana ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Waamini wajifunge kibwebwe katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Vijana waelimishwe kanuni, sheria na taratibu za utunzaji bora wa mazingira, kwa kukazia pia umoja na mshikamano, sehemu muhimu sana ya malezi na majiundo yao. Utamaduni wa ekolojia ya mazingira ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira nyumba ya wote!

Siku ya Mazingira 2019
30 August 2019, 14:47