Tafuta

Mkutano Mkuu wa Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa UISG 2019: Kauli mbiu "Watawa ni wapandaji wa matumaini ya kinabii" Mkutano Mkuu wa Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa UISG 2019: Kauli mbiu "Watawa ni wapandaji wa matumaini ya kinabii" 

UISG: Watawa ni wapandaji wa matumaini ya kinabii! Kwa maisha na utume wao!

Sr. Carmen Sammut, MSOLA, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa aliwahimiza kutafakari kuhusu namna ambayo wanawake waliowekwa wakfu wanaweza kuwa ni wajenzi wa matumaini mapya “katika ulimwengu uliogawanyika na wenye vita” na “kwa wanawake wengi na watoto wanaoteseka na kudhalilishwa utu na heshima yao kama binadamu”.

Na Sr. Nadia Coppa, ASC, - Roma.

Watawa ni wapandaji wa matumaini ya kinabii. Hii ndiyo iliyokuwa kauli mbiu iliyoongoza mkutano mkuu wa XXI wa Mama wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ambao ulifanyika mjini Roma kuanzia tarehe 6 hadi 10 Mei 2019. Sr. Carmen Sammut, MSOLA, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa aliwahimiza kutafakari kuhusu namna ambayo wanawake waliowekwa wakfu wanaweza kuwa ni wajenzi wa matumaini mapya “katika ulimwengu uliogawanyika na wenye vita” na “kwa wanawake wengi na watoto wanaoteseka na kudhalilishwa utu na heshima yao kama binadamu”. Ulikuwa ni upendeleo wa pekee anasema Sr. Nadia Coppa, Mama Mkuu wa Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, kuweza kuishi mang’amuzi hayo ya nguvu ya mwingiliano wa tamaduni na wa mashirika mbali mbali ya kitawa.

Kulikuwa na jumla ya Mama wakuu 850 wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka katika  nchi 80 duniani. Kwa moyo wa unyenyekevu, ukweli na uwazi wa moyo walitafuta namna ya kujibu pamoja maombi mbalimbali ambayo yanagusa maisha ya wakfu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia uliojeruhiwa kutokana na ubinafsi na hali ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine. Kwa kweli ilikuwa ni nafasi ya kushirikishana na kutajirisha mang’amuzi na maisha, changamoto na matamanio halali katika maisha ya watu. Sr. Nadia Coppa anasema, jambo hili lililiwa ni baraka kwa maisha yake na kwa huduma anayoitoa kama Mama mkuu wa Shirika. Mama wakuu walijikuta wakiwa wamoja kwenye meza ya kumega Neno la Mungu, kwa kuangalia hali halisi ya ulimwengu na kuwa na ndoto pamoja na ndugu zake ambao kwa hakika ni walinzi wa mbegu ya tumaini na wenye uwezo wa kuangalia ya mbeleni kwa matumaini zaidi.

Fursa hii imepyaisha ndani wake, ile furaha na shahuku ya kutaka kutafuta majibu mapya ya changamoto nyingi ambazo zinaendelea kujitokeza kila kukicha katika ulimwengu mamboleo!  Tafakari nyingi zilizotolewa zilikuwa kweli utajiri na zimeimarisha ndani mwao siyo tu uzuri wa maisha ya wakfu, bali pia wajibu wake msingi katika maisha na utume wa Kanisa na ya ulimwengu: kwamba, watawa wanapaswa kuwa ni ishara ya matumaini ya kinabii ambayo yanabubujika kutoka ndani kabisa mwa maisha ya kitawa ambayo yanawasukuma kuwaendea watu wote bila ubaguzi, zaidi sana wale walio maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwingiliano wa tamaduni katika ulimwengu wa utandawazi;  Dira na mwelekeo wa wakati ujao wa maisha ya kitawa;  muunganiko na mkamilishano wa viumbe hai kupitia Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si”, na majadiliano ya kidini na kiekumene zilikuwa ni mada zilizoendelezwa kupitia usikivu wa nguvu na wa kina, mang’amuzi na ushirikishaji wa tafakari.

Tumaini lilikuwa njia muafaka iliyosindikiza tafiti zao na kuwafanya kuona kwa pamoja upeo unaowezekana wanapofanya hija ya pamoja, kwa kutenda na kushirikishana. Zilikuwa ni siku ambazo ziliwasha ndani ya kila mmoja wao tumaini katika mtazamo wa Mungu kwa ajili ya wakati ujao; walifurahi kutambua kwamba, licha ya udhaifu ambao unagusa maisha katika ngazi zote, kama watawa wameitwa kumfuata Kristo Yesu na kuwa Sakramenti ya uwepo endelevu wa Mungu ulimwenguni. Tumaini ni zawadi ya umoja ambayo wanataka kuendelea kuijenga kupitia mahusiano ya kiimani na maagano yaliyofanywa katika upendo na wema wa kiutu unaobadilika kila siku na kupyaishwa ili uweze kung’ara zaidi. Mbegu ndogo, matendo madogo ya huruma:kiroho na kimwili ni njia ndogo zinazowezekana kumwilisha unabii na tumaini katika maisha ya watu. Ikumbukwe kwamba, huruma inajenga matumaini katika siku zijazo zilizoahidiwa na Mungu.

Matendo yao  madogo madogo ya huruma hutoa dira ya uumbaji kwa kila mtu moja moja kama unabii kwa sababu ya imani! Watawa wanaitwa na kutumwa kujenga na kuimarisha mshikamano kwa kuwaelekea wale ambao wanaishi pembezoni mwa jamii, kwa kuwa hili ni eneo la wito wa kinabii wa wale wote waliowekwa wakfu. Wanapaswa kuwa ni watu wa uponyaji katika mahusiano ya watu yaliyosambaratishwa ulimwenguni kutokana na uchoyo na ubinafsi. Kwa hiyo,  ili kuwa waaminifu katika wito wao wa kinabii, wanaweza kuwa wapandaji wa tumaini la kinabii kwa ajili ya ulimwengu ikiwa kama tu wameimarika na kuzama katika Neno la Mungu, wakilitafakari kama alivyofanya Yesu. Pamoja na Kristo Yesu aliyekuwa: maskini, mseja na mtii; wito wao wa kinabii unawataka kubaki pembezoni mwa jamii ili kutoa ushuhuda kwa kupambana na  utamaduni wa kutumia mabavu ambao unaipeleka dunia kwenye uharibifu, majanga na maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kutoka katika mang’amuzi haya, ziliibuka hamu na maamuzi mengi dhahiri ambayo watawa wanapenda kuyafanyia kazi ili kukifanya kiaminike kile ambacho wao wanakiamini na kukitolea ushuhuda. Mwishoni mwa mkutano Mama wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, anasema  Sr. Nadia Coppa, walipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.  Ulikuwa muda wa nguvu ambapo walijiachilia na kujiaminisha mikononi mwa Baba Mtakatifu ili waguswe na maneno yake ya unyenyekevu na ya kutia moyo ambayo yanawahimiza kusikiliza kilio cha maskini na kukijibu kwa njia ya huduma ya Kanisa na ulimwengu katika uaminifu wa utambulisho wa karama mbali mbali za watawa zinazowafanya kuwa kweli ni moto wa kuotea mbali katika maisha na utume wa Kanisa.

Sr. Nadia Coppa
14 August 2019, 14:33