Tafuta

Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO: Mikakati 2018-2022: Mazingira, Familia, Utume na Utakatifu wa maisha. Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO: Mikakati 2018-2022: Mazingira, Familia, Utume na Utakatifu wa maisha. 

Wanawake Wakatoliki Duniani: Malengo 2018-2022: Mazingira, Familia, Utakatifu & Utume

WUCWO, UMOFC, katika mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 15-22 Oktoba 2018, uliazimia kutekeleza mambo makuu manne katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2022. Utunzaji bora wa mazingira; Tunu msingi za maisha ya kifamilia; Umuhimu wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na Utume wa wanawake Wakatoliki, ndani ya Kanisa & Jamii.

Na Evaline Malisa Ntenga, - Roma.

Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, katika mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 15-22 Oktoba 2018, uliazimia kutekeleza mambo makuu manne katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2022. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kadiri ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kujali na kuzisaidia familia zinazoishi katika mazingira na hatarishi, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu! Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujifunga kibwebwe ili kutokomeza ubaguzi, nyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wanawake majumbani kwa kuwa na maandalizi bora kwa wanandoa watarajiwa, ili kukuza na kushirikishana upendo wa dhati, ili kuwaimarisha wanandoa na hatimaye, waweze kutakatifuzana. Wanawake Wakatoliki wanahimizwa kujielimisha zaidi ili hatimaye, waweze kutikia wito wa utakatifu wa maisha!

Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani limechota utajiri wa maazimio haya kutoka katika Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Pili ni Wosia wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia. Tatu ni Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ambao ni dira na mwelekeo wa maisha na shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha! Nne ni Waraka wake wa kitume wa Papa Francisko “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”.

Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Siku ya X ya Mkutano wa Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma, nchini Italia, kuanzia tarehe 23-27 Juni 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Kumbe, maazimio ya Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani yana kazia kwa namna ya pekee: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na utakatifu wa watu wa Mungu, unaowasukuma waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani! Wanawake Wakatoliki wanawajibika kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Ikumbukwe kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wanawake Wakatoliki ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika ngazi mbali mbali.

Wanawake ndio wenye jukumu la kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Kumbe, wanawajibika pia kutunza vyanzo vya maji kwa kutambua kwamba, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Ikiwa kama kutakuwepo na utunzaji bora wa vyanzo maji, basi, wanawake watakuwa wamechangia pia kuzima kiu ya amani duniani! Jamii inapaswa kutumia vyema rasilimali, utajiri na maliasili za dunia hii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuondokana na uchafuzi wa mazingira, ubinafsi na uchoyo. Wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na utupaji taka za plastiki ambazo zimekuwa ni tishio kubwa kwa usalama na maisha ya viumbe hai. Hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto ambayo inaweza kushughulikiwa kwa njia ya wongofu wa kiekolojia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. 

Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini. Anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo yanategemeana na kukamilishana! Wanawake wawe mstari wa mbele katika kupambana na wale wanatupa ovyo taka za sumu kwani athari zake ni kubwa katika jamii! Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kujali na kuzisaidia familia zinazoishi katika mazingira na hatarishi, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu! Mwelekeo wa pekee ni kwa ajili ya wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Huu ni mchakato wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wanawake Wakatoliki wawe mstari wa mbele katika malezi na makuzi ya watoto wao na kamwe wasikubali wakumbwe na mawimbi mazito ya ukoloni wa kiitikadi; sera za utoaji wa mimba na kifo laini.

Uhai, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Familia zinahamasishwa kuwa na matumizi bora na sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima ya wanafamilia. Uhalifu kwenye mitandao ya kijamii inazidi kukua na kuongezeka kila kukicha na matokeo yake ni biashara ya picha za ngono pamoja na nyanyaso za kijinsia. Dhamana na majukumu ya wazazi na walezi kwa watoto na vijana wa kizazi kipya ni kati ya mambo yaliyopewa kipaumbele kwenye familia. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika Barua binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia;  anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara.

Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO limeridhia Sheria hizi. Mambo msingi hapa ni kuhusu: Upendo na ulinzi wa watoto ndani ya familia; Umuhimu wa kuzingatia Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na mchakato wa kuwaundia watoto mazingira mazuri ya malezi makuzi yao. Wanawake watambue maeneo korofi yanayoweza kuhatarisha utu, heshima na utakatifu wao. Wazazi ni walimu na makatekista wa kwanza katika mchakato mzima wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ni dira na mwelekeo wa maisha na shughuli za kichungaji katika ulimwengu mamboleo. Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani linawataka wanawake kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki zao msingi, ili kukuza na kudumisha upendo na uaminifu katika maisha ya ndoa na familia.

Utenzi wa upendo wa kweli kutoka kwa Mtakatifu Paulo uwe ni dira na mwongozo makini kwa wanandoa. Kuna haja ya kuendelea kudumisha malezi na majiundo ya watu wa ndoa na familia. Watu waendelee kuheshimiana na kuthaminiana kwa kutambua kwamba, wote wanategemeana na kukamilishana katika maisha na wito wao. Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani liendelee kushirikiana na kushikamaana na taasisi, viongozi pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kutambua na kuwasaidia wanawake wanaoathirika kutokana na vipigo vya majumbani na nyanyaso kutoka katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12)  anapenda kukazia zaidi: udumifu, uvumilivu na unyenyekevu wa moyo kama alama za utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo dhidi ya tabia matumizi ya nguvu, ubinafsi na uchoyo pamoja na hali ya mtu kujiridhisha binafsi katika ufahari wake.

Wakristo wawe wanyenyekevu kwa kujikita katika ukweli na uwazi; utu wema pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya ulimi! Waamini wafurahie pia mafanikio ya jirani zao, wawasahihishe kwa upole na udugu pale wanapolegea katika dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa na huu ni ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo. Kuna waamini wanaoendelea kusimamia haki, amani na maridhiano katika jamii kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Hawa wanahesabika kuwa ni vyombo vya amani! Maisha ya Kikristo ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, furaha ya kweli inafumbatwa katika upendo! Wakristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na utulivu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha umoja na upendo wa kidugu. Waamini waoneshe uhuru na upendo wa ndani kabisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya upya wa maisha yao!

Familia ya Mungu ioneshe ujasiri wa kutoka kifua mbele kama ilivyokuwa kwa watakatifu wa nyakati mbali mbali ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani linawahimiza wanawake pamoja na familia ya Mungu katika ujumla wake, kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Hii ni safari ya maisha ya mwamini, inayomtaka kutimiza dhamana na wajibu wake kama impasavyo mwana wa Mungu. Wanawake waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha. Haya ni mambo yanayopaswa kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha pamoja na kutimiza wajibu. Wanawake washiriki katika shughuli mbali mbali za uongozi. Utakatifu wa maisha ni mwaliko na wito wa kila mwamini!

Wanawake: WUCWO
17 August 2019, 15:59