Vatican News
CELAM inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kusaidia kuzima moto unaoendelea kuteketeza msitu wa Ukanda wa Amazonia. CELAM inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kusaidia kuzima moto unaoendelea kuteketeza msitu wa Ukanda wa Amazonia. 

CELAM: Msitu wa Amazonia unateketea kwa moto! Athari kubwa sana duniani!

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, linapenda kuunganisha sauti yake, ili kulilia mshikamano wa dhati na wanannchi wa Amazonia, ili kwa pamoja waweze kushirikiana na kushikamana kuuzima moto huo. Mwaliko wa pekee kabisa unatolewa kwa viongozi wakuu wa Brazil, Bolivia, Marekani pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa. HATARI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu, mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 hapa mjini Vatican inaongozwa na kauli mbiu Sinodi ya Amazonia: “Njia mpya ya Kanisa kwa ajili ya ekolojia fungamani”. Kwa wananchi wa Amazonia, ardhi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, eneo takatifu, utambulisho na chemchemi ya tunu msingi za maisha.

Baba Mtakatifu anasema, wananchi wa Ukanda wa Amazonia ni kumbu kumbu endelevu ya utume wa Mungu aliowakabidhi binadamu wote, yaani utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Changamoto changamani zinaendelea kuibuka kila kukicha anasema Baba Mtakatifu Francisko ni sehemu ya maisha ya binadamu. Lakini mchango wa raia hawa ni mkubwa sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi kijacho, changamoto kwa walimwengu kuwa na kiasi katika matumizi ya rasilimali za dunia, hali inayohitaji kuvunjilia mbali mambo yote yanayosababisha ukosefu wa haki, ili kuwajengea watu furaha na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, limesikitishwa sana na moto mkubwa unaoendelea kuteketeza misitu ya Ukanda wa Amazonia, kiasi hata cha kutishia usalama na maisha ya viumbe hai kwenye Ukanda huu na ulimwengu katika ujumla wake. Katika Hati ya Kutendea Kazi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia, “Instrumetum laboris” inabainisha kwamba, maadhimisho ya Sinodi hii yanakita malengo yake katika Injili ya uhai, kwa kutambua kwamba, Ukanda wa Amazonia ni chemchemi ya uhai, changamoto na mwaliko wa kuishi vyema ili kuweza kupata uzima na kisha wawe nao tele!. Hili ndoto hii iweze kutimizwa kuna haja ya kuishi vyema kwa kupambana vyema na mambo yanayotishia maisha. Moto unaoendelea kuwaka kwenye Misitu ya Ukanda wa Amazonia ni tishio kwa maisha na usalama wa viumbe hai.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, linapenda kuunganisha sauti yake, ili kulilia mshikamano wa dhati na wanannchi wa Amazonia, ili kwa pamoja waweze kushirikiana na kushikamana kuuzima moto huo. Mwaliko wa pekee kabisa unatolewa kwa viongozi wakuu wa Brazil, Bolivia, Marekani pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa. Watu wenye nafasi muhimu katika Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wasaidie kusimama kidete kulinda na kutunza misitu ya Ukanda wa Amazonia unaoteketea kwa moto! Kamwe wasiruhusu uharibifu huu wa mazingira nyumba ya wote kuendelea, wala kamwe wasikubali kutaliwa na utamaduni wa kifo.

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres anasema, amesikitishwa sana na janga la moto mkali linaloendelea kuteketeza msitu wa Amazonia ambao ni muhimu sana katika maisha, ustawi na maendeleo ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Ukanda wa Amazonia unalindwa na kuheshimiwa. Juhudi hizi pia zinapaswa kuelekezwa kwenye Misitu ya Congo na ile ya Indonesia. Vyanzo vya habari vinabaini kwamba, moto huu umenzia kwenye mji wa Rondònia na kwa muda wa majuma mawili bado unaendelea kuwaka tu.

CELAM: Moto Amazonia

 

24 August 2019, 13:49