Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 21 ya Mwaka C wa Kanisa: Wokovu ni zawadi ya Mungu inayomwajibisha mwamini. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 21 ya Mwaka C wa Kanisa: Wokovu ni zawadi ya Mungu inayomwajibisha mwamini. 

Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka: Wokovu ni zawadi inayowajibisha!

Wokovu wa Mungu: Ni kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na upyaisho wa maisha na kwa kufuata Njia nyembamba ya Msalaba, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani sanjari na kujikita katika utamadunisho! Uwajibikaji binafsi ni muhimu katika mchakato wa kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, kwa kusali na kukesha!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 21 ya mwaka C wa Kanisa. Watu wote wanaalikwa na kukaribishwa kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Tunakumbushwa kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote. Ili kuweza kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, mwamini hana budi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake pamoja na kuendelea kujinyenyekesha kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka. Ni kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na upyaisho wa maisha na kwa kufuata Njia nyembamba ya Msalaba, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani sanjari na kujikita katika utamadunisho! Uwajibikaji binafsi ni muhimu katika mchakato wa kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, kwa kusali na kukesha daima

Somo la kwanza (Is 66:18b-21 ) ni kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya. Mazingira ya somo hili ni katika kipindi ambacho Waisraeli wamerejea kutoka utumwani Babiloni. Wapo katika mchakato wa kulijenga upya taifa lao na wao wenyewe kujipambanua kama taifa. Katika mchakato huu, waisraeli wanaelekeza zaidi kuwa taifa lililojifungia, taifa ambalo halihitaji mchanganyiko wala mahusiano na mataifa mengine. Mwandishi wa sehemu hii analeta unabii wa Mwenyezi Mungu kwao, unabii unaowakumbusha kuwa wao ni taifa teule, taifa ambalo Mungu amelichagua si kwa manufaa yao peke yao bali kwa njia yao aweze kuyaunganisha kwake mataifa yote ya ulimwengu mzima. Huu ni unabii unaoonesha “ukatoliki” wa mpango wa Mungu kwa watu wake. Ukatoliki ambao wote hupata nafasi machoni pa Mungu. Ndiyo maana Mungu katika somo hili anasema  “wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote nao watakuja na o watauona utukufu wangu…nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote kuwa sadaka kwa Bwana..”.

Somo la pili (Ebr 12:5-7, 11-13) ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania. Somo hili linazungumzia fadhila ya ustahimilivu na uvumilivu kama fadhila muhimu ya kumsaidia mtu kutunza imani wakati wa vipindi vigumu vya maisha. Hata hivyo, vipindi hivyo vigumu vya maisha mwandishi anavilinganisha na maonyo kama yale ambayo mzazi humpatia mwanae. Anasema kwa kawaida mzazi anayempenda mwanae humrudi, humuadhibu pale anapokosea. Na adhabu wakati ule inapotolewa huwa haipendezi lakini mbeleni mtoto huona ndani yake malezi yanayomsaidia maishani. Vivyo hivyo kwa mkristo katika njia ya ushuhuda wa imani, vipindi vigumu anavyovipitia ni vipindi vinavyoimarisha imani. Ni vipindi vinavyohitaji ustahimilivu na uvumilivu ili imani inayokomazwa katika vipindi hivyo ifikie wakati wa kumpa matunda yake.

Injili (Lk 13:22-30) Injili ya dominika ya leo kutoka Mwinjili Luka, inazungumzia mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza ni kuonesha kuwa wokovu sio suala kumbakumba, katika wokovu Mungu anashughulika na nafsi kila moja kwa upekee wake. Tunaona  mtu mmoja anamuuliza Yesu “Je, wanaookolewa ni wachache?”. Yesu hampi idadi kuwa ni wengi au ni wachache kwa sababu hiyo siyo namna ya utendaji wa Mungu. Wanaweza wakaokolewa wengi ila yule anayeuliza asiwemo kati yao. Uwingi wa idadi hautamsaidia. Badala yake Yesu anamwambia namna itakayomsaidia, nayo ni kujitahidi kupita katika mlango mwembamba. Picha hii ya mlango mwembamba na mlango mpana ni kama ile namna ya kufundisha katika hekima ya kiyahudi kwa kutumia picha ya njia mbili – ya weke haki na ya wapotevu, au ile ya mkono wa kulia na wa kushoto. Ni picha inayosisitiza njia ya maisha adilifu dhidi ya yale yasiyo adili.

Jambo lingine kubwa katika Injili ya leo ni ile dhamira ya ukatoliki wa wokovu wa Mungu. Somo hili kwa mara nyingine tena linaonesha kuwa wokovu wa Mungu ni kwa ajili ya wote na uko wazi kwa ajili ya wote. Yesu anasema “watafika watu kutoka mashariki na magharibi, toka kaskazini na kusini nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu”. Wokovu wa Mungu haujishikamishi na kabila, taifa au jamii fulani tu. Kila aliyetayari kuupokea mwaliko wake atakuwa miongoni mwa wana wa ufalme.

Liturujia J21
23 August 2019, 15:33