Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya XX ya Mwaka C wa Kanisa: Mateso ni shule ya utakatifu na mtihani wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya XX ya Mwaka C wa Kanisa: Mateso ni shule ya utakatifu na mtihani wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. 

Tafakari Jumapili 20 ya Mwaka: Mateso ni shule ya utakatifu na imani kwa Kristo na Kanisa

Mama Kanisa anafundisha kwamba, kwa mfuasi wa Kristo Yesu hatakiwi kushika imani tu na kuiishi, bali bado anapaswa aiungame, aishuhudie kwa uhakika, na aineze. Wakristo wanapaswa kuwa tayari kumkiri Kristo Yesu mbele za watu na kuthubutu hata kumfuasa katika Njia ya Msalaba, kati ya madhulumu ambayo ni sehemu ya vinasaba katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 20 ya  Kipindi cha mwaka C wa Kanisa. Mama Kanisa anafundisha kwamba, kwa mfuasi wa Kristo Yesu hatakiwi kushika imani tu na kuiishi, bali bado anapaswa aiungame, aishuhudie kwa uhakika, na aineze. Wakristo wanapaswa kuwa tayari kumkiri Kristo Yesu mbele za watu na kuthubutu hata kumfuasa katika Njia ya Msalaba, kati ya madhulumu ambayo ni sehemu ya vinasaba katika maisha na utume wa Kanisa. Huduma na ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko ni mambo msingi kwa wokovu. Waamini wanakumbushwa kwamba, mateso ni shule ya utakatifu na mtihani wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Somo la kwanza (Yer 38:4-6, 8-10 ) ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Yeremia. Yeremia alifanya utume wake wa unabii katika kipindi kigumu sana. Ni kipindi ambacho wafalme wa Israeli pamoja na viongozi waandamizi hawakuwa na hofu ya Mungu. Kipaumbele chao kilikuwa ni kukuza wigo wa madaraka yao na nguvu zao za kisiasa. Mazingira ya somo la leo ni kwamba Israeli chini ya mfalme Zedekia ipo katika hatari ya kuingia vitani na mfalme wa Babeli. Yeremia aliwaonya Israeli kutoingia vitani na kwamba wakithubutu watashindwa na mji wao utawekwa mateka chini ya jeshi la mfalme wa Babeli. Kwa utabiri wake huo, viongozi wasiopenda amani, waliokuwa wamejielekeza tayari katika vita wanamwambia mfalme kuwa Yeremia “anaidhoofisha mikono ya watu wa vita” na kwa maneno mengine anaisaliti Israeli na wanamwomba mfalme aidhinishe Yeremia kuuwawa. Yeremia anatupwa gerezani. Na gereza alilotupwa ni shimo refu lenye matope ili afie huko.  Akiwa shimoni humo, Mwenyezi Mungu anamtumia Ebed melek, mtumishi wa chini kabisa wa mfalme tena asiye Myahudi kwenda kwa mfalme na kumbadili mawazo na hivi Yeremia anaokolewa. Hili ni somo linalotuonesha namna watu wanavyoweza kuungana katika nia yao mbaya na kumuundia kisa cha kumuangamiza mtu mwema anayeonekana kuwa ni kikwazo cha kutimiza malengo yao.

Somo la pili (Ebr 12:1-4) ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania. Waraka huu baada ya kutoa orodha ya mashujaa wa imani katika somo la dominika iliyopita, somo hili linaendeleza dhamira hiyo ya imani na kutuonesha kuwa Kristo ni mfano kamili wa ushuhuda wa imani. Injili (Lk 12:49-53) Katika Injili ya dominika ya leo, Yesu anatoa kauli ambayo kidogo inatatanisha. Yeye mfalme wa amani na ambaye kuzaliwa kwake kulitangaza utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema, leo anasema hakuja duniani kuleta amani. Anasema “je mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia la sivyo bali mafarakano”. Yesu kwa kauli hiyo anaweka wazi kuwa ufalme wa mbinguni ni ufalme wa amani na mapatanao lakini tangazo la ufalme huo huleta migawanyiko.

Huleta migawanyiko kwa sababu kuupokea ufalme huo ni jambo linalomhitaji mtu kufanya maamuzi magumu, ni jambo linalomhitaji mtu kujitoa kabisa na si wote ambao kwa mara moja huweza kuifikia hatua hiyo. Yeye mwenyewe anasema ana ubatizo apaswao kubatizwa. Anasema hivi akimaanisha uchungu wa mateso ambayo yako mbele yake, mateso ambayo hana budi kuyapitia na hata sasa anatamani yatimizwe. Ni kutoka hapa tunaelewa kwa nini Yesu ansema amekuja kutupa moto duniani. Yohane Mbatizaji alitabiri kuwa ajapo Yesu atabatiza kwa Roho Mtakatifu na moto kama alama ya kutakasa. Yesu analeta leo taswira ya moto akimaanisha hukumu ambayo yeye mwenyewe amekuja kuipitisha na ataipitisha siku ya mwisho mintarafu upande mtu anaouchagua katika kuupokea ufalme wa Mungu.

Liturujia J20
16 August 2019, 17:16