Tafakari Neno la Mungu: Jumapili 19 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Utii wa imani; fadhila ya matumaini na sala kama kesha la unyenyekevu wa moyo! Tafakari Neno la Mungu: Jumapili 19 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Utii wa imani; fadhila ya matumaini na sala kama kesha la unyenyekevu wa moyo! 

Tafakari Jumapili ya 19 ya Mwaka C: Sala kama kesha ya unyenyekevu wa moyo!

Kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu utii wa imani na fadhila ya matumaini. Waamini wanakumbushwa kuwa, wanapokumbana na vizingiti katika maisha ya sala, wanapaswa kukesha kwa moyo wa unyenyekevu, kwani hizi pia zinaweza kuwa ni dalili za ukosefu wa imani, ukavu wa moyo pamoja na uzembe. Mtu mnyenyekevu hashangazwi na taabu zake.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 19 ya mwaka C wa Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu utii wa imani na fadhila ya matumaini. Waamini wanakumbushwa kwamba, wanapokumbana na vizingiti katika maisha ya sala, wanapaswa kukesha kwa moyo wa unyenyekevu, kwani hizi pia zinaweza kuwa ni dalili za ukosefu wa imani, ukavu wa moyo pamoja na uzembe. Mtu mnyenyekevu hashangazwi na taabu zake, bali zinamsaidia kutumaini zaidi na kubaki imara na katika udumifu. Rej. KKK 2729-2733. Abrahamu anawekwa mbele ya waamini kama mfano na kielelezo bora cha imani ya watu wa Mungu.

Somo la kwanza (Hek 18:6-9 ) ni kutoka katika kitabu cha Hekima. Katika sura zilizotangulia somo hili, mwandishi anazungumza juu ya watu wenye haki na watu wasio haki yaani watu wema na watu waovu. Ametetea sana maisha ya uadilifu na haki dhidi ya yale maisha yasiyo adili akionya kuwa maisha yasiyo adili hayamfikishi mtu popote isipokuwa katika uharibifu wake. Katika sura hii ya somo la leo, mwandishi analitafakari tukio la waisraeli kutoka Misri. Anatafakari uadilifu wa waisraeli chini ya kiongozi wao Musa na ukorofi wa wamisri chini ya kiongozi wao Farao. Analiona tukio hilo la ukombozi wa waisraeli akikumbuka hasa usiku ule wa pigo la kumi ambapo wazaliwa wa kwanza wa Wamisri waliuawa. Tukio hilo anaona ni kielelezo kizuri cha kuonesha hatima ya watu wema na ile ya watu waovu. Waisraeli waliokuwa wema machoni pa Mungu hawakuguswa na baa lolote lililowakumba wamisri. Anaonesha kuwa ndivyo itakavyokuwa daima kwa watu wema dhidi ya wale waovu.

Somo la pili (Ebr 11:1-2, 8-19 ) ni kutoka katika waraka kwa Waebrania na linahusu imani. Somo linazungumzia imani kama ile fadhila iliyowatambulisha watu wa Mungu katika historia nzima ya wokovu. Mungu tangu mwanzo alikuwa na makusudi yake kwa ulimwengu na kwa watu wake. Makusudi haya hakuwajulisha moja kwa moja bali aliyafunua pole pole katika namna alivyokuwa akihusiana nao. Wao hawakuyajua waziwazi makusudi ya Mungu bali ni kwa imani walizidi kupiga hatua, ni kwa imani waliyapokea maagizo ya Mungu na hata wakati ambapo hawakuona wala kuelewa chochote walikuwa kama wale wanaojua yote kuhusu kile Mungu atakachowajalia kwa wakati wake. Ndivyo somo linavyowataja mashujaa wa imani: Ibrahimu, wanawe Isaka na Yakobo pamoja na mkewe Sara.

Injili (Lk 12:32-48) Katika injili ya dominika ya leo, mwinjili Luka analeta mafundisho ya Yesu kuhusu kukesha na kujiweka tayari kwa ajili ya ufalme ambao Mungu amewaandalia watu wake. Mafundisho haya ya kukesha na kujiweka tayari anayatoa kupitia mifano mitatu. Mfano wa kwanza ni wa watumishi wanaomgonja bwana wao kutoka arusini ili wamhudumie. Hawajui arusi itaisha saa ngapi na hawajui bwana wao atarudi saa ngapi. Wanapaswa tu wawe tayari. Na Yesu anaonesha bwana wao atakapowakuta wako macho badala ya wao kumhudumia, ni yeye atakayewahudumia. Na hii ni alama ya tuzo kwa ustahimilivu wao.

Mfano wa pili ni mwenye nyumba anayelinda mali zake bila kujua ni wakati gani mwizi atakuja kuivamia nyumba na kuiba mali zake. Anahusisha ujio usiojulikana wa mwizi na ujio usiojulikana wa Mwana wa Adamu. Huu anautoa kama mwaliko wa kujiweka tayari kwa kuwa saa ya kuja Mwana wa Adamu haijulikani. Mfano wa tatu ni wa mtumishi aliyewekwa juu ya watumishi wengine ili awahudumie. Huyu atakapokutwa anatimiza vema utumishi wake atapewa tuzo lakini atakapokutwa, badala ya kuhudumia, yeye anatumia vibaya madaraka yake – anawapiga wajoli wake, anakula na kunywa na kulewa – huyu ataadhibiwa. Na Yesu anatumia lugha kali kusema kuwa atakatwa vipande viwili na kuwekewa fungu lake pamoja na wasioamini. Mifano hii yote ya injili ya leo inatualika tukeshe na kujiweka tayari. Aidha inatuonesha pia kuwa imani yetu tuliyojaliwa inatubidiisha tuishi vizuri zaidi ya wale wasioamini. Kwa imani yetu sisi tumekabidhiwa vingi na hivyo siku ya hukumu tutadaiwa vingi.

Liturujia J19
09 August 2019, 16:17