Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu ni fadhila inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu ni fadhila inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani!  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili 22 ya Mwaka: Unyenyekevu katika huduma kwa maskini: kiroho & Kimwili

Mama Kanisa katika ukarimu wake katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa, anapenda kuwaalika watoto wake pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha fadhila ya unyenyekevu katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; maskini ambao ni amana na utajiri wa Kanisa wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Katika nyakati za Yesu na hata leo hii mlo wa mchana wa Sabato ulijumuisha ndugu, jamaa na marafiki na pia ni fursa muhimu si tu ya kula pamoja bali pia kuendelea kuwa na wasaa wa kujadili juu ya Neno la Mungu walilolisikia katika Sinagogi na hata pia walijadili mambo mbali mbali kama vile ya kijamii, kisiasa na hata masuala ya kifamilia. Ilikuwa ni fursa adhimu kabisa pale ambapo kati yao alikuwepo Rabi kuweza kujadili haswa maswali ya kidini, kiteolojia na hata kimaadili. Hivyo mafarisayo, waandishi na viongozi wa kidini walitumia fursa hizo kuweza kuwafundisha zaidi masuala ya kiimani wanapokuwa mezani. Na hata Yesu mara kadhaa alitumia fursa hizo za kuwa mezani kuweza kutoa mafundisho yake. Na mezani pia si tu walikaa bila mpangilio bali kulikuwa na sheria na taratibu zake za kuketi, hivyo mwenyeji aliketi katikati au sehemu ambayo angeweza kuhudumiwa kirahisi na kwa nafasi ya kwanza na pembeni yake waliketi wageni waalikwa mashuhuri na wengine waliketi pia kwa kadiri ya nyadhifa zao kadiri ya nyadhifa zao iwe ni kidini au kidini na hata kiumri.

Ni katika muktadha huo wa kuketi mezani kadiri ya wadhifa wa kila mwalikwa ndio Yesu anatumia fursa hii kutupa mafundisho yake katika Dominika ya leo. Mwinjili Luka hazungumzii juu ya jinsi ya kuketi tunapoalikwa kwenye masherehe au mezani bali anatumia wasaa huu kuiasa jumuiya ya wakristo aliyokuwa anawaandikia na hata jumuiya zetu leo. Ni Injili inayogusa jumuiya nzima ya Kikristo yaani Kanisa na hivyo tusiishie tu katika muktadha ule wa mlo alioalikwa Yesu kwenye nyumba ya mkuu wa mafarisayo. Yesu Kristo daima anawaonya wafuasi wake kutokujikweza au kujichukulia nafasi za heshima na hivyo Injili ya leo haina lengo la kututaka tuchukue nafasi za mwisho ili tukwezwe na kupewa nafasi za heshima, ila lengo lake ni kutualika kubadili mtazamo wetu kama wakristo. Ni kuwa na mtazamo mpya wa kuwa watumishi katika jumuiya zetu kama vile Yesu Kristo mwenyewe alivyokuwa mtumishi wetu.

Yesu leo pamoja na kwamba ni mualikwa lakini haongei kama mualikwa bali kama mualika na hapo ndio tunaweza kupata ujumbe kusudiwa wa Injili ya leo. Ni Yesu anayetualika sote katika kuunda mwili wake yaani Kanisa, jumuiya ya waamini, sisi sote bila kujali nafasi au wadhifa tu waalikwa na kamwe asitokee mmoja wetu kujichukulia nafasi ya kuwa mualika. Ni kwa kuwa na mtazamo huo tu hapo mashindano na mapambano yanayotokea katika jumuiya zetu hayawezi kutokea kwani kila mmoja wetu hana budi kujiona ni mualikwa. Mathalani kuwa askofu au kasisi, au shemasi au mtawa au katekista mlei au kiongozi mlei wa jumuiya zetu, ni kwa kuwa na mtazamo sahihi kama anavyotutaka Yesu katika Injili leo tunaweza kutambua zote ni nafasi za huduma na utumishi na udogo na kuwa wa mwisho na kamwe sio fursa za kuwa mabwana wakubwa na waheshimiwa.

Leo hii naomba nikiri hata kati ya wadarajiwa kumekuwa na mapambano na chuki na magomvi kwa kukosa kuielewa na kuiishi Injili ya Yesu Kristo kwani badala ya kuona nafasi zetu ni katika kuwa watumishi na wadogo mara nyingi zimekuwa chanzo cha kujikweza na kujitafutia heshima na upendeleo wa pekee. Yesu Kristo anatualika kubadili vichwa vyetu kwani aliye mkubwa ni yule anayekuwa mtumishi kama yeye na hivyo kujifunga na kutumikia wengine na si kusubiri kupata heshima na sifa. Baada ya Yesu kuwahubiria walioalikwa sasa anamgeukia mfarisayo aliyewaalika na kumtaka pia kubadili mtazamo wake. Ilikuwa ni desturi na kawaida si tu katika nyakati za Yesu bali hata katika nyakati zetu leo. Yesu anamwalika kuwageukia watu wanaosetwa na kudharaurika na kutengwa na ndio maskini, walemavu, vipofu na viwete.

Hii ni changamoto ya kuwaalika wale wasiokuwa na kitu cha kutulipa. Ni kuwaalika kama Mungu anavyotualika kwani hakuna hata mmoja wetu hata awe tajiri au mwenye uwezo kiasi gani wa kuweza kumlipa Mungu. Ni kualika bila kutarajia chochote na ndio upendo wa Kimungu tunaopaswa kuwa nayo, upendo usio na masharti wala kujitafutia faida yake wenyewe. Kwa Wayahudi aina ya watu kama viwete, vipofu, walemavu hawakuruhusiwa hata kuingia Hekaluni pale Yerusalemu hivyo Yesu anawaalika kubadili vichwa vyao kwa maana ya mtazamo wao. Labda hata leo tunapokuwa na sherehe zetu iwe katika ngazi ya familia zetu mara nyingi wanaingia ukumbini wale tu waliochangia, lakini hiyo ipo hata katika makusanyiko na sherehe za makanisani. Mara ngapi katika sherehe zetu za upadrisho au uaskofusho au jumuiya ndogo ndogo za Kikriso au Kiparokia tunawakumbuka wahitaji au watu wenye shida na kuwaalika?

Naomba nisitoe jibu wala hukumu ila tuingie ndani mwetu na kujihoji ni mara ngapi tunawajali na kuwakumbuka maskini au watu wenye mahitaji maalumu? Lakini pia maskini, vipofu, viwete na walemavu si tu watu wenye shida na ulemavu wa kimwili bali pia wale wenye shida na ulemavu wa maisha ya kiroho, watu wanaokuwa mbali au kujisikia mbali na Mungu, Je, ni mara ngapi tumewapa nafasi hawa na kujisikia kuwa Mungu anawapenda na kuwaalika washiriki naye karamuni? Ni kwa jinsi gani kama jumuiya ya waamini tumewaweka karibu wanaokuwa mbali na Mungu? Ni mara ngapi tumekuwa wakali na kuwatenga na hata kuwafungia huduma na masakramenti ya Kanisa badala ya kuona namna za kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usio na mipaka wala kipimo? Ni maswali yakututafakarisha katika Dominika yetu hii ya leo. Yesu leo anatualika kupenda bila masharti, kupenda kama vile Mungu anavyotupenda bila kutubagua, Mungu anatupenda sote iwe tuwe wema au wadhambi bila upendeleo wowote.  Tafakari njema na Dominika njema.

31 August 2019, 11:29