Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XX ya Mwaka C wa Kanisa: Moto wa Yesu ni Uso wa huruma ya Mungu inayotakasa na kuwatakatifuza watu waja wake! Moto ni huruma na upendo wake! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XX ya Mwaka C wa Kanisa: Moto wa Yesu ni Uso wa huruma ya Mungu inayotakasa na kuwatakatifuza watu waja wake! Moto ni huruma na upendo wake! 

Tafakari Jumapili 20 ya Mwaka: Moto wa Yesu duniani! Utakatifu!

Jumapili ya XX ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, waamini wanahimizwa kutafakari kuhusu moto wa Yesu uliotupwa hapa ulimwenguni. Huu ni moto wa huruma na upendo wa Mungu. Ni moto unaoganga na kuponya; moto unaotakatifuza na kuwaokoa watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia: wema, ukuu, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Yesu leo anazungumzia juu ya moto na ubatizo, kwa hakika ni lugha ngumu kueleweka mara moja kwetu. Sehemu ya Injili ya leo tunaona Yesu anatumia lugha ya picha, hivyo hatuna budi kuelewa vema maana kusudiwa na Yesu ili kupata ujumbe kwetu pia. Katika Agano la Kale mara baada ya gharika kuu tunaona Mungu anaweka ahadi ya kutoangamiza tena dunia kwa maji bali kwa moto. (Mwanzo 9:11) Ni kwa moto Mungu ataleta haki ulimwenguni. (Isaya 66:16) Hata Yohana Mbatizaji katika Agano Jipya tayari anazungumzia kuwa Masiha atatubatiza katika Roho Mtakatifu na kwa moto. (Mathayo 3:11-12) Hivyo hata Yesu leo anazungumzia kuja kuleta moto ulimwenguni. Hata Mitume wa Yesu, Yakobo na Yohane wana wa Zebedayo wanamuomba Yesu ashushe moto kutoka mbinguni ili kuja kuwaangamizi wasamaria waliokataa kumkaribisha Yesu katika vijiji vyao. (Luka 9:54) Na wazo linalotujia mara moja pia ni juu ya moto utokao mbinguni na kuja kuwaangamiza wale wote wanaokwenda kinyume na amri na maagizo yake wakati wa mwisho wa nyakati.

Ninawaalika kutafakari vema kwani kinyume chake tunaweza kujikuta tunakuwa kinyume na: Habari Njema,upendo, wema na huruma ya Mungu na hivyo kuanza kuwa na sura potofu ya Mungu.  Moto wa Mungu hauna lengo wala shabaha ya kuangamiza na kuwaondoa wadhambi kutoka katika sura ya dunia bali ni chombo cha kututakatifuza ili kuachana na dhambi, ni chombo cha kututakasa ili kuachana na dhambi. Siyo moto wa kuja kulaani na kuangamiza watu kwani hiyo kwa hakika sio Habari Njema kwa mwanadamu na wala haileti furaha na matumaini kwa yeyote anayeisikia. Najua kuna wahubiri wengi wanapenda kutumia lugha ya kutisha na kuogofya watu na kuona Mungu basi ana hulka sawa na sisi wanadamu dhidi ya wale wanaokuwa kinyume chake. Nawasihi ni vema kuacha kuwa na Sura ya Mungu inayopotosha na kuwa kinyume na Injili: Injili ni Habari Njema yenye kuleta furaha na matumaini kwa kila inayemfikia!

Moto wa Neno lake unaokuja ili sisi wadhambi tupate kuponywa na kujaliwa uzima wa milele na si kinyume chake. Ni moto wa Roho Mtakatifu uliowashukia Mitume siku ile ya Pentekoste unatushukia nasi kila mara tumuombapo ili kuweza kujua mapenzi yake na kuyashika katika maisha yetu. Ni moto unaokuja kututia joto la kuweza kushuhudia wema na huruma ya Mungu kwa watu wote, kuweza kuwa mashuhuda wa kweli zile za imani katika maisha yetu ya kila siku. (Matendo 2:3-11) Na ndio hamu ya Yesu kuona kuwa moto huo wa Mungu kuwa umewaka katika ulimwengu wetu, katika nafsi za kila mmoja wetu ili kuangamiza kila aina ya uovu na dhambi na ndio magugu katika mioyo yetu yanaokinza ile mbegu njema ya Neno la Mungu kuweza kumea na kukua na kutoa matunda. Ishara ya pili iliyokaribu na huo moto ndio Ubatizo. Neno Ubatizo linatokana na neno la Kigiriki batezo, likimaanisha zamisha. Hivyo ni hamu yake Yesu kutaka kuzama katika mateso na kifo na ufufuko wake ili kuukomboa ulimwengu, ili kutupatia uzima wa kimungu kila mmoja wetu, ili kurejesha uhusiano uliovunjika kati ya mwanadamu na muumba wake.  

Maji ya ubatizo wa Yesu ndio kifo chake kilichokuwa kimeandaliwa na watesi wake ili kuuzima moto wa Neno lake, wa upendo wake wa kimungu, moto wa Roho wake ya Kimungu yaani Roho Mtakatifu ila matokeo yake sisi tumepata kuponywa na ukombozi wetu. Pasaka ni uumbaji mpya, ni mwanzo wa nyakati mpya, ni mwanzo mpya kwa kila mmoja wetu kwani sasa tunatembea katika mwanga na si wana tena wa giza kwani tupo huru kama wana wa Mungu na si watumwa tena wa yule mwovu. Na ndio Yesu anatukumbusha pia wanafunzi wake kuwa kama Yeye aliye Bwana na Mwalimu amekunywa kikombe kile cha mateso na kifo basi anatuandaa nasi kukumbuka ulazima wa kupitia njia ile ile ya Msalaba ya kuteswa na kukataliwa na kufanyiwa kila aina ya ubaya kama ambavyo amepitia Yeye aliye Bwana wetu. Hakuja kuleta amani duniani bali migawanyiko, ndiyo lugha ya kutualika kila mara kutambua kuwa kwa kumfuasa Kristo tutabaguliwa na kutengwa hata na watu wetu wa karibu kama wazazi au ndugu.

Ujumbe wa Injili daima ni moto kwani unakuja kututoa katika hali zetu za zamani na kuanza maisha mapya. Ni ujumbe unaokuja kuangamiza na kutetekeza kila aina ya uovu na ubaya ndani mwetu. Ni ujumbe wa kubadili vichwa na namna zetu iwe za kufikiri au za kutenda. Na kwa kuwa mashuhuda wa Injili hakika tutakunana ukinzani na upinzani wa kila aina kwani bado kuna wale wasiokuwa tayari kuangamiza na kutetekeza ndani mwao yao yalio ya ulimwengu huu na kuanza kufuata mantiki mpya, mantiki ya Mungu mwenyewe. Ndugu zangu yafaa kuwa makini Injili sio chuki, sio magomvi au vita kwa wale wanaokinza au kuwa kinyume nayo kwani narudia ikifikia hapo basi inakoma kuwa Habari Njema inakuwa kitu kingine. Mipasuko na migawanyiko anayozungumzia Yesu haipaswi kutokana na mapungufu yetu au hulka na tabia zetu bali ni kwa wale wasiokuwa tayari kubadili vichwa vyao, kwa maana ya kuisikiliza na kuishi kadiri ya moto wa Neno la Mungu. Hivyo si kwamba Yesu anatutuma kuwa kama wanaharakati au wapigania uhuru fulani kutoka na kuanza kushambuliana na kila mmoja anayekuwa kinyume na Injili, la hasha hilo sio kusudi na wala sio maana ya Injili ya leo. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

17 August 2019, 14:24