Tafuta

Vatican News
Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini tangu tarehe 18-24 Agosti 2019: Kardinali Bassetti amekazia umuhimu wa vijana kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo. Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini tangu tarehe 18-24 Agosti 2019: Kardinali Bassetti amekazia umuhimu wa vijana kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo. 

Mkutano wa Urafiki Kati ya Watu Italia- Kardinali Bassetti: matumaini

Kardinali Gualtiero Bassetti anawataka watu wa Mungu nchini Italia kila mtu kadiri ya wito na dhamana yake katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na jamii katika ujumla wake, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema utume wao. Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili na utakatifu wa maisha. Kanisa liendelee kuwekeza katika utume wa vijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake XL “40”. Kuanzia tarehe 18 -24 Agosti 2019, na unaongozwa na kauli mbiu “Jina lako linapata chimbuko lake kwa yale mambo msingi unayopania”. Hii ni sehemu ya utajiri unaobubujika kutoka katika mashairi yaliyowahi kutungwa na Mtakatifu Yohane Paulo II enzi ya ujana wake. Ni nafasi ya kuutafakari ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu, kama Mtakatifu Veronica alivyokirimiwa na Kristo Mwenyewe wakati wa Njia ya Msalaba, kuelekea Mlimani Kalvari. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mkutano huu, anawaalika waamini kuuangalia Uso wa Kristo Yesu: fukara, mtii na mseja kamili, ili aweze kuwasafisha na kuwatakasa na hatimaye, kuwapatia uwezo mpya wa kuwaangalia jirani zao kwa: huruma, upendo na kuwajali jinsi walivyo. Katika mtazamo kama huu, kwa pamoja wanaweza kupiga ukulele wa shangwe na kusema, kwa hakika: Mungu ni mkuu, mwema na anawajali.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Jumatatu, tarehe 19 Agosti 2019 katika hotuba yake, amewataka watu wa Mungu nchini Italia, kamwe wasikubali hata kidogo, baadhi ya wajanja wachache waweze kuwapoka ndoto ya maisha yao kwa siku za usoni. Huu ni ujumbe mahususi hasa kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Mbiu kwa vijana wote ni kwamba, “Mungu ni upendo”, Kristo Yesu anaokoa na kwamba, yu hai kabisa na kwa njia ya Roho Mtakatifu, vijana wanaweza kuboresha maisha yao. Sura ya tano ya Wosia huu wa Kitume inaonesha mapito ya ujana katika makuzi na ukomavu; vijana wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Vijana wanakumbushwa kwamba, wanaitwa na kutumwa kama wamisionari jasiri, ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yao katika ukweli, hii ni changamoto kwa vijana wote. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini na ukarimu, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Hiki ni kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Amewataka vijana kufanya maamuzi mazito katika maisha yao, kwa kumfuasa Kristo Yesu, ili kumtumikia Mungu pamoja na jirani zao. Ni katika mtazamo kama huu, vijana wanapaswa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Vijana watambue amana na utajiri wao; waheshimu na kuthamini tofauti zao msingi kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Miili yao ni Hekalu la Roho Mtakatifu, wajitahidi sana kuiheshimu na kuithamini na kamwe wasikubali kutumbukizwa katika ukoloni wa kiitikadi, unaovaliwa njuga  na Mashirika ya Kimataifa.

Vijana wajenge na kuimarisha mahusiano mema na matakatifu kati yao na kamwe wasikubali kutumbukizwa katika upweke hasi, kwani huko watalia na kusaga meno. Wawe makini katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Ni katika muktadha huu, vijana wajenge pia mahusiano na Fumbo la Utatu Mtakatifu na Kanisa katika ujumla wake, ili kuimarisha: imani, matumaini na mapendo. Wasikatishwe tamaa na dhambi pamoja na mapungufu ya kibinadamu yanayojionesha miongoni mwa viongozi wa Kanisa. Kardinali Gualtiero Bassetti anawataka watu wa Mungu nchini Italia kila mtu kadiri ya wito na dhamana yake katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na jamii katika ujumla wake, kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema utume wao. Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili na utakatifu wa maisha. Kanisa liendelee kuwekeza katika utume wa vijana kwa kuhakikisha kwamba, vijana wanasikilizwa, wanashirikishwa na kusindikizwa katika hija ya maisha yao hapa duniani, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Utu, heshima, uwajibikaji na utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayopaswa kukuzwa na kudumishwa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Vijana watambue karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu ili waweze kuyatumia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, na yote haya wayafanye na kuyatekeleza kwa njia ya upendo wa dhati. Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa wale waliokata tamaa. Huu ni wakati wa kusimama na kuanza kuchanja mbuga katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake na wala wasikubali wajanja wachache wawapoke furaha na matumaini katika maisha.

Rimini 2019

 

20 August 2019, 14:38