Tafuta

Vatican News
Mtandao  wa dini kwa ajili ya amani duniani "Religions for Peace" unapania kuwa ni jukwaa la majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtandao wa dini kwa ajili ya amani duniani "Religions for Peace" unapania kuwa ni jukwaa la majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  (AFP or licensors)

Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani: Ushirikiano & Mshikamano!

Mtandao wa "Religion for peace" unasema kwamba, ni wajibu wa dini mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba, zinadhibiti vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sanjari na kuondokana na misimamo mikali ya kidini na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani “Religions for Peace” ulizinduliwa kunako mwaka 1970. Hili ni jukwaa la majadiliano ya kidini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani duniani, “Religions for Peace” ambao kwa mwaka 2019 umeingia katika awamu yake ya kumi, ni tukio la maisha ya kiroho linalowaunganisha viongozi wa kidini na waamini wenye mapenzi mema kutoka katika nchi 125. Mkutano huu umezinduliwa hapo tarehe 20 Agosti na unakamilika tarehe 23 Agosti 2019 huko mjini Lindau nchini Ujerumani. Ni mkutano ambao unahudhuriwa pia na viongozi wakuu wa serikali, mashirika ya kimataifa na makundi mbali mbali ya kiraia yanayojipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sehemu mbali mbali za dunia!

Rais Frank Walter Steinmeier wa Ujerumani katika hotuba yake ya ufunguzi amekaza kusema, ni kinyume kabisa cha matamanio ya wengi kuona dini ikitumika kwa ajili ya kuhalalisha: vita, kinzani na mashambulizi ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Kimsingi dini inapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Ni wajibu wa dini mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba, zinadhibiti vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sanjari na kuondokana na misimamo mikali ya kidini na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko. Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani “Religions for Peace” ulizinduliwa kunako mwaka 1970.

Huu ni mtandao unaoratibiwa na viongozi wa kidini. Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria ambaye katika mkutano huu ni Mratibu mwenza, ndiye mwakilishi wa Kanisa Katoliki katika maadhimisho haya. Katika hotuba yake elekezi amesikitika kusema kwamba, leo hii umaarufu wa taifa lolote lile unapimwa kutokana na nguvu yake ya kijeshi na uwezo wake wa kiuchumi, ambao wakati mwingine ni matunda ya unyonyaji na ukandamizaji wa mataifa machanga duniani. Biashara ya silaha duniani, mashindano na ulimbikizaji wa silaha ni tishio kwa usalama na amani duniani.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika hotuba yake kwa wajumbe wanaohudhuria mkutano huu, amesema, tangu mwaka 1991, amekuwa akijibidiisha kuragibisha changamoto changamani zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kati ya changamoto hizi ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maendeleo fungamani ya binadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa sanjari na ujenzi wa utamaduni wa amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto hizi zinapaswa kushughulikiwa kwa njia ya mshikamano wa dhati, kila upande ukichangia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Hili ndilo lengo kuu la Mkutano wa Dini kwa Ajili ya Amani duniani. Viongozi wa kidini, serikali, wanasayansi, wachumi na wataalam kutoka katika medani mbali mbali za maisha, washirikiane kwa pamoja ili kujenga msingi utakaoiwezesha Jumuiy ya Kimataifa kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na haki; umoja na mshikamano, ili mwisho wa siku, watu waweze kuongoka, wabadilike na kuwa watu wema zaidi, kwa kutambua kwamba, hata katika tofauti zao msingi, watu wote wanaunda familia moja ya watu wa Mungu. Jambo la kukazia ni ukweli, uhuru, majadiliano ya kidini na kiekumene. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na familia nzima ya binadamu kwani madhara yake ni makubwa na kwa sasa ni kikwazo pia cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mambo haya yote yanaweza kufupishwa kwa kanuni inayokita mizizi yake katika upendo kwa Mungu, jirani na mazingira nyumba ya wote. Utu, heshima, haki msingi za binadamu; amani na utunzaji bora wa mazingira ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana.

Kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani ni kielelezo cha “dhana ya kifo cha Mungu katika maisha ya mwanadamu” na matokeo yake ni mauaji ya kimbari, vita, kinzani na uharibifu mkubwa wa mazingira; matukio ambayo yamejitokeza kwa kasi ya ajabu katika karne ya ishirini. Vita kuu ya Dunia na madhara yake, mauaji ya kimbari, Vita Baridi; Utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia. Yote haya ni matukio ambayo yanamwelekeza mwanadamu katika utamaduni wa kifo. Hofu na maamuzi mbele ni mambo yanayochangia pia kinzani na mipasuko ya kijamii. Asili ya dini ya kweli, ina mwezesha mwamini kuunganisha utu na heshima ya binadamu sanjari na uwepo endelevu wa Mungu ili kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano ya kijamii.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol amehitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, waamini wa dini mbali mbali hawana budi kujenga ndani mwao hofu ya Mungu, kwa kuambata misingi ya haki, amani na maridhiano; ukweli, upendo na mshikamano wa dhati. Licha ya changamoto za ukanimungu, lakini bado kuna kila sababu ya waamini kuendelea kuwa na matumaini ya kuweza siku moja kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Kuna haja ya kuendelea kufanya maboresho katika mahusiano ya watu, ili dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Watu wana kiu ya: haki, amani, uhuru wa kweli; huruma, upendo na mshikamano; mambo yatakayowasaidia kuondokana na utamaduni wa kifo, ili kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote.

Amani Duniani

 

22 August 2019, 15:06