Tafuta

Vatican News
Kwa mara ya kwanza Tamasha la vijana huko Parokia ya  Medjugorje limezinduliwa na Kardinali.Mahujaji wanafika huko kwa ajili ya kutafuta amani na utulivu rohoni mwao Kwa mara ya kwanza Tamasha la vijana huko Parokia ya Medjugorje limezinduliwa na Kardinali.Mahujaji wanafika huko kwa ajili ya kutafuta amani na utulivu rohoni mwao 

Medjugorje:Idadi kubwa ya wanahija inaongezeka.Watu wanatafuta hali halisi ya kiroho!

Mahojiano na Askofu Henryk Hoser, mjumbe maalum wa kitume kwa ajili ya Parokia ya Medjugorje kuhusiana na shughuli za kitume na maendeleo katika parokia hiyo kwa mtazamo wa utume aliokabidhiwa na Baba Mtakatifu Francisko.Kwa sasa ni idadi kubwa ya mahujaji wanaofika kwa kuvutiwa sala,utulivu,kitubio na kutafuta hali halisi ya amani rohoni mwao!

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kila mwaka watu wanakwenda Medjugorje katika nchi za kibalkan wakitafuta kwa namna ya pekee hali ya amani, ya sala ambayo inapatikana katika sehemu hiyo, kati ya milima ya Bosinia-Erzegovina na inatoa fursa nzuri kwa yule anayetaka kufanya uzoefu wa amani. Tangu mwezi Mei mwaka huu hasa Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kutoa uamuzi wa kuruhusu wanahija waende Medjugorje kwa kusindikizwa kiparokia, watu kwa hakika wanajiandaa rasmi kijimbo na kiparokia na siyo tena kufanya hivyo kwa mtindo wa faragha kama ilivyokuwa mwanzo na ambapo sasa idadi kubwa ya waamini wanafika kwa wingi sana wakiwemo hata wageni maarufu.

Katika kiangazi hiki katika milima ya Krizevac kwa namna ya pekee wamefika hata Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Roma, Askofu Mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji mpya na Askofu Giampaolo Crepaldi wa jimbo la Trieste. Hii ni ishara ya uhusiano kati ya Medjugorje, Kanisa la Ulimwengu na Vatican kwa mujibu wa maelezo ya  Askofu Mkuu Henryk Hoser, mjumbe maalum wa kitume kwa ajili ya usimamizi wa maparokia ya Medjugorje. Ikiwa bado hakuna habari mpya zaidi kuhusu hali halisi ya Medjugorje ambayo imetolewa na mamlaka ya Kanisa, lakini hatua nyingi ziliozopigwa mbele zinaonekana kwa upande wa kukaribisha mahujaji, yote hiyo ni shukrani kutokana na utume uliokabidhiwa na Askofu  Hoser katika eneo la Balkan. Ili kujua zaidi yafuatayo ni mahojiano na Gazeti la Baraza la Maaskofu Italia (SIR) na Mjumbe Maalum katika eneo hilo.

Askofu Mkuu Hoser tayari una uzoefu zaidi ya mwaka mmoja wa Medjugorje. Je ni jambo gani limebadilika katika kipindi hicho. Na maoni yapi uliyo nayo?

Huu ni utume wangu wa pili huko Medjugorje. Miaka miwili iliyopita nilikuja kwa mara ya kwanza ili kuelewa hali halisi na sasa ni mwaka mmoja  ninaishi hapa kama mjumbe wa kitume katika tabia maalum. Ninaweza kusema kuwa kuna mabadiliko ya kushanganza, lakini mabadiliko hayo ni ya maendeleo kuhusiana na kiungo kizima cha Medjugorje hasa katika kuhakikisha kuwa wanahija wanapata mapokezi mema na siyo mambo ya kufanya tu, lakini zaidi ya kiroho. Hii lakini ni changamoto ngumu kwa sababu idadi kubwa ya wanahija kutoka duniani kote imezidi kuongezeka sana. Na hawa wanahitaji kusindikizwa kwa lugha zao za kuzaliwa. Kutokana na hili sisi tuna masanduku 16 tu ya kutafsiri lugha moja kwa moja wakati wa liturujia na katekesi.

Zipo pongezi kubwa kwa mtazamo wa idadi ya watu ambao kila mwaka wanakwenda Medjugorie? Je ni kitu gani kinawavutia?

Ndiyo idadi kwa hakika inazidi kuongezeka, na kwa upande wetu idadi inazungukia kati ya milioni tatu  ya watu kwa mmwaka na ongezeko hilo kubwa hasa ni wakati wa kiangazi, lakini pia hata mahujaji wengine wanafikika kipindi chote cha mwaka. Ni vigumu kuelezea kuhusu kile kinachowavuta, siyo jambo la kushikika au kufumbatika na kugusa. Watu wanatafuta hali halisi ya kiroho ambayo inapatikana tu kwenye vipindi vya sala, kuabudu ekaristi, kufanya tafakari ya Neno la Mungu, kuudhuria sakramenti ya kitubio na ambayo ndiyo kitu muhimu sana kwa upande wa Medjugorje kinachojulikana na tabia hiyo.  Aidha pia sehemu kubwa wa waamini wanatoka nchini Italia na Poland, lakini pia wapo wanahija wengi kutoka sehemu mahalia, kama vile Bosnia-Erzegovina, Croazia na nchi zote za kibalkan kwa ujumla. Hali hii ya amani na kuwa na utulivu, ya kuwa na kipindi na Bwana, inawavutia watu na wanaishi kipindi cha uzoefu wa imani,wanamkaribia Mungu na wengine wengi pia wanawaleta hata marafiki zao.

Wewe unaishi kandoni mwa Kanisa la Mtakatifu Yakobo, lililokabidhiwa na Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko. Je wewe ukiwa na madaraka ya kawaida, parokia inasimamiwa na kupangwaje?

Parokia inafanya kazi vizuri, kwa sababu ya jitihada ya kuendelezwa na watu wengi, awali ya yote na  makuhani. Kwa upande wa Parokia ya Medjugorje wanatoa huduma mapadre13 wakifransiskanina  ambapo kama kuna makundi mengi ya mahujaji, pia wanasaidiwa hata na mafrateli wengine au mapadre wa jimbo la Mostar-Duvno. Vile vile msaada pia unatokana  hata kwa mapadre ambao wanasindikiza makundi mbalimbali hasa kuhusiana na sakramenti ya kitubio; lakini pia mahujaji wanafanya mafungo ya kiroho, kwa maana Medjugorje inajulikana sana kuhusu suala la mafungo ya kiroho na mfungo wa  chakula ambapo kwa wiki moja, watu wengi wanabaki wakila mkate na maji tu. Katika utaratibu mzima wa shughuli za utume wa Parokia ya Medjugorje, tuna mpango wa wiki ambao ni wenye utajiri mkubwa  sana, asubuhi kuna misa katika lugha mbalimbali na katekesi, wakati mchana ni kusali Rosari na Misa ya jioni pamoja na tafakari. Mara tatu kwa wiki kuna suala la  kuabudu Sakrameti Takatifu na mara moja kuheshimu Msalaba.  Pia kuna kuna vilima viwili: kwanza cha Krizevac ambacho ni kilima cha msalaba, mahali ambapo msalaba huo ni mkubwa na watu wanapanda kilima hicho huku wakifanya njia ya msalaba na kilima cha pili Podbrdo ni mahali ambapo kuna sanamu ya Bikira Maria ambapo wakati wa kupanda kilima hicho watu wanasali Matendo ya Rosari Takatifu.

Nchi ya Bosnia-Erzegovina ni nchi ambayo kwa mtazamo imepata pigo, kwa upande wako eneo kama Medjugorie ni rasilimali ya nchi?

Bila shaka watu wamejua Bosnia-Erzegovina kwa sababu ya Medjugorje, eneo maarufu ambalo linatoa mwelekeo chanya kwa upande wa maisha kijamii na kwa utamaduni wao uliosambaa kuhusiana na Mama Maria Malkia wa amani. Nchi za Kibalkan zimefanya  uzoefu wa vita vya kutisha na mauaji na waathirika wengi, kwa maana hiyo bado  kumbukumbu ya vita ni hai na ndiyo maana kuna haja ya uhamasishaji wa amani ambao unatufundisha kwa yule anayeishi hapa kuwa na amani. Na katika nchi hii wapo watu wa makabila na dini tofauti, na kati ya  makundi matatu tofauti ni waislam, waorthodox na wakatoliki kwa maana nyingine Medjugorje inapendekezwa kuwa, wote wanaalikwa kuwa wa amani na umoja wa kitaifa!

Je! hali ya Medjugorje ikoje ?

Hali ya Medjugorje katika miaka ya mwisho imebadilika, mimi nilitumwa na Baba Mtakatifu na ninawasiliana kawaida na Katibu wa Vatican ambapo ninamweleza shughuli zote zinazoendeshwa na hali halisi na maendeleo yake. Medjugorje hadi sasa bado haijapewa jina rasmi la Madhabahu, hapa kuna parokia tu ya Medjugorje ambayo siyo madhabahu ya kitaifa na wala kijimbo. Bado haijapata jina na bado haijahusishwa huku Medjugorje na suala lolote la madhabahu.

Katika mwaka wa mwisho, uhusiano wa kina umekuwapo na Kanisa la Italia. Wewe umekutana na maaskofu wa Umbria akiwa na  Kardinali Bassetti huko Sarajevo na tarehe Mosi Agosti, hapa Medjugorje amefika Kardinali De Donatis. Ni ishara ya ukaribu wa namna ya pekee?

Ndiyo, wameanza kuja hata makardinali na maaskofu. Kwa mara ya kwanza Tamasha la Vijana 2019  limezinduliwa Mosi Agosti na Kardinali, kwa tukio hili  alikuwa na Kardinali De Donatis, makamu askofu Mkuu wa Roma na baadaye tukio hilo lilifungwa tarehe 6 Agosti 2019 na Askofu Mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji mpya. Tunayo fuaraha kubwa kwa uwepo wa wachungaji hata wa Italia na wa ulimwengu mzima ni maonesho ya uhusiano wa kina kati ya Medjugorje, Kanisa la Ulimwengu lakini hata Vatican. Amehitimisha Askofu Mkuu Hoser kuelezea juu ya shughuli ya utume wa Medjurugorje.

Kuhusiana na utume huu wa Parokia ya Medjurgorje

Ikumbukwe kwamba Baba Mtakatifu Francisko alimtuma Askofu Mkuu Hoser kwenda kutembelea Parokia za Kibalkani hasa Medjugorje inayojulikana duniani  kutokana na uongofu wa watu wengi hata maungamo. Askofu Mkuu Henryk Hoser, ni mzaliwa wa Poland na  maisha yake yamepitia katika shughuli za kitume huko Afrika, Ufaransa, Holand, Poland na sasa hata kutumwa katika parokia ya kibalkan ijulikanayo na historia ya tukio la Maono ya  ya Bikira Maria kunako tarehe 26 Juni 1981 kwa mujibu wa watu sita ambao bado wanaishi. Lakini Kanisa bado halijatoa tangazo rasmi zaidi ya utume wa kusaidia watu waweze kusali vema na kusindikizwa kiroho.

20 August 2019, 15:39