Tafuta

Vatican News
Mwaka wa Familia nchini Tanzania: Kardinali Polycarp Pengo, anasema, familia ni Kanida dogo la nyumbani, shule ya imani na maadili Mwaka wa Familia nchini Tanzania: Kardinali Polycarp Pengo, anasema, familia ni Kanida dogo la nyumbani, shule ya imani na maadili 

Kardinali Polycarp Pengo: Familia ni: Kanisa dogo, shule ya imani na maadili

Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaadhimisha Mwaka wa Familia unaoongozwa na kauli mbiu: “Familia kama Kanisa la nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”. Kardinali Pengo anasema, kuna mila na desturi za kiafrika ambazo zilikuwa na mafao ya kijamii kwa wakati fulani, lakini sasa zimepitwa na wakati. Kuna umuhimu wa kupyaisha maisha na utume wa familia kadiri ya mpango wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa sala na tafakari ya Neno la Mungu; mahali pa kuonjesha huruma, upendo na msamaha! Ni mahali ambapo wanafamilia wanakua na kukomaa, wanapokeana kusaidiana jinsi walivyo ili kuufikia utimilifu na utakatifu wa maisha. Lakini zaidi, familia ni kiini cha uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda makini wenye mvuto na mashiko! Changamoto kwa familia ya Mungu Barani Afrika ni kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mila na desturi njema za kiafrika. Kamwe nchi za Kiafrika zisikubali kuyumbishwa kwa kulazimishwa kukubali ndoa za watu wa jinsia moja, kwani huu si mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema!

Hii ni sehemu ya mahojiano maalum kati ya Radio Vatican na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu  mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, wakati huu familia ya Mungu nchini Tanzania inapoadhimisha Mwaka wa Familia unaoongozwa na kauli mbiu “Familia kama Kanisa la nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”. Kardinali Pengo anasema, kuna mila na desturi za kiafrika ambazo zilikuwa na mafao ya kijamii kwa wakati fulani, lakini sasa zimepitwa na wakati. Kwa mfano ndoa za wake wengi, kwa sasa ni mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati! Kumbe, kuna haja kwa watu wa Mungu Barani Afrika kujitamadunisha na hivyo kukubali kuipokea Injili ya Kristo ili iweze kusafisha mila na desturi zilizopitwa na wakati, ili kujenga na kuimarisha Injili ya familia, inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa vitendo, kama kielelezo cha imani tendaji.

Kardinali Polycarp Pengo anakaza kusema, mchakato mzima wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, hauna budi kupata chimbuko lake ndani ya famili. Kutoka huko, wanafamilia wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa mchakato mzima wa uinjilishaji kama wanavyofanya wanachama wa Chama cha Kitume cha Utoto Mtakatifu. Watoto wengi, wamekuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji wa huruma ya Mungu ndani na nje ya familia zao: Wamekuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuwasaidia watoto wenye shida na wale wanaoishi katika mazingira magumu! Kwa njia ya malezi makini na endelevu, watoto hawa wanajengewa tangu mwanzo msingi wa uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Kwa upande mwingine, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” anasema kwamba, elimu na malezi kwa watoto ni wajibu msingi kwa wazazi, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa hekima, busara na uhuru. Wazazi na walezi wawe na dhamiri nyofu na haki ya kuchagua aina ya elimu kwa watoto wao, ili waweze kufanya maamuzi makini wakati wanapokabiliwa na hali tete; wawasaidie kuwa na dira na mwelekeo chanya wa maisha. Malezi yawasaidie watoto kuwajibika katika kufanya maamuzi yao. Elimu inapaswa kujikita pia katika subira jambo ambalo si rahisi sana katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambamo kuna mchaka mchaka wa maisha. Watoto wajengewe utamaduni wa kuomba msamaha pale wanapowakosea wengine, ili waweze kuwa na uhuru unaowajibisha.

Elimu ya jinsia inalenga pamoja na mambo mengine, kumsaidia kijana kukua na kukomaa katika fadhila ya upendo badala ya kuwageuza watu wengine kuwa ni vyombo vya kuridhisha tamaa ya mwili. “Ngono salama” inawajengea watu dhana dhidi ya zawadi ya maisha! Watu wakubali na kujipokea jinsi walivyoumbwa na Mwenyezi Mungu; waheshimu na kuthamini tofauti zinazojitokeza, kwani yote haya ni kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha sura ya saba kwa kujikita katika umuhimu wa kurithisha imani, kwani familia inapaswa kuwa ni mahali pa kufundishia jinsi ya kupokea tunu na uzuri wa imani; mahali pa sala na huduma. Wazazi na walezi wawe ni vyombo na mashuhuda wa katekesi makini wanayoishuhudia na kuwafundisha watoto wao kuipokea katika uhuru kamili!

Kardinali Pengo: Familia

 

19 August 2019, 14:21