Vatican News
Kardinali Louis Raphael Sako wa kwanza, Patriaki wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo ameandika Waraka wa Kichungaji kwa Wakleri akikazia huduma inayosimikwa katika utu wa binadamu. Kardinali Louis Raphael Sako wa kwanza, Patriaki wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo ameandika Waraka wa Kichungaji kwa Wakleri akikazia huduma inayosimikwa katika utu wa binadamu.  (AFP or licensors)

Waraka wa Kichungaji kwa Mapadre wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo: Utu wa binadamu!

Uongozi wa Kanisa unakita mizizi yake katika huduma makini. Hiki ni kielelezo cha utu wa mwanadamu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa si kwa ajili ya kutafuta heshima, ustawi na mafao ya mtu binafsi. Na wala si kichaka cha uchu wa mali na madaraka! Uongozi ni huduma inayomwilishwa katika upendo. Ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya: kuongoza, kufundisha na kutakatifuza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandiko Matakatifu yanamweka Kristo Yesu kuwa ni njia, ukweli na uzima. Ndiye mchungaji mwema anayewaongoza waja wake kwa mfano bora wa maisha, unyenyekevu, upendo na sadaka iliyofikia kilele chake pale juu Msalabani anapoinamisha kichwa na kutoa roho, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Yesu katika maisha yake alijitosa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanapata huduma yao: kiroho na kimwili. Kwa kuwaondolea dhambi zao, kwa kuwaponya magonjwa yao, kwa kuwalisha na kuwanywesha wakati wa njaa na kiu! Kwa miaka mitatu aliwafundisha Mitume wake tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika Heri za Mlimani na Sala ya Baba Yetu. Akawarekebisha pale walipokosea njia na kutopea katika ubinafsi. Akajitahidi kuwalinda na kuwaelekeza katika ukweli, haki na upendo. Akayafunga madonda na majeraha yao kwa imani, matumaini na mapendo, kiasi cha kuwanyanyua wale waliokata tamaa na kuanza hija mpya ya maisha.

Kristo Yesu ni mfano bora ambao viongozi wote wanaweza kujifunza kutoka kwake  namna ya kutimiza dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa. Kwa hakika, Yesu ni mfalme wa kweli na uzima; Mfalme wa utakatifu na neema; ni Mfalme wa haki, upendo na amani. Kardinali Louis Raphaël  Sako wa kwanza, Patriaki wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo, katika Waraka wake wa kichungaji kwa Wakleri wa Babiloni ya Wakaldayo anawakumbusha kwamba, uongozi wa Kanisa unakita mizizi yake katika huduma makini. Hiki ni kielelezo cha utu wa mwanadamu na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa si kwa ajili ya kutafuta heshima, ustawi na mafao ya mtu binafsi. Na wala si kichaka cha uchu wa mali na madaraka! Uongozi ni huduma inayomwilishwa katika upendo na kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu.

Kardinali Louis Raphaël  Sako wa kwanza amefafanua Waraka wake wa kichungaji wakati wa mafungo ya mwaka ya maisha ya kiroho alioyatoa kwa wakleri wa Babiloni huko mjini Erbil, nchini Iraq. Huu ni mwaliko wa kupyaisha tena ari na mwamko wa kimisionari katika maisha ya kiroho, kijamii na katika uongozi wa Kanisa kama huduma ya upendo inayomwilishwa katika unyenyekevu, uvumilivu na ustahimilivu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Iraq. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa watu wa Mungu wanaowahudumia kwa ari na moyo mkuu! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wadumu katika sala, ili kweli waweze kuwa ni Mitume aminifu wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao! Watambue kwamba, utu, heshima na ukuu watavipata, ikiwa tu kama wataweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya uongozi unaomwilishwa katika huduma ya upendo.

Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha uhusiano binfasi na Kristo Yesu kwa njia ya: Neno la Mungu, maisha ya sala; maadhimidho ya Sakramenti za Kanisa na kwamba, yote haya yanapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Wakleri na watawa waheshimiane, wapendane, wasaidiane na kushikamana katika maisha na utume wao miongoni mwa familia ya Mungu. Inasikitisha na kusononesha pale inapoonekana kwamba,  baadhi ya wakleri na watawa wanashindwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kutokana na ubinafsi wao. Wakleri na watawa wajenge na kuimarisha mafungamano ya upendo na waamini walei wanaowahudumia kwa niaba ya Kristo Yesu. Wakleri na watawa wajenge na kuimarisha tasaufi ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Kwa njia hii, wataweza kuwa ni chachu na mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya, kiasi hata cha wao kuweza kufanya maamuzi mazito ili kumfuasa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Kardinali Louis Raphaël  Sako wa kwanza anasikitika kusema kwamba, kupungua na kuendelea kunyauka kwa miito ya maisha ya kitawa na kipadre ni kutokana na kukosekana kwa mashuhuda wenye mvuto na mashiko! Kumbe, uchu wa mali na madaraka; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; utandawazi usiokuwa na mashiko wala mguso visipewe nafasi katika maisha na utume wao, kiasi cha kuwaharibia imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakleri na watawa wajitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha kadiri ya miongozo inayotolewa na Mama Kanisa. Mafungo ya kiroho ni fursa makini kwa ajili ya: kusali na kutafakari, tayari kujiandaa kwa ajili ya madhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Ni muda wa kwenda jangwani ili kujichotea nguvu za maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuliandama Kanisa na jamii katika ujumla wake! Ni muda wa kujitafutia upweke chanya na ukimya ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu.

Ni wakati muafaka wa kupyaisha ari na mwamko wa utume na shughuli za kimisionari na kichungaji katika maisha ya kiroho, kijamii na kikanisa. Kardinali Louis Raphaël  Sako wa kwanza anakaza kusema, Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” unafafanua mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Makanisa mahalia katika mchakato wa malezi na majiundo ya kipadre. Ni mwongozo makini unaotoa sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa katika hija ya malezi ya majandokasisi na mapadre kama sehemu ya majiundo endelevu. Mkazo umewekwa katika majiundo ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; umuhimu wa maisha ya Kisakramenti; Mafundisho Tanzu ya Kanisa bila kusahau malezi  na majiundo ya kiakili, kiutu na kichungaji kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Yote haya yakitekelezwa kwa umakini mkubwa, wakleri, watawa na waamini walei wataweza kutekeleza dhamana na wajibu wao katika umoja, upendo na mshikamano unaowawezesha kufanya kazi kama kikosi cha ushindi! Changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni kuendelea kupukutika kwa miito ya maisha ya kitawa na kipadre miongoni mwa waamini wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo. Bado kuna kinzani na mipasuko ya ndani kwa ndani inayopaswa kugangwa na kuponyeshwa kwa mafuta ya huruma na mapendo kutoka kwa Kristo Yesu, ili kujenga na kuimarisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa watu wa Mungu. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji bado ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu katika ujumla wake.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake kwa familia ya Mungu nchini Iraq,  ambako anatarajia kwenda kufanya hija ya kitume mwaka 2020, Mwenyezi Mungu akipenda. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ustawi na mafao ya wengi, utasaidia kuvunjilia mbali chuki na uhasama unaokita mizizi yake katika migogoro ya kidini katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini kimsingi ni mgogoro unaojikita katika uchu wa madaraka.

Kardinali Sako: Waraka

 

08 August 2019, 14:56