Kardinali Charles Maung Bo karika Waraka wake wa kichungaji anapembua kwa kina na mapana matizo, changamoto na umuhimu wa kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kardinali Charles Maung Bo karika Waraka wake wa kichungaji anapembua kwa kina na mapana matizo, changamoto na umuhimu wa kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Kardinali Charles Maung Bo: Waraka wa kichungaji nchini Myanmar: Mateso ya watu!

Kardinali Maung Bo: “Tafakari kutoka pembezoni mwa jamii; Upendo wa Mungu kwa watu na taifa la Bara la Asia” anapembua: haki na wajibu; umuhimu wa kujenga na kudumisha Injili ya amani inayokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza kati yao. Anagusia changamoto ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon nchini Myanmar katika Waraka wake wa kichungaji unaoongozwa na kauli mbiu “Tafakari kutoka pembezoni mwa jamii; Upendo wa Mungu kwa watu na taifa la Bara la Asia” anazungumzia kuhusu: haki na wajibu; umuhimu wa kujenga na kudumisha Injili ya amani inayokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza kati yao. Anagusia changamoto ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao; uhuru wa kidini pamoja na athari za misimamo mikali ya kidini na kiimani, bila kusaha changamoto changamani zinazoendelea kuwakumba wananchi wa Myanmar. Kardinali Charles Maung Bo katika Waraka wake wa kichungaji anawataka watu wa Mungu nchini Myanmar kutambua haki na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Anawataka wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kutambua kwamba, upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa litaendelea kuonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwani wao ni amana na utajiri wa Kanisa. Kanisa na Serikali vishirikiane katika kukuza na kudumisha haki jamii, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii, ili kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu wote, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni amana na utajiri mkubwa unaopata chimbuko lake katika miaka 1891 kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu na heshima ya binadamu. Ni mafundisho yanayobubujika kutoka katika majadiliano kati ya imani na akili ya mwanadamu, ili kumuenzi mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mafundisho haya yanajikita kwa namna ya pekee katika haki, amani, upendo na upatanisho. Ni mafundisho ambayo yanajenga msingi wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Kanuni maadili.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaonesha haki na wajibu; mafao ya wengi na kwamba, sera za maendeleo fungamani ya binadamu zinapaswa kumgusa mtu mzima: kiroho na kimwili kwani tatizo kubwa katika ulimwengu wa utandawazi ni ukosefu wa usawa kati ya watu hali inayopelekea kinzani na migogoro ya kijamii. Ukweli, Uhuru na Usawa ni vikolezo vikubwa na msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu.Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mipango ya maendeleo fungamani nchini Myanmar. Watu wahamasike kutafuta na kudumisha haki jamii; uhuru, demokrasia shirikishi na kwamba, kila mtu anapaswa kutekeleza vyema wajibu na dhamana yake katika maisha ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Haki za wakimbizi na wahamiaji ziheshimiwe na kuthaminiwa na wote. Papa Francisko anasema, mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma endelevu na fungamani kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha.

Kardinali Charles Maung Bo anasema, msingi wa Injili ya amani nchini Myanmar ni: wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu. Amani ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Myanmar kwa miaka mingi haijawahi kushuhudia amani ya kudumu, jambo la msingi ni kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Tofauti msingi zinazojionesha nchini Myanmar hazina budi kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote na kamwe zisiwe ni tishio kwa umoja na mafungamano ya kitaifa. Wananchi wa Myanmar wanapaswa kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza kati yao.

Huu unaweza kuwa ni mwanzo wa kuganga na kuponya tofauti, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kanisa lina thamini na kukazia tofauti msingi kama amana na utajiri wa watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, “Imago Dei”. Kardinali Maung Bo anakazia Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu vita na amani sanjari na kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ambayo kwa sasa imepitwa na wakati ili kujenga na kuhimiza kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, ili kupambana na mauaji ya kimbari. Anasema kuna haja ya kubomoa kuta na utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengi; kuta zinazoendelea kujengwa kwa kisingizio cha usalama, utulivu na amani jamii. Amani ya kweli inaweza kufikiwa kwa kujikita katika mchakato wa huruma kama unavyofafanuliwa kwenye ule mfano wa Baba mwenye huruma, mshikamano wa kisiasa; kanuni maadili na mwingiliano wa watu ndani ya jamii. 

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya familia ya Mungu nchini Myanmar ni vita, mwaliko ni kuwa ni wajenzi na vyombo vya amani. Amani ya kweli isaidie kuimarisha: upendo, demokrasia shirikishi na utawala wa sheria, umoja na mshikamano wa kitaifa. Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu! Vikosi vya ulinzi na usalama vinapaswa kusimamia haki na amani; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Familia ya Mungu nchini Myanmar kwa sasa haina budi kujielekeza zaidi katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ya kitaifa kwani upendo wa Mungu hauna mipaka. Kardinali Charles Maung Bo anaendelea kufafanua kwamba, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uhuru wa kidini ni kiini cha haki msingi za binadamu kinachompatia mwamini uwezo wa kufikiri na kutenda kadiri ya dhamiri yake nyofu na kwamba, haki hii ni chimbuko la utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uhuru wa kidini unapaswa kuzingatiwa na kuendelezwa kisheria.

Binadamu aliyeumbwa kwa akili na utashi kamili, anasukumwa na maumbile na kanuni maadili kuutafuta ukweli, kuuambata na kuushuhudia. Uhuru wa kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii na kati ya Mungu na binadamu. Myanmar kama ilivyo hata kwa nchi nyingi Barani Asia, uhuru wa kidini umetiwa rehani. Vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani ni kati ya mambo yanayoendelea kuhatarisha haki msingi za binadamu; utu na heshima yake. Ubaguzi wa rangi unaoendelea kukita mizizi yake hata katika mambo ya kidini na kisiasa ni hatari sana kwa Myanmar. Huu ni wakati wa kujenga na kuimarisha dhamiri nyofu, kwa kujikita katika Injili ya upendo na huruma, haki, amani na maridhiano. Tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu nchini Myanmar zinasimikwa katika “Metta, karuma na salam: yaani upendo, huruma na amani.

Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon nchini Myanmar katika Waraka wake wa kichungaji anabainisha pia changamoto nyingine zinazoendelea kuwapekenya wananchi wa Myanmar. Hizi ni pamoja na: Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na athari zake, zinaendelea kuwatumbukiza wananchi wengi wa Myanmar katika umaskini wa hali na kipato. Kuna maelfu ya watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Balaa la ujinga linaendelea kukua na kupanuka kwa kasi kubwa kwani takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 60% ya watoto wa shule za msingi hawawezi kuhitimu masomo yao. Hii ni hatari kwa mustakabali wa jamii kwa sasa na kwa siku za usoni. Zaidi ya asilimia 40% ya wananchi wa Myanmar wanakabiliwa na umaskini mkubwa.

Mambo yote haya yanachafua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu wanapaswa kusimama na kuanza kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Kanuni maadili na utu wema, viwawezeshe wananchi wa Myanmar kuishi kwa amani, umoja, upendo na ushirikiano kwa kutambua kwamba, Jina la Mungu ni huruma. Kanisa nchini Myanmar linataka kuwa ni chombo cha upendo, huruma, haki, amani na upatanisho wa kweli, kwa kufeyekelea mbali chuki na uhasama, ili kupandikiza mbegu ya huruma, upendo na mshikamano.

Kard. Maung Bo
17 August 2019, 15:19