Tafuta

Vatican News
Caritas Africa: Kanisa Barani Afrika halina budi kuanza mchakato wa kujitegemea kwa rasilimali: vitu, fedha na watu kama sehemu ya mcahakato wa uinjilishaji Barani Afrika. Caritas Africa: Kanisa Barani Afrika halina budi kuanza mchakato wa kujitegemea kwa rasilimali: vitu, fedha na watu kama sehemu ya mcahakato wa uinjilishaji Barani Afrika. 

CARITAS AFRICA: Kanisa Barani Afrika huu ni wakati wa mageuzi: Kujitegemea

Caritas Africa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa watu walioathirika na vita, majanga asilia; wakimbizi na wahamiaji. Kuna umuhimu kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho, ili kusaidia kusitisha na kukomeza vita, kinzani na mipasuko mbali mbali inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mkazo ni kujitegemea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; matendo ya huruma kiroho na kimwili ni mambo msingi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Upendo wa Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kuwa upendo wa kibinadamu unapata utimilifu wake katika upendo wa kimungu. Upendo huu unatafsiriwa kwa lugha ya Kigiriki kuwa ni Agape, kwa Kilatini, Caritas. Kanisa linapenda kukazia huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wake na kwamba, upendo wa Kimungu unalikamilisha na kuliwezesha Kanisa kusimama kwa miguu yake. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako tarehe 11 Novemba 2012 katika Barua yake binafsi “Intima Ecclesiae Natura” yaani “Huduma ya upendo ni asili ya Kanisa” alikazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu “Kerygma-martyria; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa “Leiturgia” na huduma ya upendo “Diakonia”.

Haya ni mambo makuu matatu yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanayamwilisha yote haya katika maisha yao kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Huduma ya upendo haina budi kugusa maeneo yote ya maisha ya waamini kuanzia katika ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi katika ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Kutokana na changamoto hii, kuna haja ya kuwa na miundo mbinu itakayosaidia utekelezaji wa Amri ya upendo kati ya watu! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, hivi karibuni jijini Kampala nchini Uganda, limehitimisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Kanisa Barani Afrika limetakiwa kuwekeza zaidi katika Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Maadili, Malezi na maisha ya kiroho kwa waamini Barani Afrika.

Maaskofu  wa SECAM wanawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ambazo ni utambulisho wa Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika. Waamini wahamasike kujiunga na vyama na mashirika ya kitume, ili kulea na kukuza imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, na kama sehemu ya ushiriki wao mkamilifu katika ujenzi wa fumbo wa Mwili wa Kristo yaani, Kanisa. Kanisa Barani Afrika halina budi kuendelea kushirikiana na kushikamana na viongozi wa kisiasa, ili kuwasaidia kuwajibika zaidi, ili kutafuta na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Gilbert Justice Yaw Anokye, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, Caritas Africa katika mahojiano maalum na Mtandao wa Habari wa AMECEA amegusia umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kuwekeza katika huduma ya maendeleo fungamani ya binadamu; kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu Barani Afrika.

Kanisa linapaswa kuhakikisha kwamba, linajitegemea kwa rasilimali fedha, vitu na watu kama sehemu ya ukomavu wa Kanisa Barani Afrika. Caritas Africa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa watu walioathirika na vita, majanga asilia; wakimbizi na wahamiaji. Kuna umuhimu kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho, ili kusaidia kusitisha na kukomeza vita, kinzani na mipasuko mbali mbali inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kanisa halina budi kusaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani athari za mabadiliko ya tabinchi zinaendelea kusababisha umaskini mkubwa wa hali na kipato; baa la njaa na utapia mlo wa kutisha; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; maafa pamoja na majanga asilia. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Barani Afrika ni kuzuia, kutibu na kukarabati pale inapowezeka. Hata hii pia ni sera na mikakati inayotekelezwa pia na Caritas Africa.

Tume za Haki na Amani za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar hazina budi kushirikiana kwani zinategemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Lengo kuu ni huduma ya maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Umefika wakati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar kuhakikisha kwamba, yanafuata muundo mbinu uliofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuunganisha huduma ya afya, wakimbizi, haki, amani, misaada na maendeleo kuwa chini ya kurugenzi moja ya maendeleo fungamani ya binadamu. Caritas Africa inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa rasilimali fedha ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali za maendeleo zinazojitokeza Barani Afrika. Umefika wakati kwa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Afrika na Madagascar kushirikiana kushikamana kwa pamoja, huku yakiongozwa na kanuni auni.

Kanisa Barani Afrika halina budi kuanza kujitegemea kama kielelezo cha ukomavu wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa Barani Afrika lianze kupunguza na hatimaye, kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka nje. Kanisa lianzishe miradi endelevu na kuisimamia kikamilifu kama inavyojionesha kwa Benki ya Caritas Kenya, Benki ya Biashara ya Mkombozi, Tanzania pamoja na Kitega Uchumi cha Kardinali Otunga, Nairobi, Kenya. Vitega uchumi hivi vikisimamiwa kwa kuzingatia kanuni maadili, ukweli na uwazi, vinaweza kuwa ni vyanzo vikuu vya fedha kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Kuna Mabaraza la Maaskofu Barani Afrika ambayo yameanzisha Makapuni ya Bima Kitaifa. Hizi ni changamoto zinazoweza kufanyiwa kazi na Mabaraza ya Maaskofu pamoja na majimbo kwa ajili ya kujitegemea, daima kila watu wakisoma alama za nyakati na kuzijibu kwa hekima na busara.

Umoja na mshikamano wa Kanisa Barani Afrika uliwezeshe hata Kanisa kuweza kujitegemea kwa rasilimali watu, yaani kuwepo na mbinu mkakati wa kubadilishana mihimili ya uinjilishaji, jambo ambalo linawezekana kabisa. Majimbo pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yaliyo bahatika kuwa na miito mingi yawe ni msaada kwa majimbo yanayochechemea kwa kuwa na uhaba wa wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu. Jambo la muhimu ni malezi na majiundo makini kwa Mapadre na watawa ili kuweza kukabiliana na changamoto katika mazingira mapya wakakotumwa na Majimbo pamoja na Mashirika yao! Majimbo yenye uwezo mkubwa kifedha yanaweza pia kusaidia malezi na majiundo kwa majimbo machanga zaidi Barani Afrika. Umefika wakati wa kufirikia na kutekeleza umoja na mshikamano wa mihimili ya uinjilishaji Barani Afrika badala ya kukimbilia Marekani na Ulaya, hata kama wanauhitaji mkubwa, lakini Caritas Africa inasema ukarimu uanzie Barani Afrika.

Askofu mkuu Gilbert Justice Yaw Anokye, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, Caritas Africa anasema, ujumbe mahususi ambao ange penda kuwapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Barani Afrika ni mapambano dhidi ya baa la umaskini Barani Afrika kwa kuhakikisha kwamba, wananchi wakati wa uchaguzi wanawachagua viongozi waadilifu watakaosimamia rasilimali za nchi zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuachana na viongozi ambao wamekuwa ni mzigo mkubwa kwa Bara la Afrika. Hawa ni viongozi waliomezwa na malimwengu na hivyo kutopea katika uchoyo na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka na matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kila aina Barani Afrika. Umaskini wa Bara la Afrika ni matokeo ya utawala mbaya, rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Bara la Afrika linaweza kusimama na kucharuka kwa sera na maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuwachagua viongozi bora, kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali za nchi zinatumika kikamilifu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na kudumisha demokrasia na utawala wa sheria. Haya yanayozungumzwa kwa ajili ya Serikali mbali mbali Barani Afrika, yanapaswa pia kuzingatiwa na Kanisa katika kuwachagua viongozi katika taasisi na ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Uchu wa mali na madaraka ni adui mkubwa wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kwa hakika “Huduma ya upendo ni asili ya Kanisa” inayojikita mambo makuu matatu kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu “Kerygma-martyria; maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa “Leiturgia” na huduma ya upendo “Diakonia”. Haya ni mambo makuu matatu yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa.

Caritas Africa.
12 August 2019, 14:50