Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamshukuru na kumpongeza Kardinali Polycarp Pengo kwa huduma mbali mbali alizowapatia watu wa Mungu nchini Tanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamshukuru na kumpongeza Kardinali Polycarp Pengo kwa huduma mbali mbali alizowapatia watu wa Mungu nchini Tanzania. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Shukrani Kardinali Polycarp Pengo! Jembe la nguvu!

Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anapenda kumshukuru na kumpongeza Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa huduma yake makini kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Amesimama kidete kulinda imani, maadili, umoja na mshikamano wa watanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2019, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuanzia sasa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambaye alibahatika kuwa na karama, uwezo na akili nyingi, kiasi cha kuweza kuchangamanua mambo na kutoa ushauri kwa wakati unaofaa.

Katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu kuanzia: nachingwea na Tunduru-Masasi,  Kardinali Pengo ameweza kusimama imara bila kuteteleka katika masuala ya imani, maadili na utu wema, na kwa njia ya msimamo wake, akaweza kuiepusha Tanzania katika dhoruba na mawimbi makali yaliyokuwa yanaisonga nchi. Kardinali Pengo katika maisha na utume wake, amekuwa ni chombo na shuhuda wa majadiliano ya kiekumene, kidini, kisiasa na kitamaduni; mambo yaliyosaidia kujenga na kuimarisha maridhiano, umoja na mshikamano wa kitaifa; daima ni kiongozi aliyesimamia: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na kipaji cha unyenyekevu na usikivu, kiasi kwamba alikuwa tayari kupokea watu, kuwasikiliza, kung’amua pamoja na kuwapatia ushauri. Kwa wale ambao wametekeleza kikamilifu ushauri wake, wamefanikiwa kupata suluhu ya changamoto zilizokuwa zinawaandama.

Kardinali Polycarp Pengo ni kiongozi aliyebahatika kuwa na ushauri chanya katika changamoto za maisha. Katika maisha na utume wake, hasa kwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, mafanikio makubwa yameonekana chini ya uongozi wake. Idadi kubwa ya Maaskofu walioko nchini Tanzania, wengi wao wamepitia katika mikono yake, kama wanafunzi na hata akawaweka wakfu kuwa Maaskofu, ili waweze kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni kiongozi ambaye amewathamini sana vijana, akawawekeza amana, utajiri, uzoefu na mang’amuzi yake katika malezi, leo hii, Jimbo kuu la Dar es Salaam linaendelea kuwa na idadi kubwa ya miito mitakatifu si tu kwa watawa na watu wa ndoa, bali hata kwa wingi wa Mapadre. Ameimarisha malezi, makuzi na majiundo endelevu ya Mapadre wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kama kielelezo cha ukomavu wa imani na mwanzo wa mchakato wa kujitegemea kwa rasimali watu, bila kusahau pia rasimali fedha. Jimbo kuu la Dar es Salaam ni kati ya Majimbo ambayo yana mwamko mkubwa katika kulitegemeza Jimbo kwa rasilimali fedha na vitu.

Hizi ni juhudi za Kardinali Polycarp Pengo katika utume wake. Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anaendelea kufafanua kwamba, Kardinali Pengo alikuwa ni mtu mwenye msimamo na malengo katika maisha na alijitahidi kuhakikisha kwamba, anatekeleza malengo yake kwa wakati. Kabla ya kung’atuka kutoka madarakani, alijipangia kwamba, Jimbo kuu la Dar es Salaam liwe limefikia Parokia 100, lakini hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2019, Parokia za Jimbo kuu la Dar es Salaam zimeongezeka zaidi ya namba aliyokuwa amekusudia. Nia ilikuwa ni njema, kuhakikisha kwamba, waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wanapata huduma ya kichungaji kwa karibu zaidi. Askofu Nyaisonga anasema, shukrani hizi kwa Kardinali Polycarp Pengo ni kwa niaba ya familia yote ya Mungu, nchini Tanzania. Kwa sadaka na majitoleo yake, yaliyowawezesha watu wa Mungu nchini Tanzania licha ya mawimbi mazito katika medani mbali mbali za maisha, kuendelea kusimama na kushikamana kama ndugu wamoja. Katika kipindi hiki cha kuachia uongozi, anamwombea Mwenyezi Mungu aendelee kumkirimia afya njema, nguvu na utashi wa kuzungumza, kushauri na kuwaongoza watu katika mwelekeo sahihi wa maisha.

Bado familia ya Mungu inahitaji kutumia hekima, busara na mapaji aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Polycarp Pengo, alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 huko Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 20 Juni 1971 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Na kwa kipindi cha miaka miwili yaani kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1973 aliteuliwa kuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Kati ya mwaka 1973 hadi mwaka 1977 alitumwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa la Laterano, Kitivo cha Taalimungu Maadili cha AlFonsianum, kilichoko mjini Roma. Aliporejea nchini Tanzania baada ya kuhitimu masomo yake, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwenda kufundisha taalimungu maadili Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.

Kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1983 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Gombera na muasisi wa Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa hakika, Kanisa la Tanzania linajivunia Seminari ya Segerea, matunda ya jasho na ubunifu wa Kardinali Polycarp Pengo. Tarehe 11 Novemba 1983 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea na kuwekwa wakfu wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari  1984 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Mtakatifu Yohane Paulo II. Akasimikwa rasmi kama Askofu wa Nachingwea hapo tarehe 19 Februari 1984. Tarehe 17 Oktoba 1986, atangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo Ii kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lengo likiwa ni kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini katika kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Akasimikwa rasmi tarehe 12 Februari 1987. Tarehe 22 Januari 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ua kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuingia Jimboni tarehe 24 Mei 1990.

Akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 12 Februari 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali na kumsimika rasmi tarehe 21 Februari 1999. Tanzania ikaweka historia ya kupata Kardinali miezi michache tu baada ya kufariki dunia, Kardinali Laurian Rugambwa. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2019, Kardinali Polycarp Pengo, akang’atuka kutoka shughuli za uongozi Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa ufupi, hii ndiyo historia ya Kardinali Polycarp Pengo ambayo imeandikwa kwa jasho, uvumilivu na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Pengo Kardinali
15 August 2019, 17:52