Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Canada linawahamasisha waamini kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Canada linawahamasisha waamini kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada: Waamini yatakatifuzeni malimwengu kwa ushuhuda amini!

Kuna hatari katika maisha na utume wa Kanisa, pale ambapo waamini walei wanajisikia kuwa wanyonge sana katika utume wao ndani ya Kanisa, kiasi cha kutamani kuwa ni wakleri. Au pale ambapo Mapadre wanawaaminisha waamini walei majukumu makubwa ya wito na maisha ya Kipadre kiasi cha kuwafanya kudhani kwamba, wao ni Mapadre. Kila mtu ana dhamana, wajibu na haki zake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake anawakumbusha daima Mapadre kwamba, wao ni wahudumu wa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanayotekelezwa na Kanisa kama sehemu ya maisha na utume wake hapa duniani na kamwe Mapadre si watumishi wa mshahara! Kuna haja kwa waamini walei kushirikiana kikamilifu na wakleri katika maisha na utume wa Kanisa, kila upande ukitambua dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa bila kuchanganya wala kuingiliana majukumu. Katika ulimwengu mamboleo kuna baadhi ya waamini walei wanadhani kwamba, kuna baadhi ya majukumu ya Mapadre wanaweza kuyatekeleza hata kama hawakuwekwa wakfu kwa ajili ya maisha, wito na utume wa Kipadre, kwa vile tu, wao wamebatizwa na kuimarishwa kwa Roho Mtakatifu katika Sakramenti ya Kipaimara! Kuna baadhi ya Mapadre nao wanadhani kwamba, wao ni watu wa mshahara wanaweza kutenda shughuli na utume wao kama waamini walei.

Hii ni dhambi ya hatari kabisa katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, kila wito una nafasi, wajibu na heshima yake ndani ya Kanisa. Kuna waamini walei ambao wanashiriki maisha na utume wa Kanisa kama: Manabii, Wafalme na Makuhani. Kuna waamini ambao wamepewa Daraja Takatifu na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu kama utimilifu wa Daraja Takatifu. Kuna watawa ndani ya Kanisa wanaolihudumia Kanisa kwa njia ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Hawa wanajifunga kwa njia ya nadhiri ya: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Kwa ujumla familia ya Mungu inaitwa na kuhamasishwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Utakatifu si upendeleo kwa watu wachache ndani ya Kanisa, bali ni mwaliko kwa waamini wote kuwa ni wakamilifu na watakatifu kama alivyo Baba yao wa mbinguni!

Kuna hatari katika maisha na utume wa Kanisa, pale ambapo waamini walei wanajisikia kuwa wanyonge sana katika utume wao ndani ya Kanisa, kiasi cha kutamani kuwa ni wakleri. Au pale ambapo Mapadre wanawaaminisha waamini walei majukumu makubwa ya wito na maisha ya Kipadre kiasi cha kuwafanya kudhani kwamba, wao ni Mapadre. Utume na maisha ya waamini walei ndani ya Kanisa ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Waamini walei kwa njia ya ushuhuda wao, wanakuwa ni vyombo muhimu sana vya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda, dhana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni sehemu ya Barua ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada inayochambua hatari kubwa kwa waamini walei kutamani kuwa Wakleri na Wakleri kudhani kwamba, wao ni watu wa mshahara katika maisha na utume wa Kanisa.

Waamini walei ni chachu muhimu sana ya utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kitamaduni, zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku! Waamini walei, wawe ni chachu ya utakatifu na mfano bora wa kuigwa katika masuala ya kisiasa; kiuchumi, kitamaduni na kiroho kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, daima wakiongozwa na dhamiri nyofu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, waamini walei ni wadau wakuu wa mchakato wa uinjilishaji unaotekelezwa na Kanisa kati ya watu wa Mataifa. Tunu msingi za Injili zinapaswa kuwa ni chachu ya mageuzi, maboresho na upyaisho katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, utume unaotekelezwa kwa dhati kabisa na waamini walei, hata kama Wakleri wanaweza kuchangia, lakini dhamana kubwa ni waamini walei! Ili kuwajengea uwezo waamini walei kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao, utakaowawezesha kutoka kifua mbele tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kuna haja ya kuwapatia majiundo makini na endelevu katika maisha na utume wao; kwa kuwawezesha kuwa na nyenzo msingi zitakazowasaidia kuinjilisha makundi ya watu katika jamii.

Makundi haya ni yale ya wataalam, wasomi na wanasiasa ambao kwa hakika ni changamoto kubwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa. Wataalam waliotalaumiwa katika taaluma mbali mbali wajengewe uwezo ili kuweza kuwainjilisha pia wataalam wenzao, kwa kuwajibika barabara mintarafu Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Waamini walei hawana haja ya kuwa ni Wakleri ili kuwainjilisha ndugu na jirani zao katika taaluma, bali mifano bora ya maisha inayofumbatwa katika chachu ya Injili inatosha kabisa. Sera na mikakati ya kichungaji haina budi kupyaishwa daima, kwa kusoma alama za nyakati na kumruhusu Roho Mtakatifu kutenda kazi yake barabara ndani ya Kanisa. Waamini walei wawajibike na kushirikiana na viongozi wa Kanisa katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakaza kusema, Parokia ni mahali panapoonesha umoja na mshikamano wa Kanisa; ni mahali panapowawezesha waamini walei pamoja na wakleri kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Vyama vya kitume vilivyoanzishwa mara tu baada ya Mataguso mkuu wa Pili wa Vatican ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa na ni msaada mkubwa kwa Parokia kukua na kukomaa katika utekelezaji wa wajibu na dhamana yake, tayari kutoka kifua mbele kwenda kuinjilisha hasa katika mambo msingi ya maisha ya binadamu. Waamini walei wawe ni “majembe” ya upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Lakini, wakumbuke kwamba, upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, unarutubishwa kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji! Kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, majirani zao waweze kuvutwa kumwendea Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia, tayari kuwasaidia kupyaisha maisha yao. Kwa kutekeleza haya yote, waamini walei wanawajibika kweli katika maisha na utume wa Kanisa, kinyume chake wanasema Maaskofu Katoliki Canada ni kupoteza dira na mwelekeo wa maisha! Ni kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kwa maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa mwamini mlei anajitafuta mwenyewe kwa ajili ya mafao yake binafsi.

Waamini walei kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, walisaidie Kanisa kutoka na kuwaendea watu wanaoishi pembezoni mwa jamii, vinginevyo, Kanisa litajikuta likijitafuta lenyewe. Kanisa liwe tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Furaha ya Injili. Waamini wanapaswa kuwajibika katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza: kwa utu na heshima ya binadamu; kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimamia na kutekeleza haki msingi za binadamu; kwa kujizatiti kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; Injili ya familia inayosmikwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Waamini walei wawajibike kulisaidia Kanisa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; kutetea na kudumisha haki zao msingi; vijana kupata fursa za masomo na kazi; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Waamini walei, wawe mstari wa mbele katika maisha ya sala kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Parokia, tayari kusimamia haki jamii, kwa kuwa ni mashuhuda wa faraja, matumaini, huruma na upendo wa Mungu kwa wale wote wanaoteseka. Changamoto hizi wanasema Maaskofu wa Canada ni wajibu na dhamana inayoweza kutekelezwa na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuwarejeshea watu utu na heshima yao kama binadamu! Waamini walei wajitahidi kuyafahamu Mafundisho Jamii ya Kanisa ili wasaidie kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, zinazopigwa “danadana” na wanasiasa mamboleo. Wawajibike kuwasindikiza wanafamilia wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha, kiasi hata cha kujikatia tamaa. Watambue kwamba, wazazi ni walezi wa kwanza wa watoto wao, jambo ambalo waamini walei wanapaswa kulivalia njuga mintarafu kanuni maadili na utu wema; maisha ya kiroh, malezi na makuzi bora ya watoto wao kadiri ya Mafundisho ya Kanisa.

Waamini walei walioko kwenye masuala ya siasa, wawe mstari wa mbele kupigania haki jamii, kusaidia kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki za wafungwa, ili wanapomaliza adhabu yao wawe ni watu bora zaidi, kuliko walivyoingia gerezani. Baraza la Maaskofu Katoliki linahitimisha barua yake nzito kwa waamini walei kwa kuwataka kuwajibika barabara katika maisha na utume wao kadiri ya wito, dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa utakatifu wa maisha!

Maaskofu Canada

 

13 August 2019, 14:18