Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam: Tafakari kuhusu: Wito, Ukuu, Utakatifu na maisha ya Kipadre. Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam: Tafakari kuhusu: Wito, Ukuu, Utakatifu na maisha ya Kipadre. 

Askofu mkuu Ruwa'ichi: Ukuu, Utakatifu, Wito & Maisha ya Upadre

Barua ya Papa Francisko kwa Mapadre Duniani kote aliyoiandika kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko duniani, inaweza kuwa tena ni fursa kwa Mapadre wenyewe pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao kutafakari kuhusu: wito, maisha, ukuu na utakatifu wa Upadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linaendelea kujitahidi kutafakari kwa kina na mapana kuhusu: Ukuu na utakatifu wa Fumbo la wito, maisha na utume wa Kipadre, ili kuweka bayana, thamani yake isiyoweza kupimika kwa mizani ya kibinadamu. Lengo ni: kulinda, kuhifadhi na kudumisha usafi na utakatifu wake kama wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Jambo la msingi kwa Mapadre ni kutambua kwamba, Kanisa linawahimiza kuwa kweli ni watumishi waaminifu, watakaomuakisi Kristo fukara, Kristo mtii na Kristo msafi katika useja! Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanazania katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara yalienda sanjari na Jubilei ya Miaka 100 ya Upadre nchini Tanzania, iliyoadhimishwa mwaka 2017.

Hii ilikuwa ni fursa kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kuweza kutafakari kuhusu: wito, maisha, utume, changamoto, vikwazo, ukuu na utakatifu wa Daraja ya Upadre katika maisha na utume wa Kanisa. Mapadre wanashiriki katika utume wa Kristo kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ilikuwa ni nafasi ya kuwakumbuka na kuwaombea mapadre wao neema, baraka, afya njema ya roho ya mwili, sanjari na kuwaombea ari, mwamko na furaha katika wito na maisha yao ya kipadre. Mapadre wanapaswa kukumbuka kwamba wao ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa linaloendelea kuhitaji watenda kazi: wema, watakatifu na wachamungu, kwa maneno mengine, mashuhuda wenye mvuto na mashiko kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya.

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre Duniani kote aliyoiandika kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko duniani, inaweza kuwa tena ni fursa  kwa Mapadre wenyewe pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Iwe ni nafasi tena ya: Kuangalia mateso na mahangaiko ya maisha na utume wa Mapadre ndani ya Kanisa. Iwe ni fursa ya kuwashukuru Mapadre kwa sadaka na majitoleo ya kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Iwe ni fursa ya kutoa neno la faraja kwa Mapadre wanaoendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, ili hatimaye, waweze kuona utukufu na ukuu wa Mungu unaofumbatwa katika Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu, kwa kumwangalia Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Mapadre Duniani, ilikuwa ni fursa kwa Mapadre wenyewe kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na wito wa Upadre. Kanisa linatambua kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache, basi, hii iwe ni fursa ya kuendelea kusali na kumwomba Bwana wa mavuno ili aweze kupeleka watenda kazi: wema, watakatifu, wachamungu na wachapakazi katika shamba lake. Kanisa liendelee kusali na kuomba ili lipate Mapadre watakaohudumia Majimbo mbali mbali, Mapadre watakaojiunga na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ili kuendelea kulipamba Kanisa la Mungu kwa karama za Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, amana na utajiri unaobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa lake.

Mapadre watumie muda wao kujitafakari kwa kumshukuru Mungu pale walipotenda kadiri ya mapenzi yake; wawe tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa kuomba msamaha pale walipoelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu, tayari kuanza upya kwa ari na moyo mkuu zaidi! Kwa vile Mapadre ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, basi iwe ni nafasi kwa familia ya Mungu katika ujumla wake kuangalia jinsi ambavyo inakuza na kudumisha umoja, upendo na mafungamano na Mapadre wake! Iangalie jinsi inavyotekeleza dhamana na wajibu wake katika utekelezaji wa sera, mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji. Iwe ni fursa ya kuangalia jinsi ambavyo familia ya Mungu inavyoendelea kujizatiti katika kuwaenzi, kuwaombea na kuwawezesha Mapadre ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu!

Askofu Mkuu Ruwa'ichi: Upadre
07 August 2019, 16:40