Askofu mkuu Gervas Nyaisonga anawataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kutumia karama na utajiri waliokirimiwa na Mungu kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo. Askofu mkuu Gervas Nyaisonga anawataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kutumia karama na utajiri waliokirimiwa na Mungu kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo. 

Askofu mkuu Nyaisonga: Tumieni karama & utajiri kutangaza Injili

Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie kufafanua: Imani ya Kanisa; viwaelimishe waamini kuhusu Sakramenti za Kanisa kama chemchemi ya neema na wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Viwaelimishe waamini kuhusu Amri za Mungu ambazo ni msingi wa kanuni maadili na utu wema; viwasaidie waamini kukuza na kudumisha utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha!

Na Thompson Mpanji, Mbeya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) hivi karibuni amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii pamoja na karama zao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mawasiliano yawawezeshe waamini kumfahamu, kumpenda, kumtumikia Mwenyezi Mungu ili hatimaye, siku moja waweze kufika mbingini, ili kufurahia maisha na uzima wa milele. Mawasiliano yawawezeshe waamini kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuachana na matendo maovu yanayochafua mahusiano na mafungamano kati ya Mungu na waja wake na badala yake, wajielekeze zaidi katika kutenda mema, kwa kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa.

Vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii kama vile: Luninga, Radio, Magazeti na Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu sana zinazoweza kutumiwa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza karama na mapaji yao na hatimaye, kuyatumia kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Askofu mkuu Nyaisonga ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uzinduzi wa Mbio za Mama Bikira Maria, Jimbo kuu la Mbeya, ili kuchangia huduma ya matangazo yanayotolewa na Radio Maria nchini Tanzania, Radio ambayo kwa sasa imejipambanua kuwa kweli ni sauti ya Kanisa kati ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Hii ni Radio ambayo inaonekana kupendwa na watu wengi, kiasi hata cha watu kuhamasika kuchangia kwa hali na mali ili iweze kuendeleza huduma yake ndani na nje ya Tanzania.

Askofu mkuu Nyaisonga amekazia umuhimu wa waamini kutumia vyema karama na mapaji waliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa sifa na utukufu wa Mungu, ustawi na maendeleo ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, kusudio la Mungu ni watu waweze kupata utimilifu wa maisha na hatimaye, uzima wa milele. Wamisionari waliopanda mbegu ya Ukristo Barani Afrika walitumia karama na mapaji yao ili kuhakikisha kwamba, wanatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati zao. Walisafiri na kutumia muda mrefu sana kwenda kutoa huduma vijijini, watu wakatubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao! Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania imekwisha gota sasa ni wakati wa kusoma alama za nyakati kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linatumia kikamilifu vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Waswahili wengi hawana utamaduni wa kujisomea vitabu vinavyouzwa na maduka ya vitabu vya Kanisa, lakini ni wepesi wa kuangalia Luninga na kusikiliza Radio kwani hii ni sehemu ya utamaduni wao, kumbe, Kanisa halina budi kuendelea kuwekeza katika vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kuhakikisha kwamba, watu wengi wanainjilishwa kadiri ya fursa zinavyoendelea kujitokeza. Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie kufafanua: Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na mambo ya nyakati.  Vyombo vya mawasiliano ya jamii, viwaelimishe waamini kuhusu Sakramenti za Kanisa kama chemchemi ya neema na wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Viwaelimishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema Amri za Mungu ambazo ni msingi wa kanuni maadili na utu wema.

Vyombo vya masiliano ya jamii, viwasaidie waamini kukuza na kudumisha utamaduni, ari na moyo wa sala. Kimsingi huu ni muhtasari wa Katekisimu ya Kanisa Katoliki inayopaswa kuendelea kufafanuliwa na wataalam mbali mbali kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii, kama sehemu ya malezi na majiundo awali na endelevu kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Vyombo vya mawasiliano ya  jamii viwe ni faraja kwa wagonjwa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Kila mwamini aguswe, ili aweze kusimama kidete, kuchangia katika ustawi na maendeleo ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa. Nguvu na jeuri yao inapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu ndiye anayepaswa kuabudiwa kuheshimiwa na kutukuzwa na wote kwani kwa njia ya Damu yake Azizi amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Waamini waendelee kujisadaka na kujinyima ili rasilimali fedha waliyokirimiwa na Mungu, iweze kusaidia katika kulitegemeza Kanisa kwa njia ya huduma makini ya mawasiliano ya jamii kwa watu wake. Rasilimali na utajiri vitumike kwa ajili ya kujenga na kudumisha mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii anasema Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga. Waamini wahamasike na kusimama kidete ili kutegemeza vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa nchini Tanzania, lakini kwa namna ya pekee Radio Maria ambayo imeendelewa kutoa huduma ya kitaifa kwa kuwashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema matangazo yake. Kila mtu achangie kadiri ya uwezo na fursa zake, ili kumtangaza na kumshuhudia Mungu asili na chemchemi ya karama, mali na utajiri alionao mwanadamu!

Radio Maria
03 August 2019, 16:33