Tafuta

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma amewataka WAWATA kuwa ni vyombo vya uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa utakatifu wa maisha. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma amewataka WAWATA kuwa ni vyombo vya uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa utakatifu wa maisha. 

WAWATA Jimbo kuu la Dodoma: Uinjilishaji, Utakatifu na Kujitegemea

Utume wa waamini walei katika mchakato wa kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu unawawajibisha kuhakikisha kwamba, nuru ya maisha yao inaangaza ili watu wengine wanapoyaona matendo yao mema, waweze kumtukuza Mwenyezi Mungu, wakitambua kwamba, upendo wa Kristo unawabidisha. Lazima wawe ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Rodrick Minja, Dodoma & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, katika mkutano wake mkuu uliofanyika mjini Dakar, Senegal kuanzia tarehe 15-22 Oktoba 2018, uliazimia kutekeleza mambo makuu manne katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2022. Mosi ni kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Pili, ni kusimama kidete kulinda, kudumisha na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Tatu ni wanawake kuhakikisha kwamba, wanachuchumilia utakatifu wa maisha. Nne ni kuhakikisha kwamba, utume wa wanawake Wakatoliki unaendelezwa ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wa maisha adili, matakatifu na manyoofu.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania, hivi karibuni, katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Seminari ndogo ya Mtakatifu Augustino, Bihawana Jimbo kuu la Dodoma, ameitaka Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Dodoma kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Wawata wawe ni mfano bora wa kuigwa na majirani zao, na hasa wale ambao wamelipatia Kanisa kisogo kwa sababu mbali mbali, ili waweze kuwashika mkono tena na kuwashirikisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kuna baadhi ya Wanawake Wakatoliki wamezama sana katika shughuli za kiofisi, biashara pamoja na maisha ya kijamii, kiasi kwamba, wamesahau kuboresha pia sehemu ya maisha yao ya kiroho. Hawa ni wanawake ambao hawashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, vikao vya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo pamoja na matukio mbali mbali ya Kanisa.

Kwa wanawake wa namna hii hata ushiriki wao kwenye Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki ni mdogo. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahimiza waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Utume wao unapata chimbuko kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo. Kwa njia hii, waamini walei wataweza kushiriki katika mchakato wa kueneza Ufalme wa Mungu pamoja na kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Wanawake Wakatoliki pamoja na kuchuchumilia utakatifu wa maisha, wanapaswa pia kuwa ni wadau katika uinjilishaji na mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa kupandikiza roho ya Injili, utu wema na utakatifu.

Ushiriki wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki katika Mafumbo ya Kanisa, uwasaidie kuboresha maisha yao ya kiroho, tayari kujisadaka na kuwajibika barabara kadiri ya upendo wa Kristo unavyowawajibisha! Karama na mapaji mbali mbali waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Waamini walei katika ujumla wao wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya imani, matumaini na mapendo; daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Fadhila, karama na mapaji haya yawe ni msingi wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu kwa kukazia: ukweli, ukarimu, moyo na imani thabiti. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa daima awe mbele ya wanawake mfano bora wa kuigwa.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya anaendelea kufafanua kwamba, utume wa waamini walei katika mchakato wa kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu unawawajibisha kuhakikisha kwamba, nuru ya maisha yao inaangaza ili watu wengine wanapoyaona matendo yao mema, waweze kumtukuza Mwenyezi Mungu, wakitambua kwamba, upendo wa Kristo unawabidisha. Lazima wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaozinyemelea familia nyingi Barani Afrika. Utamaduni wa kifo unakumbatiwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba sanjari na matumizi ya vizuia mimba mambo ambayo ni hatari sana kwa Injili ya uhai. Ni wajibu na dhamana ya Wawata kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai inayokita mizizi yake katika maisha ya ndoa na familia!

Wazazi na walezi wanapaswa kuwa karibu sana na watoto pamoja na vijana wao, ili kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwapatia mang’amuzi ya maisha kadiri ya tunu msingi za Kiinjili! Vinginevyo, wazazi na walezi watashangaa kuona na kusikia yale yanayotendwa na watoto wao! Wazazi wawe washauri makini na kamwe wasifanye mzaha na malezi pamoja na makuzi ya watoto wao, kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa.

Kumbe, Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre ambayo yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewataka Majandokasisi Seminari ya Bihawana kutambua na kuthamini wito wao na kwamba, wanapaswa kuwa ni kioo cha vijana wengine ndani na nje ya Jimbo kuu la Dodoma. Wawe ni vijana wenye heshima, adabu na maadili mema kati yao wenyewe kama Majandokasisi, mbele ya walezi na jamii inayowazunguka. Waseminari wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kuzingatia ushauri wanaopewa na wazazi pamoja na walezi wao. Waepukane na kiburi kwa sababu ni kaburi la maisha na utu wao kwa sasa na kwa siku za usoni. Waseminari wajenge ari na moyo wa kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa, ili kweli waweze kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu hata katika kipindi hiki cha malezi na makuzi. Waseminari anasema Askofu mkuu Kinyaiya, wasikubali kukaa kaa kihasara hasara!

Majandokasisi wawe ni dira na mwongozo wa kufuatwa na vijana wenzao na kwa njia hii, hata wao watakuwa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma ameishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Dodoma kwa sadaka na majitoleo yao katika mchakato mzima wa kuitegemeza Seminari Ndogo ya Mtakatifu Augustino, Bihawana, Dodoma.

Jimbo Kuu la Dodoma
31 August 2019, 11:55