AMECEA ina thamini sana mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika maisha na utume wa Kanisa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. AMECEA ina thamini sana mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika maisha na utume wa Kanisa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. 

AMECEA ina thamini mchango wa vyombo vya mawasiliano ya jamii

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA linasema kwamba, kinataka kuendelea kuwajengea na kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari za Kanisa ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa: kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji zaidi ili kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii kupitia njia za mawasiliano ya jamii.

Na Sarah Pelaji, Nairobi, Kenya & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, katika maadhimisho ya mkutano wake mkuu wa 19 kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia, ulioongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”, ilikuwa ni changamoto na mwaliko kwa watu wote wa Mungu katika nchi za AMECEA, kuhakikisha kwamba, wanakumbatia na kuambata tofauti hizi kama sehemu ya amana, utajiri na urithi unaowaunganisha na kamwe, zisiwe ni chanzo cha mafarakano na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini. Hivi karibuni, waandishi wa habari kutoka Ukanda wa AMECEA walifundwa juu ya uandaaji wa habari, kusambaza na kuzishirikisha habari hizi katika ulimwengu wa teknolojia na maendeleo ya sayansi ya mawasiliano ya jamii.

Lengo likiwa ni kuendelea kuwajengea na kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari za Kanisa ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa: kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji zaidi ili kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii kupitia njia za mawasiliano ya jamii. Askofu mkuu Philip Anyolo, Mwenyekiti wa kurugenzi ya mawasiliano AMECEA ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amesema, katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati na kuhakikisha kwamba, linatumia kikamilifu njia za mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha, dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa kikamilifu na  waandishi wa habari za Kanisa.

Maandiko Matakatifu ni kielelezo makini cha mawasiliano kati ya Mungu na waja wake, ili kuwaweka kuwa karibu zaidi naye. Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwasiliana na watu wake kwa njia ya Neno, matukio na historia mbali mbali za maisha. Vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinapaswa kuliunganisha Kanisa na walimwengu, ili kuvitakatifuza vyombo hivi, viweze kuwa ni chachu ya umoja, upendo na mshikamano kati ya watu! Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa havina budi kuwa na mwelekeo chanya zaidi katika kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, haki, amani na maridhiano kati ya watu; utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa msukumo wa pekee. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa waandishi wa habari kujiendeleza zaidi katika taaluma pamoja na kujenga mahusiano ya karibu na wakleri, watawa, makatekista na waamini walei, kwani hawa ni sehemu ya habari na walengwa wakuu wa habari za Kanisa.

Waandishi wa habari za Kanisa wao ni sauti ya Kanisa na wanyonge ndani ya jamii, kumbe wanapaswa kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Padre Anthony Makunde, Katibu mkuu wa AMECEA aliwakumbusha kwamba, mafunzo haya yalikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Maazimio ya AMECEA katika mkutano wake wa 19 uliofanyika mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Mababa wa AMECEA walizitaka kurugenzi za Mawasiliano ya Jamii kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoki Afrika Mashariki na kati kutoa taarifa kuhusu maisha na utume wa Kanisa katika nchi na majimbo yao. Kurugenzi ya mawasiliano katika nchi za AMECEA imekuwa ni kiungo muhimu sana cha mawasiliano ndani na nje ya nchi za AMECEA. Kurugenzi hii anasema Padre Makunde inaonekana kuwa na nguvu zaidi, ikilinganishwa na Kanda nyingine za Kanisa Barani Afrika.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Maaskofu wanathamini mchango wa mawasiliano ya jamii katika maisha na utume wa Kanisa! Waandishi wa habari za Kanisa, wawe wakweli na waaminifu wanapoandika kuhusu historia, mila, desturi na tamaduni za Kiafrika. Wawajulishe watu wa Mataifa kazi na utume unaotekelezwa na Mama Kanisa Barani Afrika. Mababa wa AMECEA katika mkutano wao wa 19 huko Ethiopia walisema tofauti msingi zinazopatikana kati ya watu zimo katika mpango wa Mungu anayetaka kila mtu apokee kile anachohitaji, kwa lengo la kushirikishana, kutajirishana na kukamilishana. Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wamekirimiwa akili na utashi; wana hali na asili moja na hivyo wana hadhi sawa! Mababa wa AMECEA wanaitaka familia ya Mungu kuwa ni shuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo na kamwe wasikubali kupekenyuliwa na ukabila, udini, umajimbo wala na tofauti msingi zinazojitokeza kati yao!

Hadhi sawa inafumbatwa katika usawa wa binadamu pamoja na haki jamii kama wanavyofafanua Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wamekombolewa kwa njia Fumbo la Pasaka. Haki na usawa ni mambo msingi katika kudumisha mafungamano ya kijamii. Lakini, Mababa wa Mtaguso wanakaza kusema, uwepo wa tofauti kubwa za kiuchumi na kijamii kati ya wanajamii na kati ya mataifa ya familia ya Mungu iliyo moja katika ubindamu ni kunasababisha taksiri, au kikwazo. Hali hii inapingana na  na haki jamii, usawa na hadhi ya binadamu pamoja na amani duniani. Maendeleo endelevu na fungamani yanapaswa kujikita katika ustawi na mafao ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwezeshwa na taasisi za Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa, yalenge mafao ya wengi; kwa kuratibiwa na kusimamiwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Mababa wa AMECEA wanakaza kusema, wataendelea kusimama kidete kulinda na kutetea tofauti mtetemo, hadhi sawa, umoja wa amani na maendeleo fungamani katika Ukanda wa AMECEA. Kanisa litaendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani, haki na usawa miongoni mwa familia ya Mungu pamoja na kusimamia maendeleo fungamani na haki msingi za binadamu. AMECEA inaitaka Sudan ya Kusini kuharakisha mchakato wa kutafuta suluhu ya amani, ili kuwaondolea watu mateso kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe na kwamba, AMECEA iko tayari kushiriki katika kutafuta suluhu ya kudumu. Waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani Sudan ya Kusini. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Umaskini, kiwango kikubwa cha ukosefu wa fursa za ajira, pengo kubwa kati ya maskini na matajiri ni kati ya changamoto zinazoendelea kuzikumba familia nyingi, Afrika Mashariki na Kati. Malezi na majiundo ya awali na endelevu yataendelea kupewa kipaumbele cha pekee na AMECEA kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kukuza na kudumisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa familia katika ngazi mbali mbali. Mawasiliano katika ulimwengu wa digitali yaiwezeshe AMECEA kuendelea kushirikiana na kushikamana na wadau mbali mbali katika tasnia ya mawasiliano ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kanisa liendelee kuwekeza kikamilifu katika vyombo vya mawasiliano ya jamii kama sehemu ya uinjilishaji na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Wadau wa tasnia ya habari wawajibike, waaminike na kuwa makini katika mawasiliano ya jamii. AMECEA itaendelea kujizatiti katika malezi, makuzi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya, kwa kukazia: imani, wito, mang’amuzi, maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu pamoja na elimu makini.  Kanisa litaendelea kuzivalia njuga changamoto za maisha ya vijana kama vile: Ukosefu wa fursa za ajira, umoja katika amani, maendeleo ya uongozi, maongozi ya maisha ya kiroho pamoja na kuwasindikiza vijana kuweza kufanya maamuzi mazito katika maisha yao!

AMECEA: Mawasiliano
03 August 2019, 15:45