Maaskofu wa Zambia wakiwa katika Kanisa Kuu la Mtoto Yesu pamoja na Balozi wa kitume wa Zambia na Malawi Askofu Mkuu Gianfranco Gallone Maaskofu wa Zambia wakiwa katika Kanisa Kuu la Mtoto Yesu pamoja na Balozi wa kitume wa Zambia na Malawi Askofu Mkuu Gianfranco Gallone  

ZAMBIA:Maono ya Mtakatifu Paulo VI kwa Kanisa la Afrika

Rais wa Baraza la Maaskofu Zambia amehimiza nchini Zambia kuwa igeuke kuwa Kanisa la dhati la kimisionari.Amethibitisha hayo tarehe 13 Julai 2019 katika Kanisa Kuu Katoliki la Chipata wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya maadhimisho ya Mwezi Maalum wa kimisionari Oktoba 2019. Mwezi huo utaongozwa na kaulimbiu “Mmebatizwa na kutumwa:Kanisa la Kristo katika utume.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katika Kanisa Kuu katoliki la Chipata nchini Zambia, Askofu George Zumaile Lungu Rais wa Baraza la maaskofu nchini Zambia (Zccb) amesema, nchini Zambia sasa iwe Kanisa la kimisionari la dhati katika kutimiza maono ya Mtakatifu  Paulo VI,  kuhusu suala la Kanisa la Kimisionaria la Afrika. Amesema hayo wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya shughuli za Mwezi maalum wa Kimisionari Oktoba 2019. Ni uzinduzi uliofanyika tarehe 13 Julai 2019. Kauli mbiu ya mwezi huo itakuwa ni “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. Lengo la mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 ni kutaka kukazia uhamasishaji wa nguvu na mwamko wa kimisionari katika kila nyanja zote za utume wa kimisionari.

Maono ya Mtakatifu Paulo VI  kuhusu Kanisa la Afrika

Askofu Lungu amesema Mtakatifu Paulo VI alipoitembelea Afrika na  kuwatangaza wafiadini nchini Uganda, alikabidhi Kanisa la Afrika ili liweze kuwa  na wamisionari wake wenyewe. Na hiyo ndiyo changamoto ambayo bado ipo, amesema Askofu kwa mujibu wa maelezo kutoka Shirika la Habari Cisa.  Akiendelea kukumbuka tamko la Mtakatifu Paulo VI wakati wa kutembelea Uganda kunako mwaka 1969, Askofu Lungu amesema kuwa ndoto ya Mtakatifu Papa Paulo VI ilikuwa kwamba Kanisa la Afrika na kwa namna ya pekee hata Zambia liweze kutoa mapadre wake wenyewe, watawa wake, hata waamini walei kwa ajili ya utume wa Kanisa ndani  ya nchi na  katika sehemu nyingine za utume wa kimisionari.

Ikumbukwe  pia katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Uganda imebahatika  kutembelewa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1969,  Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1993 na Baba Mtakatifu Francisko 2015. Mtakatifu Paulo VI alitembelea Uganda ili kutoa heshima zake kwa mashuhuda wa imani 22 waliotoa maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Akiwa huko alisema kwamba, mashuhuda wa imani ni watu ambao wamelipatia heshima kubwa Bara la Afrika, kielelezo makini cha upendo na huruma ya Mungu inayokita ndani ya Fumbo la Msalaba!

Waamini wawe wa dhati katika kutoa ushuhuda wa Injili

Hata hivyo naye  Balozi wa Vatican nchini Zambia na Malawi, Askofu Mkuu Gianfranco Gallone wakati wa kutoa neno  lake wakati wa shughuli ya uzinduzi huo amewashauri waamini wote wawe wa dhati hasa katika  kutoa ushuhuda wa Injili na  kwa namna ya kuwa wanyoofu katika maisha ya watu. “Sisi sote ni wafuasi wa Yesu na tunaalikwa kutofikiria kuwa sisi ni watawala binafsi wa imani za wengine” na sisi ni watumishi kwa ajili ya upendo wa Yesu”, amesisitiza Balozi wa Vatican nchini Zambia na Malawi Askofu Mkuu Gallone. Kufuatia na mpango maandalizi ya maadhimisho ya mwezi Maalum wa Kimisionari Oktoba 2019 na  ambao unaongozwa na Kauli mbiu “tumebatizwa na Kutumwa”, kwa upande wa Zambia taarifa zainasema kuwa wanatarajia kuandaa kwanza  kimajimbo nchini Zambia kabla ya  kuwa tukio  kubwa la kitaifa Mwezi Oktoba 2019!

19 July 2019, 15:00