Tafuta

Vatican News
Mheshimiwa Padre Perfect Leiya, C.PP.S. amechaguliwa kuwa Mkuu mpya wa Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania. Mheshimiwa Padre Perfect Leiya, C.PP.S. amechaguliwa kuwa Mkuu mpya wa Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania.  (Vatican Media)

Padre Perfect Leiya achaguliwa kuongoza C.PP.S. Tanzania

Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania limemchagu Mheshimiwa Padre Perfect Leiya kuwa Mkuu wa Shirika wa Kanda, Padre Vedasto Ngowi, Makamu mkuu wa Shirika, Padre Felix Mushobozi kuwa Katibu mkuu, Padre Dominic Mwaliko kuwa Mtunza hazina na Padre Greyson John Msengi kuwa Mshauri. Ndoto ya Mtakatifu Gaspar inaendelea kuchanja mbuga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ndiye amani ya dunia.  Kwa hakika amani duniani inajengeka katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru na kwamba Kristo Yesu ndiye chemchemi ya amani ya Kimasiha duniani. Kristo Yesu kwa kumwaga Damu yake Azizi, ameharibu ndani yake uadui na hivyo amewapatanisha watu na Mungu na amelifanya Kanisa lake kuwa ni Sakramenti ya umoja wa ubinadamu na ya umoja wake na Mungu. Wale wote wanaopewa dhamana na wajibu wa kuongoza, wanahimizwa na Mama Kanisa kujishughulisha kwa ajili ya ustawi wa watu wanaowaongoza; kutenda kwa hekima na haki; kulinda na kuleta umoja na mshikamano; kustawisha amani, utu na heshima ya watu wao.

Maandiko Matakatifu yanamweka Kristo Yesu kama mfano bora ambao viongozi wote watajifunza namna ya kuyatimiza hayo. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alishughulikia mahitaji halisi ya watu wake, aliwajali, aliunganisha makundi yasiyopatana na akajitoa sadaka Msalabani ili kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu ni mfalme wa kweli na uzima; Mfalme wa utakatifu na neema; ni Mfalme wa haki, upendo na amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa hakika Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujengeka na kumshuhudia Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu.

Viongozi wa Kanisa waoneshe dira na njia ya kufuata kwa mfano na ushuhuda wa maisha yao. Ni hatari ikiwa kama viongozi wa Kanisa watageuka kuwa ni “Mbwa mwitu” na kuanza kumezwa na malimwengu kwa kutafuta madaraka, fedha na mali. Hizi ni dhambi kuu zinazowaandama Makleri katika maisha na utume wao! Waamini si rahisi sana kumsamehe kiongozi wa Kanisa mwenye uchu wa mali na fedha kwa mafao yake binafsi! Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kuanzia tarehe 8-12 Julai 2019 wamekuwa wakiadhimisha Mkutano Mkuu wa Shirika. Hii imekuwa ni nafasi ya kutafakari kwa kuangalia dira na vipaumbele vya Shirika nchini Tanzania katika kipindi cha Miaka 4 ijayo kuanzia sasa na hatimaye, kuangalia wanashirika wanaoweza kupeperusha bendera hii kwa muda wa miaka minne kuanzia sasa!

Baada ya kusali na kutafakari sana, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, wamemchagua Mheshimiwa Padre Perfecr Leiya kuwa ni Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Kabla ya uchaguzi huu Padre Leiya alikuwa ni Paroko katika Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Chibumagwa, Jimbo Katoliki la Singida. Katika safu mpya ya uongozi, Padre Vedasto Ngowi amechaguliwa kuwa Makamu Mkuu wa Shirika. Padre Felix Mushobozi amechaguliwa kuwa ni Katibu mkuu wa Shirika. Itakumbukwa kwamba, Padre Mushobozi aliwahi pia kuwa Katibu mkuu wa Kanda ya Tanzania na Katibu mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi Duniani na kabla ya kuchaguliwa kwake, alikuwa ni Afisa katika Idara ya Haki na Amani ya Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, yenye Makao yake Makuu mjini Roma. Padre Dominic Mwaliko amechaguliwa kuwa ni Mweka hazina wa Shirika na Padre Greyson John Msengi amechaguliwa kuwa ni Mshauri katika uongozi mpya! Wanashirika wanawashukuru viongozi waliomaliza muda wao chini ya Padre Chesco Peter Msaga! Ndoto ya Mtakatifu Gaspar inaendelea kuchanja mbuga!

Uchaguzi Tanzania
12 July 2019, 10:42