Tafuta

Vatican News
Nabii Eliya anaheshimika sana katika Maandiko Matakatifu pamoja na Mapokeo ya Kanisa, kama mtu wa imani, matumaini na mapendo! Nabii Eliya anaheshimika sana katika Maandiko Matakatifu pamoja na Mapokeo ya Kanisa, kama mtu wa imani, matumaini na mapendo! 

Kumbu kumbu ya Nabii Eliya: Mtu wa haki, imani na mpatanishi!

Nabii Eliya anatambulikana kuwa ni mtu wa imani, matumaini na mapendo sanjari na shuhuda wa uwepo wa Mungu. Huyu ni Nabii wa haki, imara katika kutetea ukweli, Eliya mtu mwenye ari, shauku, motomoto, kiu ya kumjua, kumpenda, kumtumikia na kuishi na Mungu milele. Kama asemavyo mzaburi “kama vile mwenye kiu anavyoyatamani maji, roho yangu yatamani kuwa nawe".

Na Sr. Veronica Silvester Buganga, CMTBG - Roma.

Nabii Eliya katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa, anatambulika kama Mtu wa imani, matumaini na mapendo kwa  Mungu, shuhuda wa uwepo wa Mungu. Huyu ni Nabii wa haki, imara katika kutetea ukweli, Eliya mtu mwenye ari, shauku, motomoto, kiu ya kumjua, kumpenda, kumtumikia na kuishi na Mungu milele. Kama asemavyo mzaburi “kama vile mwenye kiu anavyoyatamani maji, roho yangu yatamani kuwa nawe milele”. Hata katika magumu, mateso, machungu ya maisha na utume wake, ameonja uwepo na msaada wa Mungu ( 1Wafalme 19:5-8) Eliya ni nabii mpatanishi: Eliya alikuwa amejawa na kuongozwa na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akawaombea wongofu wana wa israeli na kuwapatanisha na Mungu, kama tunavyoelezwa katika kitabu cha Kwanza cha Wafalme  sura ya 18, akapambana na uovu na kulikomboa taifa la Israeli katika imani potovu ya kuabudu miungu mingine, yaani walikuwa “viluka njia wa imani” hali hii ya kukosa uaminifu kwa Mungu ilimsononesha Nabii Eliya na kuhakikisha  Waisraeli wanamwamini na kumrudia Mungu mmoja.

Nabii Eliya, Mlima Karmeli na katika Kanisa: Karmeli ni mlima wenye uzuri asilia wa uoto na maua yenye harufu nzuri, mazingira yalimsaidia  Nabii Eliya kuishi maisha ya Taamuli. Wakarmeli walivutwa na Nabii Eliya katika tunu msingi alizojaliwa na Mwenyezi Mngu, hata mahujaji  wengi wa kipindi kile ambao walikuwa wakiitembelea Nchi Takatifu walikuwa wakiguswa na maisha yake. Wengi wao waliokuwa wakienda kuhiji Nchi Takatifu walikuwa wakifika pia mlima Karmeli sehemu ambayo Eliya aliishi maisha ya kieremiti. Wakarmeli waliishi mlima Karmeli karibu na chemchemi ya Eliya wakitamani kuwa kama yeye. Walimchagua Eliya “mtu wa jangwa” kuwa kama baba yao na kiongozi wao wa kiroho. Eliya alikuwa ni mtu wa sala na aliishi katika uwepo wa Mungu akimtumikia kwa uaminifu mkubwa.

Hata pale wana wa Israeli walipokengeuka na kutopea katika dhambi, yeye alisimama imara akiitetea imani halisi ya Israeli, imani kwa Mungu mmoja na kuonesha nguvu ya sala Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, waonyeshe watu leo hii kwamba wewe ndiwe Mungu wa Israeli na kwamba mimi ni mtumishi wako, nimefanya mambo haya kwa amri yako. Unijibu ee Mwenyezi Mungu ili watu wajue kuwa wewe ndiwe Mungu Mwenyezi na kwamba umeigeuza mioyo yao wakurudie” (1 Fal 18, 36-37). Kwa maisha yake Eliya anamfundisha kila mmoja wetu jinsi ya kuishi kwa vitendo upendo na imani kwa Mungu Muumbaji na Mkombozi. Alipochagua kuishi maisha ya kipweke, ni wazi alikuwa akimfundisha kila mtu njia sahihi ya kuzitawala tamaa za kimwili kwa ajili ya kuwa na moyo safi.

Eliya aliishi maisha ya kifukara, maisha ya kijangwa, maisha ya kipweke kwa utakatifu wa wazi ulioonekana kwa watu wote (Soma YsB 48:1-11). Kutokana na maisha yake ya kimonaki, anaheshimiwa sana na mababa wengi wa kimonaki ambao wanamwona kuwa yeye ndiye “mwanzilishi” wa maisha hayo. Makuu ya Mungu kupia Eliya: Mungu amejitukuza kupitia Nabii Eliya katika mambo mengi yanayotusaidia kukua kiimani  na kumtumainia Mungu katika maisha yetu, Elia amemfufua mtoto wa mama mjane, 1 Waf. 17:17.., unga na mafuta ya mama mjane hayakupungua. Ameomba mnvua ikanyesha baada ya ukame wa miaka (Anaamuru kwa nguvu ya Mungu). (1 Waf. 18: 41-46), ameishinda vita ya imani alipopambana na manabii wa Baali. Alisikia sauti ya Mungu na kuongea naye na kuelekezwa namna ya kutenda.

Tunamwomba Mungu atuunde na kututumia kama: mashuhuda, vyombo, mifereji, mito ya neema kwa maombezi ya Nabii Eliya tunaemwadhimisha kila tarehe 20 Julai na tunayemsoma na kumtafakari katika Maandiko Mataatifu. Tujaliwe uwezo wa kuongea na Mungu, kunena Neno lake, nguvu ya kuonya, kukemea mabaya, kuwapatanisha watu kati yao na Mungu na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha. Tunapaswa kuwa mashuhuda wa ukuu wa Mwenyezi Mungu. Kipawa cha utetezi wa wanyonge, kuwa manabii wa nyakati zetu, uwezo wa kuthubutu kuwa mashuhuda wa haki, ukweli, kuonja na kushuhudia uwepo wa Mungu alie hai, Mungu wa amani kama yanavyosema Maandiko Matakatifu. Ulipita upepo mkali uliovunja milima Mungu hakuwa humo, kukawa tetemeko la ardhi Mungu hakuwa humo… bali katika  sauti ndogo tulivu ya upepo mwanana Elia aliisikia sauti ya Mungu  “unafanya nini hapa?”( 1 Wafame 19, 11-14).

19 July 2019, 15:06