Tafuta

Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Kimataifa: Ukahaba si biashara hata kidogo linasema Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina. Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Kimataifa: Ukahaba si biashara hata kidogo linasema Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina. 

Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Kimataifa 2019

Biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo ni kati ya madonda makubwa yanayoendelea kunyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Nchini Argentina, mapambano haya yalianzishwa mwaka 2013. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linaendelea kuwahamasisha watu kusimama kidete kupinga biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2019 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Duniani. Hii ni siku maalum iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za kimataifa za kuragibisha athari za biashara hii katika maisha na utu wa binadamu. Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Shirika la Kazi Duniani, ILO, katika taarifa yake kwa mwaka 2018 linasema kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 45 ambao wameathirika kutokana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Mapungufu makubwa katika sheria ili kudhibiti uhalifu huu, adhabu ndogo inayotolewa pamoja na baadhi ya watu kutofahamu madhara ya biashara, hizi ni kati ya changamoto ambazo zimebainishwa na wanaharakati dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo!

Kashfa hii imeanza kuzoeleka kati ya watu, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni jambo la kawaida katika maisha. Lakini, huu ni ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Takwimu zinaonesha kwamba, hii ni biashara inayozalisha zaidi ya bilioni 150 kwa mwaka kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Biashara hii ni janga na donda ndugu kwa utu na heshima ya binadamu, inapaswa kufikia ukomo, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kamwe mwili wake si bidhaa ya kuuzwa au kununuliwa kama bidhaa sokoni. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Duniani linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusikiliza na kujibu kilio cha wanawake na wasichana wanaoteseka kutokana na kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Siku hii iwe ni nafasi ya kushirikishana kuhusu ukubwa wa tatizo, changamoto zilizoko na mbinu mkakati wa kupambana na biashara hii ambayo ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Vyombo vya ulinzi na usalama vishirikiane ili kudhibiti uhalifu huu wa kimataifa, ili kuweza kupata matokeo chanya na yale yanayodumu. Biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo ni kati ya madonda makubwa yanayoendelea kunyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Nchini Argentina, mapambano haya yameanza kushika kasi tangu mwaka 2013. Na kila mwaka, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linaendelea kuwahamasisha watu kusimama kidete kupinga biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu 2019 nchini Argentina inasema, “Ukahaba si kazi”. Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipokuwa anahutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati katika kupambana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mapambano haya lazima kwanza kabisa yalinde na kuheshimu: utu na haki msingi za binadamu. Pili ni kwa kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato na tatu ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vatican daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na biashara haramu ya binadamu ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuridhia Itifaki ya Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwani ni biashara inayowanyanyasa watu wengi zaidi. Ndiyo maana Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliwataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha utashi wa kisiasa katika mapambano haya.

Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake mbali mbali limeendelea kujipambanua kuwa ni kati ya wadau wakuu wanaopambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kuwasaidia waathirika ili waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida. Utumwa mamboleo unaendelea kukua na kukomaa, kumbe, unahitaji watu kulitambua hilo na kuchukua hatua madhubuti, hii ikiwa ni pamoja na kubadili mtindo wa maisha. Ikumbukwe kwamba, mafanikio katika maisha yanapatikana kwa juhudi na maarifa, kwa kujinyima na kujiwekea malengo thabiti. Serikali mbali mbali zinapaswa pia kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuwapatia mahitaji msingi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ndiyo maana kunako mwaka 2015 alipokuwa anazungumza na mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali mjini Vatican aliwataka kuhakikisha kwamba, wanasaidia katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Kikundi cha Mtakatifu Martha kilianzishwa katika jitihada hizi za Baba Mtakatifu Francisko kuwahusisha wadau mbali mbali katika mapambano haya dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo! Baba Mtakatifu hivi karibuni akizungumza na wajumbe wa RENATE, yaani Mtandao wa Mashirika ya Kitawa Kimataifa katika Mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu alikaza kusema, utumwa mamboleo ni matokeo ya umaskini, ukosefu wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; ubaguzi na ukosefu wa elimu, fursa za ajira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, hata utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya utumwa mamboleo na kwamba, huu ni utashi wa kimaadili unaopaswa kufanyiwa kazi na wadau mbali mbali duniani.

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na kashfa ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo, alianzisha Siku ya Kupambana na Biashara ya binadamu na Utumwa Mamboleo ndani ya Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tangu wakati huo, tarehe 8 Februari, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josephine Bakhita, aliyetekwa nyara kutoka Sudan, akakombolewa na hatimaye, akabatizwa na kuwa mtawa!

Papa: Utumwa

 

30 July 2019, 14:58