Vatican News
Mama Kanisa anawaalika waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa wakleri ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mama Kanisa anawaalika waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa wakleri ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.  (Vatican Media)

Endeleeni kuombea toba, wongofu na utakatifu wa Wakleri duniani!

Kardinali Vincent Gerard Nichols, katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, amewataka Wakleri kuwa ni chemchemi na mashuhuda wa Injili ya furaha; wajiaminishe katika huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wao. Na watambue kwamba wao ni wamisionari mapadre na kamwe si wakleri wafanyakazi waliobobea katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 alitamka kwamba, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ukumbusho kwamba, Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa watu! Mapadre ni wahudumu wa Neno, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Ni katika mukadha huu, Kardinali Vincent Gerard Nichols, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Westminster ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, amewataka Wakleri kuwa ni chemchemi na mashuhuda wa Injili ya furaha; wajiaminishe katika huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wao. Na watambue kwamba wao ni wamisionari mapadre na kamwe si wakleri wafanyakazi waliobobea katika maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya Miaka 450 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Douai, ambacho kimekuwa ni kitovu cha malezi na majiundo awali na endelevu ya wakleri nchini Uingereza na Walles. Kardinal Nichols amewakumbusha Wakleri kwamba, wameitwa na kuteuliwa na Mwenyezi Mungu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba wanakuza na kudumisha upendo wao kwa Kristo na Kanisa lake, kwani hadi sasa wamempenda kidogo sana, ikilinganishwa na upendo wa Kristo Yesu kwa ajili yao. Jambo la kwanza, Kanisa linapoombea toba, wongofu na utakatifu, Mapadre wenyewe wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha kwa kushirikishwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu katika kazi ya ukombozi, ili waweze kuwagawia watu wa Mungu mafumbo ya Kanisa. Mapadre wawe makini ili wasitumbukie katika hali ya kukata na kukatishwa tamaa, kiasi hata cha kuzama katika upweke hasi na kuanza kuogelea katika ugonjwa wa sonona na madhara yake ni makubwa kwa mapadre wenyewe hata kwa waamini wanaowahudumia.

Mapadre wawe makini katika matumizi ya rasilimali muda, wawe ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa watu waliokata tamaa na kwamba, yote haya yapate mwanzo na hatima yake kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya: Maisha ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Jambo la Pili, Kardinali Nichols anasema, Mapadre wasiwe na jambo lolote lile la kujivunia wala kujisifu mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia ya Kristo Yesu ambaye alifanywa kwao hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa: Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana. (Rej. 1Wakor. 1: 29-31). Kama walivyokuja hapa duniani, ndivyo watakavyorejea udongoni, siku watakapokuwa wameitwa na Mwenyezi Mungu! Kumbe, jambo la msingi ni kujikabidhi na kujiaminisha katika huruma na upendo wa Mungu. Sheria, kanuni na taratibu za maisha ni nyenzo msingi katika kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha na kamwe si kikwazo cha uhuru wa Wakleri.

Mapadre wajenge na kudumisha urafiki, uhusiano na mafungamano ya dhati na wakleri wenzao pamoja na waamini wanaowahudumia, ili kushirikishana: imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waendelee kuboresha uhai wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Jambo la tatu anasema Kardinali Nichols watambue kwamba, wao ni wamisionari mapadre na kamwe si wakleri wafanyakazi waliobobea katika maisha na utume wa Kanisa. Kama wamisionari mapadre, wanatumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili  kwa wagonjwa hospitalini na majumbani, kwa watoto wa mafundisho ya dini shuleni bila kuwasahau wakatekumeni wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa. Huduma kwa makundi yote haya isitolewe kwa mazoea! Mapadre watekeleze dhamana, wito na utume wao kwa upole na unyenyekevu mkuu; kwa hekima na busara; kwa uchaji na Ibada kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya wema na utakatifu wa maisha.

Wakleri wakuze ari na mwamko wa kimisionari wa kutaka kulihudumia Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kimsingi, Wakleri wanapaswa kuwa ni chemchemi na mashuhuda wa huruma, upendo, msamaha na ukarimu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Wakati huo huo, Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa Mapadre aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre, lakini pia iwe ni siku ya kujenga na kudumisha umoja na udugu miongoni mwa wakleri. Mapadre wanapoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu wakumbuke kwamba, wanawabeba waamini waliokabidhiwa na kupigwa chapa katika sakafu ya nyoyo zao.

Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wakleri wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waonje huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari makini ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji.

Kardinali Beniamino Stella anawaalika wakleri kujitaabisha kusoma na kutafakari ujumbe unaotolewa mara kwa mara na Baba Mtakatifu ili waweze kuboresha maisha na utume wao; katika uchovu na uchungu wa maisha na utume wa Kikasisi, waweze kupata faraja na matumaini yanayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba wito na utume huu mtakatifu umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mapadre wanaopitia vipindi vigumu vya maisha na utume wao, wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upole; wasikilizwe kwa makini; wasaidiwe kufikia mang’amuzi na ukomavu katika maisha. Huu ni wajibu wa kwanza kwa Maaskofu mahalia lakini hata kwa Jumuiya nzima ya waamini pamoja na familia zao, ambazo mara nyingi zinabeba Msalaba mzito! Wakleri ni watu ambao wanapaswa pia kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao! Kamwe Mapadre wasidhaniwe kuwa ni mashine za kutolea huduma ya mambo matakatifu!

Mapadre wapendwe katika ukweli na uwazi; wasaidiwe kupata mahitaji yao msingi. Waamini walei, wakishirikiana, wakisaidiana na kushauriana na Mapadre wao, maisha na utume wa Kanisa vitasonga mbele kwa ari kubwa zaidi! Pale Mapadre wanapoonekana kuchoka na kuanza kukata tamaa, waamini wawe mstari wa mbele kuwaenzi kwa sala na sadaka zao; kwa kutambua na kuthamini huduma zao pamoja na ushauri wa kidugu! Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, iwe ni fursa ya kuendelea bila kuchoka kuwasindikiza Mapadre katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

Utakatifu wa Mapadre

 

20 July 2019, 11:03