Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa linataka kuwajengea wanawake uwezo utakaowasaidia kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa linataka kuwajengea wanawake uwezo utakaowasaidia kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! 

Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa: Nguvu ya wanawake!

Wanawake Wasabato wamejifunza taalimungu katika Jumuiya za Kisabato; dhamana na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na mchango maalum wa wanawake katika kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika ulimwengu mamboleo. Ili kuweza kufanikisha azma hii, kuna haja ya kukazia malezi na majiundo ya kiroho na kimwili kwa wanawake wengi zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa (Baptist World Alliance, BWA), lililoanzishwa kunako mwaka 1905 huko nchini Uingereza, hivi karibuni limewakutanisha wanawake zaidi 400 kutoka katika nchi 50, huko Nassau nchini Bahamas, ili kujadiliana kuhusu umuhimu wa kupambana na changamoto za ushuhuda wa Kikristo katika ulimwengu mamboleo. Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa lina jumla ya Vyama vya Wanawake wa Kisabato vipatavyo 239 vinavyotoa huduma yake katika nchi 139. Katika mkutano huu, Wanawake Wasabato wamejifunza taalimungu katika Jumuiya za Kisabato; dhamana na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na mchango maalum wa wanawake katika kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Ili kuweza kufanikisha azma hii, kuna haja ya kukazia malezi na majiundo ya kiroho na kimwili kwa wanawake katika ngazi mbali mbali za maisha yao. Hatua hii lazima isindikizwe na ushiriki wa wanawake katika maisha ya hadhara na katika utume wa Kanisa. Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa linawapongeza wanawake kwa kuwa mstari wa mbele kuyatafsiri Maandiko Matakatifu kadiri ya lugha na makabila yao, urithi mkubwa kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Wanawake wanapaswa kusoma alama za nyakati na kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linakuwa ni chachu na taa katika mapito yao. Katika mkutano huu, wajumbe wameliomba Kanisa kutafakari kwa kina na mapana kuhusu Utume wa wanawake Wakristo katika Kanisa, ilikumbukwa kwamba, kumekuwepo na wanawake wengi ambao wamenyanyasika na kunyimwa haki zao msingi hata ndani ya Kanisa lenyewe!

Wanawake Wasabato wameweza pia kujadili changamoto, matatizo na fursa wanazozipata kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda wa maisha na tunu msingi za Kikristo katika maeneo yao ya kijiografia. Majadiliano ya kiekumene, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa ni kati ya changamoto zilizoibuliwa na wajumbe wa mkutano huu. Wanawake Wasabato wameazimia kwamba, wataendelea kujizatiti kusoma, kutafakari, kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kuanzia katika ngazi za kifamilia kama sehemu ya mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Katika mkutano huu, Mchungaji Tomas Mackey kutoka Argentina amechaguliwa kuongoza Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa, “BWA” katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2025.

Huyu ni mchungaji ambaye kwa muda wa miaka 30 amejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya familia ya Mungu kuanzia katika Kanisa mahalia hadi sasa amefikia ngazi ya kimataifa. Mama Vee Tetseo amechaguliwa kuwa Katibu mkuu wa Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa. Wanawake hawa katika sala na maombi yao, wamewakumbuka Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake hasa huko Sri Lanka. Mkutano mwingine wa Shirikisho la Wanawake Wasabato Kimataifa unatarajiwa kufanyika Julai 2020 huko Rio de Janeiro, nchini Brazil. Kwa sasa Shirikisho hili linajipanga kuzindua Kampeni ya Uinjilishaji Kimataifa inayofumbatwa katika majadiliano ya kiekumene kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha ya kila siku!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù alionesha masikitiko yake makubwa kutokana na nyanyaso na dhuluma ambazo wanawake wanakumbana nazo katika maisha na utume wao, kutokana na utamaduni wa mfumo dume ambao umepitwa na wakati! Hawa ni wanawake ambao wameendelea kujizatiti katika kulinda na kuzitegemeza familia zao katika huduma ya elimu, afya na ustawi katika ujumla wake. Wanawake bado wanabaguliwa hata katika maeneo ya kazi na kwamba, hawa ndio waathirika wakuu wa balaa la umaskini, mauaji ya wanawake pamoja na nyanyaso ambazo zinakwenda kinyume kabisa cha utu na heshima yao. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu amepembua kwa kina mapana kuhusu “Nafasi na dhamana ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo”.

Kwanza kabisa, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kutambua kwamba, kuna usawa na utofauti, kama kielelezo makini kinachotafuta uwiano mzuri unaojikita katika mahusiano dhidi ya utamaduni wa mfumo dume unaoendelea kumkandamiza mwanamke.  Kuna umuhimu wa kuvuka kishawishi cha kudhani kwamba, wote ni sawa sawa, kwa kushindwa kutambua tofauti, katika utambulisho wa mtu na asili kwani mwanamke na mwanaume wanakamilishana. Pili, Baba Mtakatifu anasema, uwezo wa mwanamke kuzaa ni kanuni na utambulisho maalum kwa wanawake ambao wamejaliwa uwezo wa kuendeleza zawadi ya maisha, kwa kuilinda na kuidumisha. Kanisa linapenda kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika medani mbali mbali za maisha ya mwandamu; kwani wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu na majiundo; shughuli na mikakati mbali mbali ya kichungaji na kwamba, wanawake wanaonesha sura ya huruma ya Mungu kwa binadamu.

Ni watu wanaojisadaka kwa njia ya huduma, kwa kuonesha ukarimu, kimsingi, wanawake ni sawa na tumbo la Kanisa linalopokea na kuzaa maisha. Tatu, Baba Mtakatifu anajaribu kuangalia mwili wa mwanamke kati ya tamaduni na bayolojia, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanamke mwili unaopendeza, lakini pia umesheheni madonda ambayo wakati mwingine yamesababishwa na dhuluma pamoja na nyanyaso. Mwili wa mwanamke ni kielelezo cha maisha, lakini kwa bahati mbaya, unaharibiwa hata na wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwasindikiza katika maisha! Kuna mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, biashara ya ngono na vitendo vya ukeketaji; mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuyavalia njuga, ili kusitisha vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake duniani, kiasi cha kuwageuza kuwa kama bidhaa inayouzwa sokoni, bila kusahau umaskini unaosababisha wanawake wengi kuishi katika mazingira magumu na hatarishi; kiasi hata cha kunyanyaswa, kielelezo cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine.

Nne, Baba Mtakatifu anapopembua kuhusu wanawake na dini anakazia zaidi mwelekeo wa kutafuta ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.  Anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa.  Wanawake ni wadau wakuu katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye utajiri mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa wanawake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya hadhara, katika medani mbali mbali: kisiasa, kiuchumi, kijamii na kikanisa. Wanawake wapewe fursa ya kushiriki mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji wa mikakati na sera mbali mbali; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya kifamilia. Wanawake wasaidiwe kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa.

Nguvu ya Wanawake
23 July 2019, 10:17