Tafuta

Vatican News
Sekretarieti Kuu la Kanisa Katoliki Eritrea inasikitishwa na kampeni chafu zinazoendeshwa dhidi yake kama sehemu ya utaifishwaji wa hospitali zake na Serikali! Sekretarieti Kuu la Kanisa Katoliki Eritrea inasikitishwa na kampeni chafu zinazoendeshwa dhidi yake kama sehemu ya utaifishwaji wa hospitali zake na Serikali! 

Kampeni chafu dhidi ya Kanisa nchini Eritrea! Utaifishaji!

Inasikitisha kuona kwamba, Serikali katika mchakato mzima wa kutaifisha miundo mbinu ya huduma ya afya inayomwilikiwa na kuendeshwa na Kanisa haijasikika ikitamka kwamba, taasisi hizi zinataifishwa kwa sababu ya kukithiri kwa rushwa; matumizi mabaya ya rasilimali fedha katika sekta ya afya, ukosefu wa ujuzi, maarifa na utaalam wa kuendesha taasisi hizi. Maamuzi mbele, Hatari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti Kuu ya Kanisa Katoliki Eritrea, Er.C.S. imeandika barua kufafanua kuhusu utaifishwaji wa taasisi za afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Eritrea uliofanywa na Serikali ya Eitrea katika siku za hivi karibuni. Kanisa linasema, Serikali ya Eritrea imetaifisha jumla ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zaidi ya 29. Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea limepinga hatua hii ya Serikali kutaifisha miundo yake ya huduma ya afya bila kutoa sababu za msingi! Bwana Tajan Abedel Aziz, Msemaji mkuu wa Wizara ya Afya amesikika akipotosha umma kwamba, hili lilikuwa ni zoezi na shughuli za kiofisi na wala Serikali haikuwa inapania kutaifisha Hospitali za Kanisa wala kuwatisha wafanyakazi wake. Lakini kimsingi Serikali ya Eritrea imefanya maamuzi haya bila ya kujadiliana na Kanisa Katoliki ambalo ni wamiliki wake halali. Viongozi waliotumwa kutekeleza zoezi hili, walifanya yote kwa niaba ya Serikali na wala hapa hakuna ubishi wowote.

Kuna baadhi ya Hospitali Serikali imetumia nguvu na kwenye baadhi ya vituo vya afya, wafanyakazi wamefukuzwa kwa nguvu, kiasi hata cha kushindwa kuwahudumia wagonjwa. Kuna baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati walilazimishwa kuweka sahihi kwenye Hati inayohamisha umiliki wa Hospitali na vituo hivi kutoka kwa Kanisa kwenda kwa Serikali. Pale waliposita kutekeleza amri hii, walitishiwa kuhusu usalama wa maisha yao na kutakiwa kutekeleza amri bila kuhoji maswali kwani huu ulikuwa ni uamuzi kutoka ngazi ya juu na wao walikuwa wanatekeleza wajibu wao tu. Huu ni ushuhuda kwamba, uhuru wa kuabudu na kidini nchini Eritrea haukuzingatiwa kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Kimsingi, Serikali ya Eritrea haina dini lakini wananchi wake wa dini na madhehebu yao.

Upendo kwa Mungu na jirani ni kanuni inayoendesha shughuli za huduma ya afya zinazotolewa na Kanisa Katoliki nchini Eritrea, kanuni hii haikuheshimiwa wala kuthaminiwa. Kanisa katika maisha na utume wake, limeendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kusimamia misingi ya haki, amani na maridhiano na kamwe halijawahi kuingilia masuala ya kisiasa, ingawa hata hii ni sehemu ya utume wake, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote! Kanisa Katoliki limekuwa likitoa huduma ya afya kwa watu wote bila upendeleo, jambo linaloweza kushuhudiwa na wale wote waliopata huduma kutoka katika vituo hivi! Kutaifishwa na hatimaye kufungwa kwa Hospitali, Vituo vya afya na Zahanati za Kanisa Katoliki kumesababisha kudhorota kwa huduma hii nchini Eritrea.

Kanisa Katoliki linasema, kuna Serikali ambazo hazina dini sehemu mbali mbali za dunia, lakini bado hata taasisi za afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo zinaendelea kufanya kazi bila vizingiti vyovyote. Hali hii ni kinyume cha Eritrea. Sekretarieti kuu ya Kanisa Katoliki nchini Eritrea inamshutumu kwa namna ya pekee Bwana Edoardo Calcagno ambaye ameendelesha kampeni ya kulichafua Kanisa, bila kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya taaluma yake kama mwandisi wa habari. Sekretarieti kuuu inajiuliza ni nani ambaye anachochea mpasuko huu kati ya Kanisa na Serikali na lengo lake ni nini? Bwana Edoardo Calcagno ameshutumu taasisi za afya zinazoedeshwa na kusimamiwa na Kanisa kuwa ni “vichaka vya rushwa na ufisadi wa fedha na mali ya taasisi hizi na kwamba, uamuzi wa Serikali ya Eritrea ni sehemu ya mbinu mkakati wa kutaka kukomesha vitendo hivi”.

Sekretarieti Kuu ya Kanisa Katoliki nchini Eritrea inasema haya ni maamuzi mbele yaliyofanywa na Bwana Edoardo Calcagno bila hata ya kujitaabisha kutafuta ukweli upande wa pili wa watuhumiwa hawa, hali inayoonesha kwamba, shughuli hii imetekelezwa bila ya kuzingatia ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Eritrea. Akaunti za Kanisa kuhusu Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati ziko sawa na zina kaguliwa mara mbili kwa mwaka. Inasikitisha kuona kwamba, Serikali katika mchakato mzima wa kutaifisha miundo mbinu ya huduma ya afya inayomwilikiwa na kuendeshwa na Kanisa haijasikika ikitamka kwamba, taasisi hizi zinataifishwa kwa sababu ya kukithiri kwa rushwa; matumizi mabaya ya rasilimali fedha katika sekta ya afya, ukosefu wa ujuzi, maarifa na utaalam wa kuendesha taasisi hizi. Kama Serikali haijatoa shutuma hizi dhidi ya Kanisa, Je, Bwana Edoardo Calgano amezipata wapi? Uragibishaji wake dhidi ya Kanisa nchini Eritrea hauna mashiko wala mafao kwa familia ya Mungu nchini Eritrea.

Eritrea: Afya
11 July 2019, 15:21