SECAM Miaka 50: Vipaumbele Barani Afrika: Dhana ya Sinodi, Jumuiya Ndogondogo, Ndoa na familia; Sakramenti za Kanisa, Wakimbizi & Wahamiaji & Haki na Ulinzi wa Watoto wadogo! SECAM Miaka 50: Vipaumbele Barani Afrika: Dhana ya Sinodi, Jumuiya Ndogondogo, Ndoa na familia; Sakramenti za Kanisa, Wakimbizi & Wahamiaji & Haki na Ulinzi wa Watoto wadogo! 

SECAM: Jubilei ya Miaka 50: Vipaumbele vya Kanisa Afrika

Mababa wa SECAM wanaendelea kubainisha vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo; Maisha ya ndoa na familia; utume wa vijana, Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Wakimbizi, wahamiaji na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Haki, amani na maridhiano ni muhimu kwa Bara la Afrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linaendelea na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na mkutano mkuu wa 18 wa SECAM na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 28 Julai 2019 kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Kampala, Uganda. Mkutano huu unaongozwa na kanuni inayowataka Mababa wa SECAM: Kuangalia, Kuamua na Kutenda! SECAM inasema, mchakato wa uinjilishaji Barani Afrika unakwenda sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa vinaanza kujitokeza kwani Mababa wa SECAM wamekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, mwelekeo mpya wa utendaji wa Kanisa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zinapaswa kuimarishwa na kuendelezwa ili kujenga misingi ya umoja, udugu, upendo na mshikamano kati ya waamini kwani huu ndio mfumo na utambulisho wa Kanisa Barani Afrika, bila kusahau utume wa vijana na familia! Ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili kuendelea kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, umesisitizwa sana. Hii iwe ni fursa ya waamini kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Katekesi ya awali na endelevu ni muhimu sana katika kupyaisha uelewa wa Mafundisho tanzu ya Kanisa, ili waamini waweze kuwa tayari kuyashuhudia, kuyalinda na kuyatetea pale yanaposhambuliwa.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika ni changamoto changamani inayohitaji kuvaliwa njuga na Kanisa Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika imetakiwa kuwa macho dhidi ya utamaduni wa kifo unafumbatwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba, kifo laini pamoja na shinikizo la ndoa za watu wa jinsia moja; mambo ambayo kimsingi yanasigana na kanuni maadili, utu wema na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sanjari na hili, Mababa wa SECAM wanasema, haki msingi na ulinzi wa watoto wadogo ni kati ya changamoto na vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, kwa sasa na kwa siku za usoni. Mababa wa SECAM wanasema, Familia inakabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia sanjari na mabadiliko msingi katika maisha ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi; mambo yanayochangia kushamiri kwa ubinafsi, ubabe na anasa.

Maaskofu wanabainisha kwamba, hivi ni vishawishi ambavyo kimsingi vinasigana sana na tunu msingi za maisha ya kifamilia kadiri ya mapokeo na tamaduni njema za Kiafrika; yaani ile hali ya mtu kujitosa kisawasawa katika upendo! Maaskofu wanakazia umuhimu wa kufanya maandalizi ya kina kwa wanandoa watarajiwa, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia, jambo ambalo linahitaji mikakati makini ya kichungaji kuhusu utume wa familia. Maaskofu wanawataka waamini waliopewa dhamana katika tume ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia kuhakikisha kwamba, zinatekeleza dhamana na wajibu wake bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia Barani Afrika. Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia inahusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho anasema Papa Francisko. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa.

Mababa wa SECAM wanaitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa macho na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; kazi za suluba kwa watoto wadogo pamoja na kukazia haki msingi za watoto wadogo. Kanisa Barani Afrika halina budi kujiwekea Mwongozo wa utekelezaji wa sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa. Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia amekazia umuhimu wa familia ya Mungu Barani Afrika kusimama kidete kulinda, kutunza, kuendeleza pamoja na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa Barani Afrika liwe ni shuhuda na chombo cha haki, amani na upatanisho hasa katika nchi zile ambamo bado kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kisiasa kama inavyojionesha nchini Sudan ya Kusini.

Wajumbe wa SECAM wamekumbushwa jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko alivyowapigia magoti viongozi wakuu wa Serikali na Upinzani nchini Sudan ya Kusini, akiwataka kuanza kuandika ukurasa mpya wa ujenzi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa utakaosimamia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu huko Sudan ya Kusini. Kanisa Barani Afrika linapaswa kuendelea kuwa ni chombo na shuhuhda wa misingi ya haki, amani na upatanisho. Umoja wa Afrika uwe ni chachu ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza, watekeleze wito huu kwa ari na moyo mkuu! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, CERAO limekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha demokrasia na utawala bora Barani Afrika kwa kuzingatia: demokrasia shirikishi, uhuru wa watu kutoa maoni yao; utawala wa Sheria sanjari na kuzingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; vita, kinzani na vitendo vya kigaidi pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani ni mambo yanayohitaji kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Toba na wongofu wa ndani; majadiliano ya kidini na kiekumene; ujenzi wa dhamiri nyofu pamoja na ushiriki mkamilifu wa waamini walei ni mambo muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika; kuteteleka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; maendeleo ya sayansi, teknolojia na utandawazi yanapaswa kuangaliwa kwa kina na mapana katika vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, katika sera na mikakati yake! Kwa upande wake, Askofu mkuu John Baptist Odama wa Jimbo kuu la Gulu, Uganda, amekakazia kuhusu nafasi, dhamana na utume wa  Makatekista katika mchakato wa: kufundisha na kulea imani.

Makatekista wanapaswa kuwezeshwa kikamilifu ili waweze kufundisha kwa umakini mkubwa kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na maisha ya sala, ili waamini waweze kupata neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya. Makatekista wanao wajibu wa kuwasaidia waamini kumwilisha imani yao katika uhalisia wa maisha kwa njia ya ushuhuda unaoleta mvuto na mguso. Ni watu wanaopaswa kuwasaidia waamini kujenga na kuimarisha moyo wa sala kama njia ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao. Askofu mkuu Anthony Muheria wa Jimbo kuu la Nyeri, nchini Kenya, amewataka Mababa wa SECAM kuhakikisha kwamba, katika sera na vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, waamini walei wanapewa kipaumbele cha pekee ili waweze kuwa ni nyenzo msingi za kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Waamini walei kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo hata wao wanashiriki katika: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, kumbe, ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa nyakati hizi. Waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika waendeleze majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mababa wa SECAM wanawashukuru na kuwapongeza waamini wote ambao wameendelea kusimama imara na thabiti katika imani, matumaini na mapendo, licha ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu, kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, itawasaidia sana watu wa Mungu Barani Afrika kutembea kwa pamoja, huku wakiwa wameshikamana kwa dhati. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya kwanza ambayo mwamini anaweza kuchota roho ya kweli ya kikristo.

Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaotembea pamoja katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Hii ni Jumuiya inayofumbatwa katika misingi ya: imani, matumaini na mapendo kwa kuambata mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndiyo wakimbizi na wahamiaji; maskini, wazee na wagonjwa ambao wanaonekana kana kwamba si mali kitu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Itakumbukwa kwamba, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM linaundwa na: AMECEA, yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati. IMBISA yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika. CERAO/RECOA: yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi pamoja na CEDOI, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Bahari ya Hindi.

SECAM: Vipaumbele
26 July 2019, 14:18