Mababa wa SECAM wamemchagua Kardinali Philippe Ouèdraogo kuwa Rais wa SECAM; Askofu Sithembele Sipuka na Askofu Lucio Andrice Muandala kuwa Makamu wake & Pd. Akaabiam, Katibu. Mababa wa SECAM wamemchagua Kardinali Philippe Ouèdraogo kuwa Rais wa SECAM; Askofu Sithembele Sipuka na Askofu Lucio Andrice Muandala kuwa Makamu wake & Pd. Akaabiam, Katibu. 

SECAM Jubilei miaka 50: Viongozi wapya. Kard. Ouèdraogo, Rais SECAM

Kardinali Philippe Ouédraogo kutoka Burkina Faso amechaguliwa kuwa Rais wa SECAM na Askofu Sithembele Sipuka kutoka Afrika ya Kusini, amechaguliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Askofu Lucio Andrice Muandula kutoka Msumbiji amechaguliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa SECAM. Pd. Terwase Henry Akaabiam, kutoka Nigeria, ameteuliwa kuwa Katibu mkuu wa SECAM.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM yamefikia kilele chake Jumapili tarehe 28 Julai 2019 kwa Ibada ya Misa iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Kampala, Uganda. Maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. SECAM katika mkutano wake wa 18 imemchagua Kardinali Philippe Nakellentuba Ouédraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina Faso kuwa Rais wa SECAM na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Gabriel Mbilingi aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa muda wa miaka sita!

Askofu Sithembele Sipuka wa Jimbo katoliki la Mthatha, Afrika ya Kusini, amechaguliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Askofu Lucio Andrice Muandula wa Jimbo la  Xai Xai, Msumbiji amechaguliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa SECAM. Mheshimiwa Padre Terwase Henry Akaabiam, kutoka Nigeria, ameteuliwa kuwa Katibu mkuu wa SECAM na hivyo kuchuku nafasi ya Padre Joseph Komakoma kutoka Zambia ambaye amemaliza muda wake wa uongozi. Baada ya mkutano wake, SECAM imetoa  ujumbe kwa familia ya Mungu Barani Afrika unaoongozwa na kauli mbiu “Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh. 13:3: 10:10). SECAM pia imetoa Tamko la Kampala kuhusu wajibu na wosia kwa familia ya Mungu Barani Afrika. 

SECAM: Viongozi
29 July 2019, 14:10