Tafuta

Vatican News
SECAM: Jubilei ya Miaka 50: Ujumbe kwa Familia ya Mungu Barani Afrika: Jubilei: Muda wa kushukuru, kujenga umoja na kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa! SECAM: Jubilei ya Miaka 50: Ujumbe kwa Familia ya Mungu Barani Afrika: Jubilei: Muda wa kushukuru, kujenga umoja na kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa! 

SECAM: Ujumbe kwa Familia ya Mungu Barani Afrika: Shukrani, Umoja & Matumaini

Mababa wa SECAM katika Ujumbe wao kwa Watu wa Mungu Barani Afrika na Madagascar wanakazia umuhimu wa Jubilei kama muda wa kushukuru, muda wa kujenga umoja na kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa! Ujumbe kwa familia ya Mungu Barani Afrika unaoongozwa na kauli mbiu “Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM yamefikia kilele chake Jumapili tarehe 28 Julai 2019 kwa Ibada ya Misa iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Kampala, Uganda. Maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. SECAM katika mkutano wake wa 18 imemchagua Kardinali Philippe Nakellentuba Ouédraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina Faso kuwa Rais wa SECAM na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Gabriel Mbilingi aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa muda wa miaka sita!

Mababa wa SECAM katika Ujumbe wao kwa Watu wa Mungu Barani Afrika na Madagascar wanakazia umuhimu wa Jubilei kama muda wa kushukuru, muda wa kujenga umoja na kuyaambata ya mbeleni kwa matumaini makubwa! Ujumbe kwa familia ya Mungu Barani Afrika unaoongozwa na kauli mbiu “Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh. 13:3: 10:10). Mababa wa SECAM wanamshukuru Mwenyezi Mungu chemchemi ya uhai kwa wema na upendo wake mkuu alioonesha kwa kuchagua Bara la Afrika kuwa ni makazi mapya ya Kristo Yesu, kama alivyosema Mtakatifu Paulo VI. Waamini kwa kuimarishwa na Neno na Sakramenti za Kanisa, wanajitoa kikamilifu na kujiaminisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu.

SECAM inamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1969 kwa ajili ya kumbu kumbu ya Mashahidi wa Uganda na kuwataka waamini Barani Afrika kuwa ni wamisionari kwa Bara la Afrika ili kuhakikisha kwamba, Ukristo unakita mizizi yake Barani Afrika. SECAM inamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo na huduma ya Wamisionari ambao wamewasaidia watu wa Mungu kumfahamu Kristo Yesu ambaye ni Njia, Ukweli na Uzima. Mababa wa SECAM wanamshukuru pia Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe na matashi mema kwa SECAM, ili iendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu Barani Afrika.

SECAM inalishukuru pia Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kwa mchango wake mkubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Inawashukuru watu wa Mungu nchini Uganda kwa ukarimu wao pamoja na wale wote waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzisha kwa SECAM inafanikiwa kwa kiasi kikubwa! Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu Barani Afrika. Umoja na mafungamano haya yanapata chimbuko lake kutoka katika imani kwa Kristo Yesu, Kanisa lake na kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Sala ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM imesaidia kuamsha tena kumbu kumbu angavu ya Mashahidi wa Uganda katika akili na nyoyo za waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ni tukio la Kikanisa ambalo limewakusanya wajumbe kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, kielelezo cha ukatoliki wa Kanisa unaofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Maadhimisho ya Jubilei imekuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, changamoto ni kuendelea kumwilisha ujumbe wa Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja, ili ulimwengu upate kusadiki. SECAM inaendelea kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa huduma ya haki, amani na upatanisho, kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa shughuli za kichungaji.

SECAM inakaza kusema, lengo ni kusimama kidete dhidi ya: ukoloni wa kiitikadi, ukwapuaji wa ardhi Barani Afrika; kinzani za kisiasa na kuyumba kwa misingi ya demokrasia shirikishi; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; vitendo vya kigaidi pamoja na biashara ya silaha duniani! Mababa wa SECAM wanaendelea kusema kwamba, Jubilei ni kipindi cha kukumbatia ya mbeleni kwa matumaini, kwa ajili ya familia na nchi mbali mbali Barani Afrika. Ni muda wa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazofumbatwa katika ndoa kati ya bwana na bibi, jukwaa la kwanza kabisa katika mchakato wa uinjilishaji.

SECAM inaendelea kuhimiza umuhimu wa familia ya Mungu Barani Afrika kukita uelewa wake kadiri ya mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. SECAM kwa njia ya vyombo vyake vya huduma kama Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas, Tume za Haki na Amani pamoja na taasisi mbali mbali, SECAM itaendelea kujizatiti zaidi katika huduma ya maendeleo fungamani ya binadamu, sanjari na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. SECAM inakaza kusema, shughuli za kisiasa na kijamii ni sehemu ya uinjilishaji unaopania kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Afrika.

Mashahidi wa Uganda wanawakumbusha watu wa Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanakuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa kwa kutekeleza kiaminifu zile ahadi za Ubatizo. Mashahidi wa Uganda ni mfano bora wa kuigwa na waamini wote Barani Afrika, lakini zaidi na Makatekista wanaojisadaka kila siku kwa ajili ya kuwaandaa watu wa Mungu kupokea na kuadhimisha mafumbo ya Kanisa. Watoto na vijana ni wadau muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji Barani Afrika. Hawa wanapaswa kulindwa na kupewa malezi na majiundo makini, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu!

Mababa wa SECAM wanatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wanawake katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na jamii katika ujumla wake. Ushiriki mkamilifu wa wanawake katika elimu, afya na uinjilishaji hauna mbadala hata kidogo! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linasema, ili kuendelea kuenzi Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wa SECAM Barani Afrikam Mababa wa SECAM wanatarajiwa kutoa Hati ya Kampala ili kuwasaidia watu wa Mungu kuboresha uelewa wao kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, ili aendelee kuwa kweli ni Njia, Ukweli na Uzima.

Mwishoni mwa Ujumbe wao, Mababa wa SECAM wanajiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Afrika, Mtakatifu Yosefu pamoja na Mashahidi wa Uganda sanjari na watakatifu wote wa Afrika na Madagascar, ili waweze kuwahamasisha zaidi, wawe na ari na moyo wa kumfuasa Kristo Yesu. Ni matumaini ya Mababa wa SECAM kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 yatakuwa ni chachu ya upyaisho wa maisha mapya katika Kristo Yesu na huduma kwa Injili na Ulimwengu katika ujumla.

SECAM: Ujumbe

 

30 July 2019, 15:47