Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake Barani Afrika. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake Barani Afrika. 

SECAM: Jubilei ya Miaka 50: Kilele 28 Julai 2019: Mshuhudieni Yesu!

Ilikuwa ni tarehe 29 Julai 2018, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ilipozindua mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa, wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Paulo VI, mwaka 1969. Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linajiandaa kuadhimisha Mkutano wake mkuu wa 18 kuanzia tarehe 20 Julai, siku ya kuwasili kwa wajumbe zaidi 400 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, hadi tarehe 29 Julai 2019 siku ya kuondoka. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Familia ya Mungu Barani Afrika inamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wa SECAM Barani Afrika. Kama kawaida ya maadhimisho ya Jubilei, hiki ni kipindi muafaka cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Jubilei ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza, ili kuanza kujiaminisha tena kwa ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Mkutano wa SECAM huko Kampala, Uganda unatarajiwa kutoa Waraka wa Kampala, ambao utajikita zaidi katika shughuli za kichungaji Barani Afrika. Waraka huu, utaonesha vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika kwa siku za usoni. Kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 28 Julai 2019 kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo. Tukio hili litaadhimishwa kwenye Majimbo mbali mbali Barani Afrika, kwenye Parokia, Vigango na Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo! Kilele cha Mwaka wa Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM umepambwa kwa namna ya pekee na shukrani, toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho pamoja na familia ya Mungu Barani Afrika kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Ilikuwa ni tarehe 29 Julai 2018, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ilipozindua mchakato wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa, wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1969. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Kilele chake kitakuwa ni tarehe 28 Julai 2019. Familia ya Mungu Barani Afrika ilitumaini kwamba, ingekuwa ni fursa tena kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Bara la Afrika, lakini kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika, Baba Mtakatifu hatakuwepo katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM. Kilele hiki ni kuanzia tarehe 23-28 Julai 2019, huko Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Monsinyo John Baptist Kauta, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, zinaonesha kwamba, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda kwa kushirikiana na Maaskofu Katoliki Uganda walikuwa wamemwalika Baba Mtakatifu Francisko kuhudhuria. Maaskofu zaidi ya 400 kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika wanatarajiwa kuhudhuria Hali ya Bara la Afrika; Uinjilishaji wa kina; Toba na Wongofu wa ndani; Majadiliano ya kidini na kiekukeme pamoja na maazimio ni kati ya mambo makuu yaliyojadiliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. SECAM katika mkutano wake wa kumi na sita, uliohitimishwa Julai, 2013 huko Kinshasa, DRC. Wajumbe wa SECAM waliamua kuadhimisha Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, kama njia ya kuenzi mchango mkubwa uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, baada ya kuchapisha Waraka wake wa kichungaji, “Africae Munus” yaani “Dhamana ya Afrika”, kunako mwaka 2011. 

SECAM inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, bado kuna sababu msingi za kuendelea kujikita katikamchakato wa upatanisho, haki na amani Barani Afrika, ukizingatia changamoto changamani zinazoendelea kuiandama familia ya Mungu Barani Afrika! Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa SECAM kwa mwaka huo wa 2013 yaliongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika katika huduma ya haki, amani na upatanisho. SECAM imetoa Maazimio ambayo yanapaswa kutendewa kazi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, kwa kutambua kwamba, kama Kanisa, linapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana fika na ubaguzi, nyanyaso na mifumo yote ile ambayo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kujitakasa kutoka katika undani wa Kanisa lenyewe. Kanisa halina budi kusimama kidete kuzungumza ukweli na uwazi kama sehemu ya mchakato wa kupambana na sera za kisiasa, kijamii na kidini kwa kuonesha nafasi ya Kanisa kama familia ya Mungu katika huduma ya haki, amani na upatanisho.

SECAM imejiwekea sera na mikakati madhubuti ya kushirikiana na Vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Barani Afrika katika kukoleza na kuimarisha majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. SECAM inapenda kukazia Mafundisho Jamii ya Kanisa, hasa miongoni mwa waamini walei, ili waweze kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye mvuto na mashiko wakitambua kwamba, wao kimsingi wanapaswa kuwa ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia. SECAM imewataka waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika na watu wenye mapenzi mema, kutambua, kuheshimu na kuendeleza dhamana, utu na heshima ya ndoa ya Kikristo na Familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu na kadiri ya tunu msingi za Kiinjili. Wajumbe wa SECAM wanatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika mikakati ya upatanisho, haki, amani na Uinjilishaji wa kina; wanawake wapewe fursa ili waweze kuchangia karama na utajiri wao katika maisha na utume wa Kanisa.

SECAM inawataka kwa namna ya pekee viongozi Wakatoliki kutoelemewa na uchu wa mali na madaraka, bali watambue kwamba, uongozi ni kwa ajili ya huduma kwa jirani zao na wala si fursa ya kujilimbikizia mali. Watumie karama, taaluma na mafanikio walio bahatika kupata kama baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli; daima wakiwa mstari wa mbele kulinda na kutunza mazingira, kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. SECAM ina shauri kwamba, kila Jimbo Barani Afrika liunde Tume ya Haki na Amani pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaoliwezesha Kanisa Barani Afrika, kuweza kumwilisha ujumbe wa Dhamana ya Afrika katika maisha na vipaumbele vyake!

SECAM pia inatambua umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa waamini na wananchi wanaoishi Barani Afrika. Majadiliano ni nyenzo muhimu kwa ajili ya kudumisha msingi wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutolea ushuhuda wao kama nyenzo ya kushirikishana upendo wa Mungu kwa watu wote. SECAM inasema, majadiliano haya hayana budi kujikita katika ukweli, heshima na uvumilivu sanjari na kuwa na mikakati kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa ajili ya mafao ya wengi Barani Afrika kwa kuvunjilia mbali miundo inayochangia uwepo wa dhambi na mambo yote yanayochangia umaskini na nyanyaso katika utu na heshima ya binadamu. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar linaendelea kuhimiza umuhimu wa kuenzi Injili ya Uhai kwa watoto, familia pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula na lishe bora; huduma bora ya elimu na afya na kwamba, elimu inachangia kwa namna ya pekee katika kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho kati ya watu.

SECAM kwa namna ya pekee, imewakumbuka pamoja na kuonesha mshikamano wake na nchi za Kiafrika ambazo kwa sasa zinakabiliana na vita, chuki na madhulumu ya kidini na kisiasa hasa: DRC, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Nigeria, Misri, Mali na baadhi ya sehemu ambazo mambo si shwari sana. SECAM inakumbusha kwamba, rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika unapaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Bara la Afrika na wala si kwa ajili ya kikundi cha watu wachache na familia zao tu! SECAM inaendelea kufafanua kwamba, ukabila, udini na umajimbo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati Barani Afrika. Badala yake familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujikita katika ujenzi na udumishaji wa misingi ya haki, amani na utulvu na kwamba, kuna haja ya kuendelea kujikita katika dhamana ya uinjilishaji wa kina, kama sehemu ya mchakato unaopania toba na wongofu wa ndani, Yesu Kristo akipewa kipaumbele cha kwanza katika uhalisia wa maisha ya waamini.

SECAM 50 YRS
18 July 2019, 16:48