Tafuta

Vatican News
Rais Yowei Kaguta Museveni wa Uganda amewataka Maaskofu wanaotoka Ukanda wa Maziwa Makuu kushirikiana ili kuimarisha misingi ya haki, amani na upatanisho! Rais Yowei Kaguta Museveni wa Uganda amewataka Maaskofu wanaotoka Ukanda wa Maziwa Makuu kushirikiana ili kuimarisha misingi ya haki, amani na upatanisho!  (AFP or licensors)

SECAM: Haki, amani na upatanisho Ukanda wa Maziwa Makuu!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa kitume, Africae munus" anasema, Upatanisho na haki ni misingi mikuu miwili ya amani duniani! Upatanisho wa kweli unafumbatwa katika wongofu wa kwelii; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tofauti msingi za kidini na kiimani ni amana dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani; ukabila na umajimbo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” analitaka Kanisa Barani Afrika kuwa chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu likibidishwa na imani inayomwilishwa katika Injili ya upendo, Kanisa lazima liwe ni chombo na shuhuda wa upatanisho, haki na amani. Huu ni utume maalum ambao unapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa Katoliki Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujielekeza zaidi katika amana na utajiri wa Neno la Mungu ili iweze kushiriki kikamilifu katika huduma ya upatanisho, haki na amani kwa kuwa watumishi aminifu wa Neno la Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani duniani! Waamini wawe ni mashuhuda wa upendo katika ukweli, kwani hii ndiyo chemchemi ya amani ya kudumu. Waamini wajitahidi kumwilisha ukweli wa Sakramenti ya Upatanisho, wajenge na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kukazia utamadunisho wa Injili na uinjilishaji wa utamadunisho.

Upatanisho na haki ni misingi mikuu miwili ya amani duniani! Upatanisho wa kweli unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tofauti msingi za kidini na kiimani, uwe ni utajiri na amana dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani; chuki na uhasama kwa misingi ya udini. Watu watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi na asili ya umoja, upendo na udugu na kamwe hawezi kuwa ni chanzo cha: vita, mauaji na vitendo vya kigaidi. Waamini wana wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na maridhiano, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu. Waamini walinde na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani uchafuzi wa mazingira ni kielelezo pia cha kumong’onyoka kwa utamaduni, kanuni maadili na utu wema!

Ni katika muktadha huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, “CENCO”. Itakumbukwa kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano nchini DRC. Rais Museveni amewaomba Maaskofu kutoka Ukanda wa Maziwa Makuu kushirikiana na kushikamana kwa dhati ili kusaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Ni matumaini ya Rais Museveni kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda litashirikiana kwa dhati na "CENCO" ili hatimaye, kuweza kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa na ukosefu wa misingi ya haki na amani nchini DRC, ili hatimaye, haki, amani na maridhiano kati ya watu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Eneo la Maziwa Makuu kwa miaka mingi sasa limekuwa ni uwanja wa vita, kinzani za kikabila na kisiasa; kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka DRC, Rwanda na Burundi ni matokeo ya kinzani hizi, kiasi hata cha kuongezeka vitendo vya uhalifu wa kikanda na kimataifa. Ni matumaini ya Rais Yoweri Kaguta Museveni kwamba, Kanisa Barani Afrika litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho!

Kwa masikitiko makubwa, Askofu Marcel Utembi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC amesema, kuna askari wa kukodiwa kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika wanaoshiriki katika vita na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na upatanisho kwa faida zao binafsi. Hawa ni chanzo kikubwa cha ukosefu wa amani na utulivu katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, hata kuna Askari wa kulipwa kutokana Uganda, wanaendesha mashambulizi ya kushtukizia huko Kaskazini Mashariki mwa Uganda. Rais Kaguta Yoweri Museveni amewahakikishia Maaskofu wa "CENCO" kwamba, atasaidia kila linalowezekana ili kurejesha tena amani na utulivu Eneo la Maziwa Makuu. Pamoja na mambo mengine, amekazia umuhimu wa ushiriki mkamilifu wa raia katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

SECAM: Upatanisho
26 July 2019, 13:48