Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XVII: Changamoto: Shindeni vikwazo vya sala kwa kusali zaidi! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XVII: Changamoto: Shindeni vikwazo vya sala kwa kusali zaidi! 

Tafakari Jumapili XVII ya Mwaka: Vuka vizingiti vya sala kwa kusali!

Sala ya Baba Bwana ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake. Kristo Yesu amekuwa ni mfano bora wa mtu anayesali kwa kujiachilia na kujiaminisha mikononi mwa Baba yake wa mbinguni. Sala si lele mama ina ugumu na changamoto zake katika maisha! Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, jifunzeni kuvuka vikwazo vya sala kwa kusali zaidi!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari Masomo ya liturujia ya dominika ya 17 ya mwaka C wa Kanisa. Baba Yetu Uliye mbinguni au Sala ya Bwana ni sala inayomwonesha mwamini uso wa huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu. Huu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake na mwongozo thabiti wa maisha ya Mkristo. Sala ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo kama anavyofundisha na kushuhudia Yesu mwenyewe katika maisha yake. Katika mafundisho yake makuu, Yesu anawafundisha wanafunzi wake namna ya kusali vyema, huku wakimwelekea Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma.

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mwa 18: 20-32 ) ni kutoka katika kitabu cha Mwanzo. Bwana Mungu anadhamiria kuiangamiza miji ya Sodoma na Gomora kwa sababu dhambi zao zimeongezeka sana. Abrahamu anasimama mbele za Bwana akisali na kumuomba asiiangmize, asiiangamize kwa sababu ndani yake wamo wenye haki ambao kwa uadilifu wao wanaweza kuwa sababu ya miji ile kuokolewa. Mara sita Abrahamu anamwomba Mungu akimsihi kuhusu idadi ya wenye haki katika miji hiyo, akipunguza idadi hadi kufikia 10. Kwa bahati mbaya katika miji yote hiyo idadi ya wenye haki haikufika 10. Miji inaangamizwa. Hakuna idadi ya kutosha ya wenye haki wanaoweza kuizuia hasira ya Mungu kwa miji hiyo ya Sodoma na Gomora.

Somo la pili (Kol 2:12-14 ) ni kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai. Katika somo hili Mtume Paulo anaelezea maana ya ubatizo katika fumbo la ukombozi wa mwanadamu. Kristo amemkomboa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ni kwa njia ya ubatizo mwanadamu analishiriki fumbo hili. Ubatizo ni kupitishwa katika mauti ya Kristo, kuzikwa pamoja naye na kufufuka pamoja naye. Ni kwa njia ya ubatizo mtu anayapata yale mafaa ya ukombozi aliyoyaleta Kristo.

Injili (Lk 10:38-42) Katika Injili ya dominika ya leo, Yesu anawafundisha wanafunzi wake Sala ya Baba Yetu. Wayahudi walikuwa na sala zao walizozisali kwa nyakati maalumu. Yohane Mbatizaji pia aliwafundisha sala wanafunzi wake. Leo mwanafunzi mmoja anamwomba Yesu naye awape sala itakayowatambulisha kama wanafunzi wake. Yesu anawafundisha sala ya Baba yetu. Kimsingi katika sala hii Yesu hawafundishi maneno mapya au maneno ya siri watakayoyajua wao tu bali cha kwanza anawafundisha kuhusu yule wanayemwomba wakisali. Mnaposali semeni “Baba yetu uliye mbinguni”. Ni jambo la kwanza na la msingi kujua ni nani wanayemwomba na wana uhusiano gani naye. Na Yesu anawaonesha ukaribu walionao na Mungu kiasi cha kumwita Baba.

Ni kutoka hapo sala yao iwe kwanza ni ya kumtukuza Baba na kujiweka chini ya mapenzi yake ndipo waweze kumwomba kwa ajili ya mahitaji yao ya kimwili na ya kiroho. Na tena kwa njia ya mfano wa rafiki mwenye saburi Yesu anawaonesha kuwa Baba wamwombaye ni baba anayeaminika, ni baba wa kumwendea kwa kujiaminisha kwake, si kama mwanadamu anayeweza kugeuka. Sala yao iwe ni sala ya kudumu na ya bila kuchoka. Yesu anawaonesha kuwa sala ya Baba yetu ambayo amewafundisha pamoja na kuwa ni sala kwa yenyewe lakini pia ni mfano wa kufuata wakati wowote mtu anaposali. Sala yoyote ya mfuasi wa Kristo iwe ni sala inayomtambua Baba, inayomtukuza na inayomweka mtu chini ya mapenzi ya Baba na ni kutoka katika mwelekeo huo sala ijielekeze katika mahitaji ya mwombaji, mahitaji ya kimwili na ya kiroho.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanatupa dhamira ya sala na kutualika tutafakari juu ya maisha yetu ya sala. Mtakatifu Augustino anaielezea sala kuwa ni kuuinua moyo kumuelekea Mungu. sala ni mawasiliano kati ya kiumbe na Muumba wake ambapo kiumbe kinakiri ukuu, utakatifu, enzi na sifa za Muumba na hapo hapo kutambua udogo, uhitaji na utegemezi wake kwa Muuba. Kwa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu sala ni kutazama tu kuelekea mbinguni. Sala ni mlio wa shukrani katika yote mawili: majaribu na furaha. Ni kwa njia ya Kristo na kwa mastahili ya sadaka yake msalabani mwanadamu amepata nafasi ya kumuita Mungu Baba na kutumaini kutoka kwake neema kwa maisha yake.

Uhusiano huu mpya kati ya Mungu na mwanadamu hudumishwa na kufanywa hai daima kwa njia ya sala. Mungu amewaagiza watu wake kumwendea kwa sala. Kristo amefundisha kusali na yeye mwenyewe amekuwa mfano wa kwanza wa kusali na hivi akatuhakikishia kuwa sala zetu hazipote bure kwani kila aombaye hupewa, abishaye hufunguliwa na atafutaye hupata.  Kumbe sala na maisha ya kikristo havitengani, ni pande mbili za sarafu moja. Tunapotafakari leo juu ya maisha yetu ya sala tujibidiishe kufufua ndani yetu moyo wa sala. Tusali kwa dhati na tumwombe Mungu ili maisha yetu yote yawe sala. Kusali wakati mwingi huwa na changamoto na ugumu wake. Upo uchovu wa kimwili lakini pia zipo juhudi za yule mwovu ambaye hataki kutuona tukipiga hatua katika sala. Mtu hujifunza kusali kwa kusali na huvuka vikwazo vya sala kwa kusali. Ushuhuda wa watakatifu walioushinda ulimwengu kwa njia ya sala uwe kichocheo chetu katika kukuza maisha ya sala.

Liturujia J17 Mwaka C

 

26 July 2019, 10:37