Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVI ya Mwaka: Jengeni urafiki wa kweli na Kristo Yesu kwa njia ya: Tafakari, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma kwa jirani! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVI ya Mwaka: Jengeni urafiki wa kweli na Kristo Yesu kwa njia ya: Tafakari, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma kwa jirani!  (Vatican Media)

Tafakari Jumapili XVI: Jengeni Urafiki: Neno, Sakramenti & Kazi

Wakristo wajibidishe kuwahudumia jirani zao huku wakiendelea kujitajirisha katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kielelezo cha imani tendaji! Waamini wakizama sana katika malimwengu, wanaweza kujikuta wakijitafuta na kujihudumia wao wenyewe. Yesu Kristo anapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya sala na huduma kwa jirani.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Ndugu wapendwa katika Kristo, Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari zake, anaendelea kukazia kuhusu umuhimu wa sala na kazi kama kielelezo cha maisha ya Mkristo, kama ilivyojionesha wakati Yesu alipotembelea Familia ya Maria na Martha, dada zake Lazaro. Sala na kazi ni chanda na pete na wala hakuna msigano wa aina yoyote ile; ni mambo yanayopaswa kumwilishwa kikamilifu katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Yesu anamwonya Martha aliyejitaabisha mno kwa mambo ya kidunia na kwamba, alihitaji pia kusikiliza Neno la Mungu, kama alivyokuwa anafanya dada yake Maria, huu ndio mwelekeo sahihi kwa mfuasi wa Kristo. Wakristo wajibidishe kuwahudumia ndugu zao wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, huku wakiendelea kujitajirisha katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kielelezo cha imani tendaji! Waamini wakizama sana katika malimwengu, wanaweza kujikuta wakijitafuta na kujihudumia wao wenyewe.

Yesu Kristo anapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya sala na huduma kwa jirani. Baba Mtakatifu anawaka waamini kujenga utamaduni wa kuzungumza na Yesu kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; mambo ambayo yanajenga na kuimarisha uhusiano wa karibu na Kristo, kama alivyokazia Mtakatifu Benedikto, Abate, Ora et Labora! Huduma kwa maskini na wahitaji ipate chimbuko lake kutoka kwa Kristo kwani huduma hii pia inaweza kumpeleka mwamini kwa Kristo. Ni mwaliko kwa waamini kumwomba Bikira Maria, Mama aliyefaulu kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kuhudumia, ili awafundishe kutafakari Neno la Mungu na kusali kwa uaminifu, daima wakiwa makini kuona na kuguswa na shida za jirani zao kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema!

Ndugu wapendwa, leo tena tunamshukuru Mungu kwa kutupata nafasi ya kusikiliza neno lake. Dominika iliyopita tulitafakarishwa sana juu ya dhana ya ujirani na tukaongozwa na jibu la kibiblia katika habari ya Msamaria mwema. Na pengine wengine tukapanua tafakari yetu kutoka jirani yangu ni nani mpaka kujiuliza kuwa mimi ni jirani ya nani.  Neno la Mungu dominika hii linatupa nafasi ya kusikia au kuona uwepo wa Mungu kati yetu. Mwandishi wa somo la kwanza anamwonesha Mungu katika sura ya mwanadamu. Mungu anawakilishwa katika sura ya mwanadamu na wakiwepo malaika wawili anaongea na kula na Abrahamu. Hapa twaona upendo thabiti wa Mungu kwa Abrahamu na mkewe na hapa Mungu anathibitisha tena ahadi yake ya uzao ambayo tayari aliitoa kwa Abrahamu – Mwa. 12:1-3. Hapa muelekeo wa Mungu kwa upendeleo wa taifa la Israeli unaonekana wazi.

Upendeleo huu umeonekana tangu wito wa Abrahamu na sasa anauthibitisha. Katika uthibitisho huu, ile hatari iliyoonekana kuikumba ile ahadi inapotea. Lengo la kanisa hapa kuweka somo hili ni kuonesha uwepo au ukaribu wa Mungu kwa watu wake. Katika somo la Injili twaona uwepo huu wa Mungu kwa njia ya Mwanae. Yesu yuko nyumbani kwa kina Martha na Maria – mwinjili Yohani anasema ni huko Bethania – 11:1. Mahali hapa Bwana alizoea kupita na kupumzika alipokuwa akifanya safari zake karibu na Yerusalemu. Martha anahudumia na Maria anakaa na Yesu. Ila kuna malalamiko toka wa Martha akimtaka ndugu yake atoe huduma kwa ugeni uliokuwepo. Yesu anasema wazi –Maria kachagua fungu lililo jema – kukaa na Bwana. Urafiki wa Yesu na familia ya Lazaro uko wazi katika maandiko – Yoh. 11:5 – Yesu alimpenda Martha, pamoja na dada yake na ndugu yao Lazaro.

Yesu anataka kutufundisha nini hapa anaposema Maria kachagua fungu lililo jema? Tumeona kuwa Martha anahudumia na Maria anasikiliza. Wote wawili wanafurahia uwepo wa Bwana Yesu. Martha anachagua kufanya kazi au kuhudumia na Maria anachagua kukaa na Bwana, kujenga mahusiano zaidi. Mwinjili Marko 3:14 – anasema kuwa wale walioitwa walikuwa na majukumu mawili – kukaa na Bwana. Maana yake  kukaa na Bwana, kumfahamu, kuhusiana naye na kulishwa naye  na halafu kutumwa, yaani kwenda kuwatumikia wengine, kutangaza habari njema kwa maneno na matendo. Mara nyingi wengi wetu tunapata shida kuweka hili vizuri na pengine tunatanguliza huduma kabla ya kujenga mahusiano thabiti. Kinachotakiwa hapa si kuchagua kati ya Martha na Maria ili kuwa upande wa mmoja.

Mtume wa kweli anatakiwa kuwa Martha na Maria. Ila kadiri ya maandiko utaratibu unakuwa kwanza kukaa na Bwana na kutenda kazi yake. Ye yote aliyesikia neno la Bwana anawajibishwa kwenda kutangaza habari njema. Ili kumtangaza Bwana, hatuna budi kukaa naye, kumjua vizuri, kumpenda na kumtumikia. Wengi wetu tunahangaika sana hapa. Tunataka kufanya kazi ya Bwana kabla ya kumjua, kuwa na mahusiano thabiti na Bwana mwenyewe. Tunataka kufanya kazi ya Bwana kabla ya kumfahamu Bwana wa kazi. Mwandishi mmoja Fred Craddock anasema kuwa watu wengi wanampoteza Mungu na malengo ya sala kwa vile wanasahau kwamba kinachotakiwa si kuongea sana juu ya Mungu bali twatakiwa kuongea na Mungu na kukaa naye. Leo pia tunapata nafasi ya kutafakari tena juu ya dhana ya urafiki. Inasemekana kuwa urafiki uko katika namna tatu – mtu hupendwa kwa kwa jinsi alivyo au kile alicho nacho au kwa kile afanyacho.

Aidha inasemekana kuwa urafiki wa kweli wahusisha mvuto na uelewa wa ndani kati ya watu wawili. Ni muungano wa roho mbili. Urafiki huu wavuka ule wa tamaa ya mwili. Watu wa kale walisema urafiki wa kweli ni roho moja katika miili miwili. Urafiki wa kweli hujengwa katika mambo mazuri na yenye ukweli. Ni tofauti na urafiki wa wanaojiunga kufanya uovu.  Urafiki unadai fadhila, jibu toka kwa apendwaye na hulishwa na uaminifu. Biblia imejaa vifungu vinavyosifu urafiki – rafiki mwaminifu ni hifadhi imara, aliyempata amepata hazina – Bin Sira 6:14. Kipimo cha urafiki ni uaminifu na ukweli. Kumbuka msemo wa Kiswahili – akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Tunapewa changamoto kubwa sana sisi wanadamu tunapotafakari juu ya urafiki wa kweli wa Yesu, ule wa kuwa tayari kutoa uhai wake kwa ajili yetu.

Kristo Yesu alikuwa na utukufu lakini hakung’ang’ania hilo. Akaacha hayo akaja kwetu ili kutupata  - Fil. 2:5-11. Akawa tayari kufa tena kifo cha msalaba. Urafiki wa kweli huzaa uzima. Bahati mbaya sehemu kubwa ya urafiki kati yetu inakita kwenye kile alicho nacho au kile afanyacho mwingine. Na si kwa jinsi alivyo. Yesu alitupenda kwa jinsi tulivyokuwa. Je urafiki kati yetu unakita katika misingi ipi? Tutafakarishwe na habari kama ilivyo katika hadithi za Esopo. Tunasoma habari ya watu wawili mmoja kiwete na mwingine kipofu na ilitokea wakajikuta katika mazingira magumu na hatarishi na namna ya pekee na ya haraka ya kujiokoa ikiwa ni wao wenyewe tu kusaidiana. Ilibidi wafanye maamuzi ya haraka na salama. Kipofu alikubali kumbeba kiwete mgongoni. Mmoja akawa macho kwa mwingine na mwingine akawa miguu kwa mwenzake. Wakasalimika. Dhana ya urafiki na uaminifu inawaokoa na hatari ya kifo. Walisaidiana kwa jinsi walivyo.

Huu nido urafiki hai. Mtu anapendwa kwa jinsi alivyo. Na ndivyo alivyofanya Mungu na ndivyo anavyofanya Yesu. Sisi tumesahau dhana hii na kuhusisha urafiki na alicho nacho mtu au afanyacho. Je urafiki kati yetu ukoje? Kwa urafiki kati yetu tunapata uzima au ni majanga? Inasemekana kuwa ili urafiki wetu uwe na mizizi imara na kuzaa matunda hauna budi kujikita katika kuyatambua mapenzi ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Ili tuweze kufanya kazi ya Bwana na kutimiza mapenzi ya Mungu hatuna budi kwanza kukaa na Bwana ili tuweze kutambua vizuri mapenzi yake na hivyo kuweka katika matendo kile tulichokifahamu.

16 July 2019, 16:18