Tafuta

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kutangaza, kushuhudia sanjari na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini walei wanaitwa na kutumwa kutangaza, kushuhudia sanjari na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! 

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XIV: Utume wa waamini walei!

Huku kutumwa kwa hao 70 kuna maanisha utume wa walei. Kwa hiyo utume huu unatuhusu sote – wabatizwa. Kauli mbiu ya Yesu iko wazi - mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache. Na wajibu huu unajikita katika mambo makuu mawili: sala na utendaji. Hapa ndipo ubatizo wetu unawapata wajibu rasmi. Tukumbuke kuwa sisi sote ni wamisionari. tunaitwa na kutumwa duniani!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.  - Dodoma

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanatambua na kuthamini sana mchango wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Unawaalika walei kushirikiana kikamilifu na viongozi wa Kanisa katika kutekeleza wajibu wao wa: Kinabii, Kikuhani na Kifalme unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Waamini walei washiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili kujichotea neema na baraka katika maisha yao, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya tunu msingi za Kiinjili. Wakleri wawe mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, waamini walei wanasaidiwa kukua na kukomaa katika maisha na utume wao; wawe mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Ndugu zangu, baada ya dominika iliyotangulia kutupatia changamoto ya ufuasi, leo tunaona Yesu akiwatuma watu waende kupeleka Habari Njema. Tulipata nafasi kuona jinsi Yesu anavyotaka tumfuate na anaweka bayana masharti ya ufuasi. Pia tuliweza kuona wasiwasi wa mwanadamu katika kumfuata Bwana. Lakini pia tulipata kuona jibu analotupatia mtume Paulo ili ufuasi uwezekane. Mtume Paulo anasema ili ufuasi uwezekane ni lazima kuongozwa na roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya roho yake Kristo. Kwa namna hii ufuasi utawezekana.

Leo tunasikia katika Injili juu ya utume wa wafuasi 70. Injili ya Luka ina habari mbili za utumaji wa mitume. Sura ya 9 wanapelekwa wale 12 na sura ya 10 wale 70. Injili ya Matayo ina habari ya kutumwa mitume 12 tu. Huku kupelekwa 70 kadiri ya Luka kwaelezea utume wa kimataifa na ule wa Matayo (10:6) kwaelezea utume katika taifa ya Israeli – kwa kondoo waliopotea wa Israeli. Kadiri ya Wayahudi wa wakati huo yapo makabili 12 ya Israeli na mataifa 70 katika ulimwengu. Kwa hiyo huku kupelekwa kwa hao 70 kwaelezea utume wa Kristo kwa mataifa. Kadiri ya wataalamu wa Maandiko Matakatifu utume wa mitume 12 unawekwa wazi siku ile ya Karamu ya mwisho. Huku kutumwa kwa hao 70 kuna maanisha utume wa walei. Kwa hiyo utume huu unatuhusu sote  wabatizwa.

Ni upi utume wa walei? Kauli mbiu ya Yesu iko wazi - mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache. Na wajibu huu unajikita katika mambo makuu mawili: sala na utendaji. Kumbuka ule msemo – sali kama vile kila kitu kinamtegemea Mungu na fanya kazi kama vile kila kitu kinakutegemea wewe. Hapa ndipo ubatizo wetu unawapata wajibu rasmi. Tukumbuke kuwa sisi sote ni wamisionari. Katika kutekeleza hayo, Yesu anaweka wazi sifa za hao mitume na utume wenyewe – upole na unyenyekevu na anaweka wazi wajibu rasmi akisisitiza kuwaponya wagonjwa – lengo ni kuutangaza ufalme wa Mungu. Yesu anawaagiza wawekeze katika Injili na kujiepusha na mahangaiko ya kawaida ya maisha. Anawakumbusha wategemee nguvu za kimungu katika utendaji. Nguvu hii ya Mungu ndiyo inayowezesha yote hayo.

Taarifa ya ushindi ya wale waliotumwa inaonesha ushindi wa nguvu ya Mungu. Ni kielelezo ya kile tunachokiona katika somo la kwanza. Katika somo hili twasikia habari juu ya Yerusalemu iliyo hai na ambayo wote waweza kupata uhai mpya - kunyonya na kunywa. Somo laongea juu ya ujio wa ufalme wa Mungu hapa duniani katika Yerusalemu. Ili hayo yawezekana yahitajika roho mpya na moyo mpya. Mtume Paulo katika somo la pili anajivunia ushindi unaoletwa kwa msalaba wa Kristo – Kristo mzima, anajivunia Kristo. Anasema wazi anayejivuna na ajivune katika Kristo – 1 Kor. 1:31; 2 Kor. 11:16-21. Majivuno yetu leo ni yapi au yako katika jambo lipi? Mtume Paulo alitimiza wajibu wa kwanza kabisa wa mbatizwa. Kuutangaza ufalme wa Mungu.

Katika mwaliko huu wa ufuasi kila kitu kinapata maana mpya katika ufalme wa Mungu. Yesu anaposema ufalme wa Mungu umekaribia anatoa mwaliko wa utendaji na mtazamo mpya wa maisha. Mwaliko wa Yesu kama  tubuni na kuiamini injili, mpende adui yako,  kama mkono wako unakukwaza ukate, ni afadhali kuingia ufalme wa Mungu u kigutu kuliko kuukosa ni mwaliko wa kufanya mabadiliko na kuwa tayari kuutangaza ufalme. Maisha mapya ya Mtume Paulo baada ya kuitwa yaendelee kutupa changamoto. Katika kitabu ‘Yesu wa Nazareti’ cha Papa Mstaafu Benedikto XVI, anasema kuwa upya na upekee wa habari ya Yesu ni kwamba daima Mungu anatualika tutende sasa. Toka hapa twaweza kuelewa hitaji haraka la utendaji kadiri ya mafundisho ya Yesu kuhusu ufalme. Tumesikia dominika iliyopita, anayetaka kunifuata na akaangalia nyuma hafai kwa ufalme.

Katika Ebr. 3:13 – tunasoma neno hili‘bali mfarijianane moyo kila siku iwezayo kuitwa ‘leo’ asije mmoja wenu akadanganywa na dhambi na kushupaa moyo’. Kwa maana hii asikiaye sasa mwaliko huu au asomaye neno hili anatakiwa kutenda sasa. Huu ndio mwaliko tuupatao katika injili ya leo. Wajibu wa ufuasi unakuwa hai na kuwajibishwa kama yule aliyesikia ujumbe huu miaka 2000 iliyopita au miaka 10 iliyopita. Kwake Kristo ufalme wa Mungu uliongoza maisha yake na ushuhuda wake na anatualika kwa ujio wake kila siku. Sisi tunamgeukia Mungu tukisema – ufalme wako ufike. Lakini Mungu anatugeukia na kusema kupitia Kristo, ufalme wa Mungu upo kati yetu. Usingoje wala kusubiri. Karibu. Ujumbe wa Neno la Mungu katika Mk. 1:15 – wakati umefika, na ufalme mwa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini injili bado unabaki ujumbe hai kama ulivyotamkwa na Yesu mwenyewe. Mungu na watu wake watudai kuuweka katika matendo.  Tumsifu Yesu Kristo.

04 July 2019, 14:09